NGORONGORO HEROES KWENDA SUDAN MEI 2
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) inatarajia kuondoka kesho (Mei 2 mwaka huu) kwenda Sudan kwa ajili ya mechi dhidi ya Sudan itakayochezwa Mei 5 mwaka huu.
Msafara wa Ngorongoro Heroes utakaokuwa na watu 28 ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Kambi utaondoka saa 8.45 mchana kwa ndege ya Kenya Airways.
Ngorongoro Heroes itaagwa rasmi kwa kukabidhiwa Bendera ya Taifa kesho (Mei 2 mwaka huu) saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Wengine katika msafara huo ni wachezaji na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Kim Poulsen. Mechi hiyo ya marudiano namba 16 itachezwa kwenye Uwanja wa Khartoum kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa za Sudan.
Iwapo Ngorongoro Heroes ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 3-1 itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza na Nigeria ambayo yenyewe imefuzu moja kwa moja kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo.
Mechi ya kwanza itachezwa Julai 28 jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika Nigeria kati ya Agosti 10, 11 na 12 mwaka huu. Fainali za U20 kwa Afrika zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria.
MECHI KUCHANGIA TWIGA STARS SASA MEI 6
Mechi maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie itachezwa sasa itachezwa Mei 6 mwaka huu badala ya Mei 4 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi hiyo, imesogezwa mbele kwa siku mbili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kujitokeza kuchangia Twiga Stars. Awali ilikuwa ichezwe Ijumaa ambayo ni siku ya kazi, hivyo imesogezwa hadi Jumapili ambayo ni siku ya mapumziko.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni ambapo viingilio kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu ni sh. 2,000, VIP C na B itakuwa sh. 5,000 wakati VIP A ni sh. 10,000.
Twiga Stars ambayo kwa sasa haina mdhamini na kambini katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani kujiandaa kwa mechi ya mashindano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia.
Timu hizo zitapambana Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa na kurudiana Juni 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mshindi atashiriki fainali za AWC zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
RUFANI YA AFRICAN LYON KUJADILIWA MEI 2
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana Mei 2 mwaka huu kujadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na klabu ya African Lyon.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu inailalamikia TFF ikipinga uamuzi uliofanywa na Kamati yake ya Ligi juu ya kuvunjika kwa pambano la ligi hiyo kati ya Azam na Mtibwa Sugar lililochezwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Katika rufani yake, Lyon imedai uamuzi uliofanywa na Kamati ya Ligi ya TFF haikuwa sahihi, kwani haukuzingatia kanuni za ligi hiyo kuhusu timu inayogomea mchezo.
Kamati hiyo chini ya Kamishna Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana inatarajia kufanya kikao chake kuanzia 8 mchana.
PONGEZI KWA TIMU YA SIMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Simba kwa ushindi wa mabao 3-0 ambao iliupata juzi (Aprili 29 mwaka huu) dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan katika mechi ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Dar es Salaam.
Ushindi huo umetokana na ushirikiano uliopo kuanzia kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama wa klabu hiyo na Watanzania kwa ujumla.
Ni imani ya TFF kuwa Simba haijabweteka kwa ushindi huo na badala yake sasa inajipanga kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa nchini Sudan ili kuondoa Al Ahly Shandy kwenye michuano hiyo na kusonga mbele.
TFF kama kawaida itaendelea kutoa ushirikiano kwa Simba ili kuhakikisha inafika mbali kwenye mashindano hayo, na ikiwezekana kuandikika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa Kombe la Shirikisho.
PAZIA LIGI KUU VPL KUFUNGWA MEI 5
Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itafikia tamati Mei 5 mwaka huu kwa bingwa kujulikana ambapo timu zote 14 siku hiyo zitakuwa uwanjani.
Klabu kongwe za mpira wa miguu nchini Simba na Yanga zitakutanisha timu zao katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nayo Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha na Ruvu Shooting itacheza na Villa Squad katika Mabatini, Mlandizi.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Coastal Union na Toto African itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, African Lyon na JKT Ruvu (Uwanja wa Manungu, Morogoro), Azam na Kagera Sugar (Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro).
Kwa mujibu wa kanuni namba 4(2)(c) ya Ligi Kuu ya Vodacom, timu tatu za mwisho katika msimamo wa ligi zitashuka daraja. Tayari Moro United na Polisi Dodoma zimeshashuka, iliyobaki itajulikana baada ya mechi za Jumamosi ambazo zote zitaanza saa 10 kamili jioni.
MIKOA SITA YAOMBA UENYEJI LIGI YA TAIFA
Mikoa sita imeshaomba kuwa wenyeji wa Ligi ya Taifa itakayochezwa katika vituo vitatu tofauti. Ligi hiyo inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inatarajia kuanza baadaye mwezi huu.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kukutana wakati wowote kupitia maombi hayo kabla ya kufanya uamuzi wa vituo na tarehe ya kuanza ligi hiyo.
Mikoa iliyoomba vituo ni Dar es Salaam, Kigoma, Lindi, Mara, Shinyanga na Singida.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment