NI orodha ndefu ya wachezaji waliohama kutoka Simba kwenda Yanga na kutoka Yanga kwenda Simba, tangu enzi za akina Emanuel Mbele 'Dubu', lakini ni wachache waliong'ara kote kote.
Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Zamoyoni Mogella, Method Mogella (sasa marehemu), Hamisi Gaga (sasa marehemu), Deo Njohole, Akida Makunda, Alphonce Modest, Monja Liseki, Shaaban Ramadhan, Eustace Bajwala, Joseph Katuba (sasa marehemu) wote hao ni baadhi ya wachezaji waliotoka Simba na kwenda kucheza Yanga.
Maulid Dilunga 'Mexico', Ezekiel Greyson 'Jujuman', Justin Mtekere (wote marehemu), Ally Yussuf 'Tigana', Yussuf Macho, Godwin Aswile, Ismail Suma, Steven Nemes, Nico Bambaga, Bakari Malima, Willy Martin, Edibily Lunyamila, Mtwa Kihwelo, Omar Hussein 'Keegan', Athumani China, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Mohamed Banka na Amri Kiemba wote pia ni baadhi ya wachezaji waliotoka Yanga na kucheza Simba. Banka na Kiemba wamo kwenye kikosi cha msimu huu (2009/10) pia.
Athumani China akiwa Yanga, aliifunga Simba bao la mapema, dakika ya tatu, Oktoba 9, mwaka 1991 kwenye Ligi ya Muungano, wakati watoto wa Jangwani wakiibuka na ushindi wa 2-0. Bao la pili la Yanga lilifungwa na Abubakar Salum 'Sure Boy' dakika ya 54.
China tena aliifunga Yanga akiwa Simba, lilikuwa bao la pili katika ushindi wa 4-1 kwa Wekundu wa Msimbazi, Julai 2, mwaka 1994. Ally Yussuf Suleiman 'Tigana', pia alifunga mabao kote kote, Thomas Kipese kadhalika naye aliwafunga Simba na baadaye Yanga.
Akida Makunda aliihama Simba kuingia Yanga akiwa hana kumbukumbu ya kufunga bao kwenye mechi ya watani, lakini mara baada ya kutua kwa wana Jangwani aliingia kwenye orodha ya nyota waliofunga mabao kwenye mechi baina ya wababe hao wa soka ya Tanzania.
Ilikuwa Februari 21, mwaka 1998 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati huo ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, wakati Makunda alipofunga bao lililoelekea kuwatoa Yanga kifua mbele kwenye mchezo huo, dakika ya 46.
Lakini Athumani Macheppe alizima shangwe za wana Yanga zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo huo kumalizika kwa bao lake safi.
Sahau kuhusu Akida, kama yupo mchezaji ambaye aliyewapa raha mashabiki wa timu zote hizo, basi ni Said Nassor Yussuf Mwamba (pichani), maarufu kama Kizota enzi zake, aliyefariki dunia Februari 11, mwaka 2007. Kizota ni mchezaji aliyewasisimua kwa namna yake mashabiki wa Yanga na Simba kutokana na mabao yake.
Kizota alifariki dunia baada ya kugongwa na gari eneo la Veterinary, akiwa anatoka kushuhudia mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, Raundi ya Awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textil de Pungue ya Msumbiji. Alitoka kwa huzuni uwanjani siku hiyo baada ya kushuhudia timu yake ya zamani, Simba ikitolewa na wageni kwa mikwaju ya penalti 3-1, kufuatia sare ya jumla ya 2-2.
Mchezo wa kwanza Msumbiji, Simba ililazimisha sare ya 1-1 na marudiano nayo pia walibanwa kwa sare aina hiyo hiyo, hivyo kufanya mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti. Ntota ya timu ya kiwanda cha nguo Msumbiji ndiyo iliyong'ara jioni hiyo.
Kama kuna miaka ambayo Kizota alifanya vitu vya 'babu kubwa' kwenye soka ya Tanzania, basi ni 1993, kwani mapema tu mwaka huo aliibuka mfungaji bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda, akiiwezesha Yanga pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwafunga wenyeji, SC Villa.
Lakini pia, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Tanzania. Yote tisa, kumi ni pale Kizota alipofunga mabao mawili peke yake, wakati Yanga inaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam.
Ilikuwa ni Machi 27, mwaka huo 1993, wakati Kizota alipomchambua kipa hodari nchini enzi hizo, Mwameja Mohamed katika dakika za 47 na 57.
