MSHAMBULIAJI wa Villa Squad, Nsa Job, amepata ulaji wa kwenda kufanya majaribio Sweden kutokana na kiwango chake kuwa juu kwa sasa.
Mwenyekiti wa Villa, Uledi Ramadhani, alisema Nsa alimwambia kuwa anatarajia kuondoka nchini mara baada ya ligi kumalizika kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Alisema awali Nsa alimwambia anaenda Ulaya bila kuwatajia sehemu aendayo lakini watu wake wa karibu wakamwambia anakwenda Sweden ambako ametafutiwa timu na wakala wake.
“Nsa aliniambia anatarajia kwenda Ulaya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa mara baada ya ligi kumalizika ingawa hakuniambia ni nchi gani anaenda, ila wenzake waliniambia amepata timu Sweden.
“Binafsi namuunga mkono kwa hilo kwa kuwa sisi tunapenda maendeleo, hivyo tutafurahi tukiona amefanikiwa kwa kuwa ni njia mojawapo ya kuitangaza Villa,” alisema Uledi.
Nsa alipotafutwa kuzungumzia mpango huo alikiri: “Kweli naondoka kati ya tarehe sita au saba mwezi wa tano, nakwenda Sweden kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.”
Nsa aliyejiunga na Villa Julai, mwaka jana akitokea Yanga, amefanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa katika michezo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara akiwa amefunga mabao kumi mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment