Search This Blog

Monday, May 21, 2012

MAPINDUZI: LLOYD NCHUNGA APINDULIWA NA WAZEE WA YANGA - TARIMBA ARUDISHWA - TFF YASEMA HAIYATAMBUI MAPINDUZI

WANACHAMA 721 wa Yanga wamemtimua Mwenyekiti wao Lloyd Nchunga na Kamati yake ya Utendaji ikiwa ni pamoja na kuwataka wasijaribu kufika makao makuu ya klabu hiyo kwa kuwa hawana imani nao.

Katika mkutano wa dharula wa wanachama wa Yanga uliofanyika jana kwenye uwanja wa Kaunda huku  Mwenyekiti wa mkutano huo akiwa Bakili Makele na Katibu  akiwa Ibrahim Akilimali ambaye ni Katibu wa Baraza la Wazee, walitangaza hali ya hatari kwa Mwenyekiti wao Nchunga kwa kumtaka asikanyage klabuni hapo na iwapo atafika kwa nguvu basi atahatarisha maisha yake.

"Kuanzia kesho kila tawi litoe wanachama watano kuja kulinda hapa klabu na posho tutawalipa, hatutaki kumuona mtu anaitwa Nchunga na watu wake hapa,"alisema Makele ambaye pia ni mwenyekiti wa Vijana wa Yanga na kushangiliwa kwa nguvu na wanachama waliohudhuria mkutano huo huku gari mbili za Polisi wa FFU zikiwa nje zikizunguka zunguka na askari kanzu ambao walikuwa ndani kulinda amani.

Hata hivyo mkutano huo ambao ulianza sa 6:15 mchana na kumalizika saa 8:45 mchana ulifanyika kwa utulivu.

"Tunamuagiza Katibu (Selestine Mwesigwa) kesho (leo) aende akatuletee Bank Statement (taarifa ya benki) ya klabu ya Yanga, ni haki yetu tunataka kujua kilichoingia kilichotumika, ili kudhibiti hii akaunti ya Yanga na Nchunga asiweze kutoa tena fedha, ifungwe,"alisema Makele.

Alisema,"nawaomba wanachama msitishe kwa muda zoezi la kulipia kadi zenu mpaka hapo tutakapowatangazia," alisema huku akishangiliwa na kundi la wanachama walioudhuria mkutano huo.

Mkutano huo ulimrushia shutuma mbali mbali Nchunga na kudai kuwa ndio chanzo cha Yanga kupokonywa pointi tatu kwenye mechi yao na Coastal Union na pia yeye ni chanzo cha kuisababishia madeni makubwa klabu hiyo.

Wanachama hao kwa pamoja waliazimia kuwasilisha maazimio ya kikao chao kwa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) na kwa msajili wa vyama vya michezo wilaya ya Ilala ili waende kwenye uchaguzi mdogo.

Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahimu Akilimali alisema,"kuna barua tumempa Nchunga juzi ambayo alipewa masharti na mmoja wa wanachama wetu mzito kidogo akimtaka kutekeleza yafuatayo, kwanza afanye ukaguzi wa mahesabu ya Yanga kuanzia mwaka 2006 hadi 2012, pili akubali kila baada ya miezi minne aweke wazi hesabu za Yanga kwenye vyombo vyote vya habari na mwisho aendeshe zoezi la kura za maoni ndani ya siku 90  klabu iendeshwe kibiashara au tuendelee kuwa na mfumo huu na amesema kama Nchunga atakubali kufanya hivyo vyote, atarudisha majeshi yake moja kwa moja na Yanga haitakuwa tena na shida ya fedha."

"Na pia zoezi la usajili linaanza rasmi kesho (leo), mwanachama wetu wa siku nyingi Abbas Tarimba atakuwa mshauri wa Kamati ya usajili ambayo ni Kamati maalumu tuliyoiunda na kuandaa timu kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Kagame,"alijinasibu huku akishangiliwa kwa nguvu na wanachama hao.

KATIBA KIKWAZO
Nchunga hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila majibu, lakini hata hivyo kwa mujibu wa katiba ya Yanga ibara ya 22 (2) inazungumzia mkutano wa dharura, ambapo inasema endapo nusu ya wajumbe (wanachama) wamewasilisha ombi kwa Kamati ya Utendaji kwa maandishi, Kamati ya utendaji italazimika kuitisha mkutano kwa kipindi kisichozidi siku 30 baada ya ombi hilo kuwasilishwa.

