Search This Blog

Thursday, May 3, 2012

DSM DEBY COUNTDOWN: TUTAWAFUNGA YANGA NA KUCHUKUA UBINGWA ASEMA MILOVAN

KOCHA Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic ametamba kikosi chake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayofikia tamati keshokutwa.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Zanzibar ambapo timu yake imeweka kambi, Cirkovic alisema kutokana na hali ilivyo, kikosi chake kinampa moyo kwamba kinaweza kushindana katika michuano yoyote.


“Kikosi changu kiko vizuri na kina uwezo wa kushinda mechi yoyote inayokuja mbele yake hata ya marudiano dhidi ya Al Ahly Shandy itakayofanyika Sudan,” alisema.


Simba inakabiliwa na mechi ya marudiano ya raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya timu hiyo inayotarajiwa kufanyika Sudan katikati ya mwezi huu ambapo timu hiyo imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kushinda mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


"Nina imani na kikosi changu kutokana na hali iliyokuwa nayo...nina uhakika kitafanya vizuri dhidi ya Yanga na hata katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho," alisema Cirkovic.


Simba itacheza na Yanga mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara ambapo ili kutwaa ubingwa,

inahitaji pointi moja, kinyume na hapo inabidi izidishe maombi ili Azam ipoteze mechi ya
mwisho dhidi ya Kagera Sugar, kwa vile nayo ikishinda na Simba ikifungwa zitakuwa
zinalingana pointi na hivyo bingwa atalazimika kuamuliwa kwa tofauti ya mabao.

Cirkovic alisema katika mchezo huu anaomba sapoti ya mashabiki wa Simba akiwataka wajitokeze kwa wingi uwanjani kuwashangilia ili kuzidisha nguvu ya kutwaa ubingwa ambao msimu uliopita waliukosa kwa tofauti ya bao moja.


“Nawathamini sana mashabiki, na kushinda kwetu hata katika mechi zilizopita ilitokana na kuja kwao kwa wingi uwanjani kutushangilia na wengine waliopata nafasi walithubutu hata kusafiri mikoani kuhakikisha wanashuhudia timu ikicheza, nafarijika sana na mashabiki wangu,” alisema.


Simba inatarajiwa kurejea siku hiyohiyo ya mechi ambapo itafikia moja kwa moja uwanjani ikitokea Zanzibar.

No comments:

Post a Comment