KOCHA wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', Kim Poulsen amewapa majukumu ya ufungaji mabao kiungo mshambuliaji, Haruna Moshi 'Boban' na mshambuliaji Mbwana Samata katika kikosi chake kilicho kambini hivi sasa.
Katika mazoezi ya kikosi hicho yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Kim amekuwa akiwachezesha pamoja Boban anayeichezea Simba na Samata anayekipiga katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuonyesha maelewano makubwa na wakupachika mabao mengi ya kiufundi.
Kim amekuwa akikigawa kikosi chake katika timu mbili na kuwachezesha pamoja, Samata anayetumika kama mshambuliaji namba tisa na Boban anayetumika kama mshambuliaji namba 10.
Kitendo cha Kim, kumtumia Boban kama mshambuliaji badala ya kiungo kama asili yake, kimeonekana kuwa na faida, kwani kimetoa fursa kwa chipukizi wa JKT Ruvu, Frank Domayo kutumika kama mpishi namba nane.
Naye Mrisho Ngasa ambaye amekuwa akimtumia kama winga wa kushoto kama ilivyo kwa Mwinyi Kazimoto anayecheza winga wa kulia, mara kadhaa amekwaruzana na Kim kutokana na tabia yake ya kung'ang'ania kukaa pembeni badala ya kuingia ndani kuwasaidia viungo Domayo na Shaabani Nditi hasa pale mashambulizi yanapoelekezwa kwao.
Katika safu ya ulinzi, kocha huyo Mdenmark amekuwa akimpanga Aggrey Morris kama mlinzi wa kati akisaidiana na Kelvin Yondan anayecheza namba nne huku Shomari Kapombe akiimarisha ulinzi wa kulia kama ilivyo kwa Waziri Salum anayedhibiti nafasi ya beki wa kushoto.
Picha halisi ya kikosi cha kwanza cha Kim kutokana na mazoezi hayo ni kipa Juma Kaseja, Shomari Kapombe,Wazir Salum, Kelvin Yondan, Aggrey Morris, Shaaban Nditi, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Haruna Moshi'Boban', Mbwana Samata na Mrisho Ngasa.
Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) inatarajiwa kutua leo saa 10 jioni kwa ndege ya Air Malawi tayari kwa kuivaa Taifa Stars kesho katika pambano la kimataifa la kirafiki litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Taifa Stars itaikabili The Flames ikiwa ni maandalizi ya mechi yake ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan, huku pia Malawi ikitumia mechi hiyo kujiandaa kupambana na Kenya.
Viingilio katika mtanange wa Taifa Stars na Malawi vitakuwa Sh 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, Sh 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, Sh 15,000 kwa jukwaa la viti maalumu B na C na Sh 20,000 kwa jukwaa la viti maalumu A.
No comments:
Post a Comment