Search This Blog

Friday, May 18, 2012

TANZANIA BWANA: ETI NSAJIGWA AMEISHA? SOMA SABABU 5 KWANINI NAAMINI NSAJIGWA BADO NI HAZINA YANGA.

Shedrack Nsajigwa akifanyaiwa mahojiano na mchezaji mwenzie Shabaan Kado

Tanzania ni moja ya nchi zilizojaliwa neema barani  Afrika
 kama si Duniani kwa ujumla.
Hakuna kitu kinachoisumbua nchi yetu kama kuwepo kwa watu kwenye maeneo wasiostahili, watu wasiokua na sifa na uwezo ndio wamejazana kwenye sekta nyeti hapa nchini.


Hayo madudu ndio hasa yanasababisha uchumi wa nchi yetu unashuka kila kukicha, hivi karibuni baada ya mchezo baina ya watani wa jadi hapa nchini Simba na Yanga kumalizika kwa Yanga kupokea kipigo cha mabao 5:0 kuliibuka mambo mengi sana hasa kwenye klabu ya Yanga (leo sitazungumzia mapambano yanayoendelea kati ya wanaojiita wazee wa Yanga na viongozi waliopo madarakani ).

Kwenye mchezo huo mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi aliibuka nyota wa mchezo je kuna anayebisha juu ya hilo? Jibu ni hakuna, sasa kilichonisikitisha ni baada ya kusoma habari kibao za kutoa kontena la lawama kwa baadhi ya wachezaji kama vile Nurdin Bakari na Shadrack Nsajigwa eti hawastahili kuichezea tena Yanga viwango vyao vimeisha,jamani kiwango cha mchezaji kinaisha kwenye mchezo mmoja?
 Hayo ni mazungumzo ya wanaojiita wadau wenye sauti ndani ya Yanga ambao hutoa mapendekezo ya nani anatakiwa kuachwa na nani anatakiwa kusajiliwa, baada ya kusikia maoni ya juu ya kuachwa kwa beki na nahodha Nsajigwa nilipigwa na bumbuwazi, kwa mtazamo wangu hata kama wangetakiwa kubaki wachezaji wawili tu ndani ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao Nsajigwa angekua mmojawapo, kwanini?

1. Kushushwa kiwango, kustaafishwa na Okwi


Shadrack anahukumiwa kwa kushindwa kumkaba Okwi, hili mimi nalifananisha na mwizi kuingia kwenye ofisi na kuiba halafu umuhukumu aliyekuwepo ofisini pasipo kujiuliza huyo mwizi kaingiaje mpaka ndani ya ofisi wakati kuna walinzi nje na mapokezi? Kwanini usijiulize kwanza hilo, mfano huu unafanana kabisa na kesi ya Nsajigwa, baada ya kujiuliza Okwi alikuwa anaipataje mipira ya hatari na kwanini Simba walikuwa wanashambulia kupita upande mmoja wa kushoto, mimi nadhani tatizo lilikuwa  ni la timu nzima kushindwa kuja na mpango mkakati wa kuizuia Simba kutengeneza mashambulizi upande huo, kwa kifupi Nsajigwa hakushuka kiwango kwenye mchezo dhidi ya Simba bali siku hiyo mfumo mzima wa timu ulikwama, hata kama ingekuwa mchezaji anatakiwa kustaafishwa kwa kushindwa kumkaba mchezaji wa timu pinzani basi leo Fernando Torres angekuwa kashamstaafisha Nemanja Vidic na kina Messi na Ronaldo wangekua wameshawastaafisha mabeki wote wa La Liga.


2. Wahusika kutokuwa na malengo ya mbali


Nsajigwa ni mmoja wa wachezaji wachache ambao ukiwa nao kwenye timu unatakiwa kumshukuru mungu, lakini tatizo la kuwa na watu ama viongozi wasiokuwa na maono linapelekea kuchukulia vitu kirahisi rahisi tu, ngoja nikupeni mfano ulio hai mwaka jana Simba walimstaafisha kiungo Nico Nyagawa kwa nguvu huku akiwa bado na msaada mkubwa kwenye timu tena naye alikua ni nahodha kama ilivyo kwa Nsajigwa, faida ya uwepo wa Nsajigwa kwenye timu ni zaidi ya kucheza jamani, kurudisha heshima kwa wachezaji vijana kutokana uwepo wa kaka yao, pia ni bahati kuwa na mchezaji ambaye ni rahisi kuambukiza siri ya mafanikio kwa wenzake na mwisho katika hili kuna aliyewahi kujiuliza kwanini kina Giggs na Scholes pale Man Utd, Carragher pale Liverpool wanaendelea kuwepo? Je ni kwasababu wana viwango vikubwa kushinda vijana waliopo kwenye hizo timu?, jamani muda mwingine baadhi ya wachezaji hulelewa ili waje wawe hazina hapo baadae, ila kwasababu vilabu vyetu vinaongozwa na wanasiasa na watu wasiokuwa na sifa za kuviongoza hawaoni kama wachezaji kama Nsajigwa wanaweza kuendelea kuwepo klabuni kwa ajili ya kuwalinda na kuwatunza vijana wapya.


3. Kumbadilishia majukumu


Yaani hakuna mtu pale klabuni anayeweza kuona kwamba Nsajigwa bado ni hazina kiwanjani ? Javier Zanetti wa Inter Milan anaweza kutumika kuuelezea umuhimu wa Nsajigwa kwasababu wote ni ma-wing back, namna ya kuendelea kuvuna matunda yao hawa jamaa ni kuwapunguzia majukumu kiwanjani, mfano kuna aliyewaza nini kitatokea kama Shadrack atapewa jukumu moja tu kiwanjani la kukaba ama kushambulia tu, kwa mtazamo wangu ili kuendelea kumfaidi Nsajigwa si kumstaafisha bali ni kumpunguzia majukumu kutokana na umri wake kuwa mkubwa.


4. Kuja kuwa sehemu ya benchi la ufundi.


Narudia tena kwasababu asilimia kubwa ya wanaojihusisha na vilabu hivi hawana Mitizamo ya mbali, Mipango na mikakati ya kuviendeleza hivi vilabu kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine basi njia pekee wanayoiona ni kuwafukuza wachezaji, kumbe wanaweza kuwekeza kwa wachezaji hawa kwa ajili ya faida ya baadae kwa klabu, wachezaji kama Pawasa, Matola, Salvatory Edward na Nsajigwa wanaweza kuendelea kuwepo na kupatiwa kozi za ukocha ili baadae waje wazifundishe hizo klabu.

Namalizia hivi :
Shadrack Nsajigwa bado yupo yupo kwanza!

No comments:

Post a Comment