Search This Blog

Wednesday, May 2, 2012

SHOMARI KAPOMBE NA FELIX SUNZU WATAKIWA TP MAZEMBE

SIKU mbili baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, kiraka wa Simba, Shomari Kapombe na mshambuliaji wa timu hiyo, Felix Sunzu wameanza kupigiwa hesabu na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Habari ambazo zimekuwa zikizagaa na kuripotiwa na vyombo vya habari, zinadai kuwa klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ilituma mawakala wake kwa ajili ya kuangalia soka ya wachezaji hao ambao ni vipenzi vya mashabiki wa Simba kwa sasa.

Katika mchezo wa Jumapili, Kapombe 'alivalishwa viatu' vya Juma Nyoso aliyekuwa nje kwa kadi nyekundu na kuimudu kikamilifu nafasi hiyo katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Chanzo cha habari kilipasha kuwa ujumbe wa watu wawili ulitumwa kwa ajili ya kuwaona pamoja na kufanya mazungumzo ya awali na wachezaji hao kwa ajili ya kujiunga na timu yao.

Habari zilizopatikana baadaye zilisema kuwa Kapombe anabanwa na mkataba na hata hivyo imeelezwa kuwa Simba haiwezi kumwachia kwa sasa wakati Sunzu amekataa kuondoka na lengo lake ni kuona Simba inatwaa ubingwa wa Bara na Kombe la Shirikisho.

"Unajua wale mabwana walikuwa wanawataka hawa wawili, lakini Sunzu amekataa ila Kapombe hajawa muwazi, sasa sifahamu msimamo wake, lakini inawezekana anabanwa na mkataba," kilisema chanzo hicho ndani ya Simba.
 
 Kapombe alipotafutwa kuzungumzia suala hilo,  ambapo alisema mpaka sasa hana taarifa zozote za jamaa hao wa TP Mazembe.

"Kaka sina taarifa zozote za hao jamaa, wala hajanifuata ila wakinifuata mimi nipo tayari kuzungumza nao, kwa sababu ni mazungumzo,"alisema Kapombe.

Klabu ya TP Mazembe tayari imeishawachukua wachezaji wawili kutoka Simba ambao ni Mbwana Samata na Patrick Ochan, pia timu hiyo imemchukua mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania, Thomas Ulimwengu.

No comments:

Post a Comment