Search This Blog

Tuesday, May 1, 2012

NIYONZIMA: SIONDOKI YANGA

KIUNGO mahiri wa Yanga, Haruna Niyonzima Fabregas, amewahakikishia mashabiki kwamba ana mwaka mwingine mmoja (siku 365) wa kuvaa jezi katika timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani kama asipopata timu nje ya nchi na wala vuguvugu la watu kujiuzulu halimhusu.

Hata hivyo Mnyarwanda huyo amekiri kwamba mambo yalikwenda ndivyo sivyo msimu huu wa Ligi Kuu Bara, lakini wataing'ang'ania Simba Jumamosi ijayo kulinda heshima yao kama wachezaji na hadhi ya klabu.

Haruna amekuwa akihusishwa na kuondoka Yanga hasa baada ya mwanachama aliyemnunua Rwanda, Bin Kleb, kujiuzulu kwenye nafasi zote za uongozi na kukaa kando.

Sababu nyingine inayotajwa kutaka kumkimbiza mchezaji huyo Yanga ni ukweli kuwa klabu hiyo imekosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa barani Afrika mwakani.

"Siwezi kuondoka Yanga kienyeji, nina mkataba nao, kitakachotokea ni kwamba kama nitapata timu nje ndipo nitaondoka, lakini vinginevyo nitakuwa hapa kwa msimu mwingine tena," alisema.

"Hayo mambo mengine ya viongozi wamejiuzulu mimi kama mchezaji hayanihusu, kazi yangu mimi ni uwanjani na kutekeleza mkataba wangu."

Akizungumzia mechi ya Simba, alisema: "Tutaing'ang'ania Simba na tutaifunga kutunza heshima yetu kwa vile hatuna cha kupoteza na msimu umeshaharibika kwa upande wetu.

"Tunataka ushindi tu, hakuna cha ziada na tutafanya kazi kwelikweli uwanjani, ndicho kitu pekee tunachoweza kuwalipa mashabiki wetu kwa sasa.".

source:mwanaspoti

No comments:

Post a Comment