Kipengele cha (3) kinasema wito wa mkutano unatakiwa utolewe angalau siku 15 kabla ya mkutano wakati kipengele cha (4) kinasema ajenda, nyaraka muhimu zipelekwe kwa wanachama siku saba kabla ya mkutano.

Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, pia mkutano wa dharula kwa ajili ya kutoa maamuzi yoyote ikiwa ni pamoja na kutokuwa na imani na kiongozi yoyote unatakiwa kuhudhuriwa na nusu ya wanachama hai wa klabu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alipoulizwa Yanga ina wanachama wangapi alisema Yanga ina wanachama hai 12,000.

Hata hivyo mmoja wa wanachama wa klabu hiyo ambaye hakutaka kutajwa kwa madai kuwa sio msemaji wa Yanga alisema,"huu mkutano wa dharula ulioitishwa ni batili kwa kuwa idadi ya wanachama wa Yanga haikutimia kwa ajili ya mkutano wa dharula."

Alisema,"ili mkutano wa dharula ufanyike unatakiwa uhudhuriwe na nusu ya wanachama wa Yanga, klabu yetu  ina wanachama 14,000 na nusu yake ni 7,000 na pia mkutano wa dharula kama umeitishwa lengo likiwa ni kutokuwa na imani na kiongozi yoyote inatakiwa nusu ya wanachama waliopiga kura siku ya uchaguzi mkuu itimie."

Alisema,"uchaguzi uliomuweka madarakani Nchunga ulihudhuriwa na wanachama 3116 na nusu yake ni 1558, hivyo idadi ya mkutano wa leo haijatimia kwa hiyo ni mkutano batili.

"Mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano ni Mwenyekiti sio mwanachama wala kikundi cha watu, baraza la Wazee kama hawana imani na Mwenyekiti walitakiwa watafute saini za wanachama 1558 ambazo ni nusu ya wanachama na kuwasilisha kwenye kamati ya utendaji ambayo itafanya mchakato wa kuitisha mkutano wa dharula ambao utapiga kura za kutokuwa na imani na Mwenyekiti au kiongozi yoyote na kuitisha uchaguzi mdogo."

Kwa upande wao Shirikisho la Soka Tanzania kupitia kwa Ofisa Habari wake Boniface Wambura alisema TFF imeweka wazi kanuni zake na Yanga wenyewe wanajua hilo.
"Kama wanachama watamuondoa mwenyekiti wao, itabidi wafanye uchaguzi, kwa sababu TFF haifanyi kazi na kamati za muda hilo lipo wazi na kama wanataka kumtoa kiongozi ni lazima wafuate taratibu za katiba yao."

Wakati huo huo; idadi ya wajumbe waliojiuzuru Kamati ya Utendaji ya Yanga imefikia saba baada ya jana Mohamed Bhinda, Pascal Kihanga na Mzee Yusuf kutangaza kukaa pembeni. Wengine ni Davis Mosha, Ally Mayai, Seif Magari, na Abdallah Bin Krebu.
source:mwananchi.co.tz

4 comments:

  1. Kama inavyosema katiba ya Yanga, "Bishana mpaka kufa!"

    ReplyDelete
  2. nasikitika kuona soka la tz linaharibiwa na watu wachache ambao hawajui chochote kuhusu soka.timu ikifungwa ama kuwa na misukosuko kidogo hambayo haiepukiki ktk soka lolote lile wanataka viongozi wajiuzulu!jamani tubadirike wabongo tuache ushamba,tangu lini soka likawana mapinduzi ya uongozi?upuuuuuuuuuuuzi mtupuuuuuuuuuuuuuuuuuuu.................!!!!!!!!!!!.Wazee wa yanga badirikeni wale kwenye soka hamjui kitu kazi yenu kushkiria mila za ushirikina ktk mpira jambo ambalo ktk soka la sasa halipewi nafasi,ndo maana timu zetu hazifanyi kitu ktk mechi za kimataifa.

    ReplyDelete
  3. yanga oovyo, mnaacha soka la vijana mnakimbilia malumbano mnaboa

    ReplyDelete
  4. yanga mbona hamuwazi maendeleo hizo siasa acheni ...ni lini mtatoa mchezaji atakayecheza ulaya au atakuja kwa siasa mf drogba sio siasa ni uwekezaji,wekezeni kwa vijana kwani mnashindwa nini nyie kila mwaka ubingwa ..ubingwa mbona hamna jipya niliipenda yanga lakini nimeamia azam..by jeremia,udom

    ReplyDelete