Search This Blog

Sunday, May 13, 2012

BAKARI MALIMA JEMBE ULAYA - 3

Nonda Shabani 'Papii ' watatu waliosimama kutoka kushoto,Bakari Malima wapili waliochuchumaa kutoka kushoto

*Awaaga wazazi wa Nonda, aamua kuondoka Kinshasa

*Akumbushia mkasa wa madawa ya kulevya ulivyompata
*Alipotua airport, akajikuta yuko mikononi mwa polisi
Na  Saleh Ally
WIKI ILIYOPITA tuliishia Malima akiwa ameshauriwa kuondoka Kinshasa kwa kuwa haukuwa mji salama kutokana na watu wengi kumuomba fedha kila walipokuwa wakimuomna. Je, atachukua uamuzi gani? Endelea.
BAADA ya kupewa ushauri ule na mdogo wake na Nonda, niliona kilikuwa ni kitu kizuri na hasa kwa kuwa alizungumzia suala la usalama. Nikachukua uamuzi wa kurejea nyumbani maana sikutaka kupatwa na matatizo tena.
Kabla ya hapo, miaka kama minne iliyopita nilikuwa nimeingia katika matatizo makubwa sana ya kuhusishwa na uingizaji wa madawa ya kulevya nchini. Nikaona nirejee nyumbani ili kuepuka kuingia kwenye matatizo hayo tena.
Nikafunga safari na kurejea Dar es Salaam salama, lakini nilifanya hivyo baada ya kuagana vizuri na familia ya Nonda ambao niliishi nao kwa kipindi kifupi lakini kama ndugu wa damu.
Nilianza maisha upya, lakini kabla sijaendelea mbele labda niwarudishe nyuma kidogo kuhusiana na sakata kuhusiana na kuhusishwa na uingizaji wa madawa ya kulevya nchini.
Kipindi hicho nilikuwa nimeshaingia mkataba wa kuichezea Vaal Professional ya Afrika Kusini. Kabla ya Yanga kunikubalia, nililazimika kurejea nyumbani na kumuacha Nonda Shabaan anacheza huko. Siku mimi natua Sauz, nikaambiwa alishaondoka wiki mbili kabla kwenda Uswiss alikopata timu.
Nilijiunga na Vaal baada ya mwisho wa msimu kukakataa kusaini Yanga na kuamua kwenda Afrika Kusini ambako niliingia mkataba wa kuichezea timu hiyo. Nilicheza vizuri tu na nikawa napata namba, mwisho nikawa mchezaji tegemeo.
Maisha yalienda vizuri kabisa, nilipewa nyumba nzuri tu nje kidogo ya jiji la Johannesburg. Baadhi ya Watanzania walikuwa wanafikia pale, wakati fulani kuna dada mmoja alikuwa ni mfanyabiashara akawa anakuja anafikia pale, baada ya siku kadhaa anaondoka na kurejea Dar es Salaam.
Ikawa hivyo kawaida na nilimzoea kwa kuwa wakati mwingine nami nilimpa maagizo kupeleka nyumbani. Kwa kifupi akawa ni rafiki na mtu ambaye tunaheshimiana sana.
Siku moja, wakati anaondoka nikaamua kumsindikiza uwanja wa ndege. Lakini ilikuwa hivi, mzunguko wa kwanza ulikuwa umeisha, maana yake na mimi nilikata tiketi ya kurudi Dar es Salaam siku iliyofuatia. Huyo dada alikuwa anaondoka siku hiyo.
Tulipokuwa pale uwanja wa ndege akatokea jamaa mmoja ambaye alionekana ananijua vizuri, akanisalimia halafu akaniuliza kama nilikuwa nasafiri, nikamuambia nilikuwa namsindikiza dada yangu. Basi alikuwa na mzigo mkononi, kiboksi kidogo kimefungwa vizuri sana, akaomba yule sister amsaidie kukifikisha Dar.
Sikuona kama kuna shida hata kidogo, lakini akamuambia hakuwa na sababu ya kumpa  palepale, badala yake akamuomba aingie kwa kufuata taratibu nyingine, yeye angempelekea ule mzigo ndani ya ndege ili ampunguzie bugudha ya kubeba.
Basi, wote wawili hatukuona kama ni kitu kibaya kwa kuwa alisema kuna mtu angekuja uwanja wa ndege Dar kuja kukipokea. Kiliandikwa jina hadi namba ya simu, kweli yule jamaa alifanya hivyo. Mimi sikujua zaidi kilichoendelea na nilirejea nyumbani na kuendelea na maandalizi ya safari kurudi Dar siku iliyofuata.
****************
Nikiwa Johannesburg sikujua kilichokuwa kinaendelea. Mambo yalikuwa yamebadilika kabisa Dar es Salaam, yule dada alishikwa na kile kifurushi, kumbe ndani yake kulikuwa na madawa ya kulevya.
Alipohojiwa akasisitiza haukuwa ni mzigo wake, alieleza namna alivyokabidhiwa na mtu ambaye ananijua mimi. Hivyo kilichofuatia ni askari polisi kumuweka chini ya ulinzi.
Pia hakukuwa na mawasiliano yoyote kati yangu naye, hivyo sikujua kama alikuwa amekutwa na matatizo makubwa kama hayo. Mimi niliendelea kujiandaa na safari ya kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya mapumziko kabla ya kurudi Afrika Kusini kuendelea na ligi nikiichezea timu yangu ya Vaal Professional.
Siku iliyofuata nilifika uwanja wa ndege mapema, bado sikujua lolote lililokuwa linaendelea Dar es Salaam. Nilichofanya ni kununua zawadi kwa ajili ya watu wangu. Hivyo nilikuwa na mabegi yangu yaliyosheni vizuri.
Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (DIA), nilijaribu kufanya mambo yangu haraka haraka ili niwahi kutoka kwenda nyumbani. Maana nilikuwa nimepamiss sana, nilipomaliza kila kitu wakati ninatoka, mtu mmoja alinifuata na kuniuliza kama mimi ndiyo Bakari Malima, nikajibu ndiyo.
Akanisema ana mazungumzo na mimi, sasa nikaona kama ananichelewesha tu. Nikataka kwenda lakini akaniomba tusogee pembeni. Akajitambulisha yeye ni askari, akataka kugua mabeki yangu. Sikuwa na ujanja, nikakubali na tujaongozana kwenda vyumbani.
Kule, niliwakuta askari wengine ambao walikuwa wamevaa kiraia. Wakaniuliza kama namjua fulani wakitaja jina la yule dada, nikawaeleza ndiyo na jana yake nilimsindikiza uwanja wa ndege alikuwa anakuja Dar. Wakanieleza mwanamke amekamatwa na madawa ya kulevya na mimi nijahusika.
Hivyo, kitu cha kwanza walitaka kupekua mizigo yangu upya. Mimi nilikuwa bado kama sielewi, niliona ni kama sinema au ninaona. Nikawaruhusu waanze kufanya ukaguzi huku nikiangalia kwa umakini mkubwa nikihofia nisije nikabambikiwa kitu au nilishabambikiwa.
MALIMA amekushawekwa chini ya ulinzi na tayari ameanza kupekuliwa kuhusiana na madawa ya kulevya. Je, nini kitakutwa kwenye mabegi yake? ENDELEA KUFUATILIA.

1 comment:

  1. wengine wote ambao huwa mnasafiri, hapa kuna somo, usipokee wala usibebe mzigo wa mtu ambao hujui ndani kuna nini.

    ReplyDelete