Search This Blog

Friday, May 4, 2012

DSM DERBY COUNTDOWN: PAPIC SIMBA WATATUFUNGA - KUISHTAKI YANGA FIFA

KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic amesema mazingira ya sasa ndani ya klabu yake hiyo yanatoa fursa kubwa kwa Simba kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Jumapili.

Simba na Yanga zitavaana keshokutwa kwenye mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Awali mechi hiyo ilipangwa kupigwa kesho, lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliamua kusogeza mbele kwa siku moja baada ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kutoa agizo la kurudiwa kwa mchezo kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar.

Akizungumza jana, Papic aliyeacha kuifundisha timu hiyo tangu Aprili 24 baada ya kibali chake cha kufanya kazi kuisha muda wake alisema Simba ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika pambano dhidi ya Yanga kutokana na wachezaji wa Simba kuwa katika hali nzuri kisaikolojia.

"Nitakwenda uwanjani kuangalia pambano hilo kama mpenzi tu wa soka, lakini kimsingi Simba ina nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo tofauti na Yanga, hii ni kutokana na hali halisi ya mazingira ya timu hizi kwa sasa.

"Sifahamu vizuri kinachoendelea huko wakati huu, lakini ukweli Yanga haijatulia, sina sababu ya kukuelezea zaidi nadhani unafahamu hilo hasa kwa kutumia kigezo cha kujiamini, Simba ina nafasi kubwa ,"alisema Papic bila kufafanua zaidi.

Katika hatua nyingine, Papic alisema yupo katika hatua za mwisho kabla ya kuwasilisha malalamiko Shirikisho la soka la Dunia Fifa baada ya uongozi wa Yanga kupuuza madai yake ya kutaka alipwe takribani sh 24 milioni malimbikizo ya mishahara yake ya miezi miwili.

"Kila kitu nimekiandaa, nafikiri Jumapili niwatawasilisha Fifa malalamiko yangu, sikupenda kuchukua uamuzi wa kuishtaki Yanga, lakini sasa nitalazimika kuchukua hatua zaidi baada ya madai yangu kupuuzwa,"alisema Papic.

Alisema licha ya mara kadhaa kufanya jitihada za  kuwasiliana na uongozi wa Yanga kupitia simu ya mkononi bado amekuwa hapati ushirikiano kitendo kinachomfanya aone ni kama dharau kwake.

"Ninavyokuambia mara ya mwisho kuwasiliana na Mwenyekiti wa Yanga ni Aprili 25, tangu hapo nikimpigia hapokei simu yangu, sasa nielewe vipi kama sio dharau?," alihoji Papic.

No comments:

Post a Comment