Simba ikielekea kulala 2-0, shukrani kwake Edward Chumila (naye marehemu pia) aliyewafungia Wekundu wa Msimbazi bao la kufutia machozi, dakika ya 75.
Baada ya kipigo kikali cha mabao 4-1, Julai 2, mwaka 1994, Yanga ilivunja kikosi ikiwafukuza karibu nyota wake wote wa kikosi cha kwanza kwa tuhuma za kuhusika kuihujumu timu katika kipigo hicho kilichotokana na mabao ya George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi, bao la kufutia machozi la Yanga likifungwa na beki imara, Constantine Kimanda.
Kati ya nyota waliotupiwa virago Yanga ni Kizota, ambaye kutokana na makali yake wakati huo, akiwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania na miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi kilichochukua Kombe la Challenge nchini Kenya, Simba wakamwambia: "Usipate tabu Said, njoo upumzike huku".
Kizota alitaka kuwaonyesha Yanga kwamba, walifanya kosa kumwacha na katika mchezo wa marudiano baina ya watani hao wa jadi wa Ligi Kuu ya Bara, Oktoba 4, 1995, Yanga ikiwa inaelekea kabisa kushinda mchezo huo 1-0, Said Mwamba alitibua furaha ya wana Jangwani dakika ya 70 kwa kufunga bao safi la kusawazisha.
Yanga ilitangulia kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake mahiri enzi hizo, Mohamed Hussein 'Mmachinga' dakika ya 40. Bao la Kizota liliwachanganya Yanga na dakika tisa baadaye, wakapachikwa bao la pili. Safari hiyo alikuwa ni Mchunga Bakari 'Mandela' aliyewaambia wana Jangwani; kutangulia si kufika.
Baada ya msimu huo, Yanga walikiri kosa lao na wakaenda kumpigia magoti Kizota arejee nyumbani. Kwa sababu Kizota alikuwa anaishi nyumba ya pili kutoka klabu ya Yanga, akiishi na mkewe Tosha, Mtaa wa Jangwani, hivyo ilikuwa rahisi kumrubuni na kurejea nyumbani.
Na aliporejea Yanga, Kizota aliifunga tena Simba. Ilikuwa Novemba 9, mwaka 1996, katika sare ya ajabu ya watani, ya mabao 4-4 mjini Arusha.
Kizota aliifungia Yanga bao la kusawazisha lililofanya sare ya 3-3 katika dakika 70, baada ya awali Kipese kuifungia Simba, dakika ya saba, Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 28, Ahmed Mwinyimkuu kuifungia Simba la pili dakika ya 43, kabla ya Dua Said kufunga la tatu dakika ya 60 na Mustafa Hoza kuisawazishia Yanga kwa kujifunga dakika ya 64.
Sanifu Lazaro aliifungia Yanga bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 75, lakini walishindwa kulinda lango lao na kuruhusu bao la dakika za lala salama, lililofungwa na Duwa Said dakika ya 90, hivyo kuwa sare ya 4-4.
Kizota alijiunga na Yanga mwaka mwaka 1988, akitokea timu ya Shirika la Posta la Tabora, enzi hizo likijulikana kama Posta na Simu, wakati akicheza kama kiungo.
Baada ya kung'ara akiwa na Yanga, msimu wa 1988 ulipomalizika alichukuliwa na Al-Jazira ya Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. Akiwa Abu Dhabi katika timu yake mpya, Kizota alikutana na aliyekuwa nyota wa timu ya Taifa ya Malawi, Lawrence Waya, ambaye alikuwa winga machachari sana enzi zake. Kwa pamoja Kizota na Waya waliifanya timu yao kuwika mno katika soka ya Uarabuni.
Kutokana na vitu vyake vya uhakika, Kizota alikubalika mno na mashabiki wa soka Abu Dhabi, jambo ambalo lilifanya Waarabu waanze kumrubuni abadili uraia na kuwa raia wa huko. Ghiliba hizo hakupewa Kizota peke yake, bali hata Waya.
Kizota aliingiwa na ghiliba hizo na kuanza kufanyiwa taratibu za kupewa uraia, lakini wakati taratibu zikifanywa, mwanasoka huyo aliomba likizo ya kurejea nyumbani Tanzania kuoanana na familia yake na ndipo alipobadili mawazo ya Uarabu. Hiyo ilikuwa ni mwaka 1989.
"Hakuna kingine ni Yanga tu, nilipofika tu viongozi wakasema wananihitaji sana, hivyo nikaamua kubaki Yanga," aliniambia Kizota nilipozungumza naye mwaka 1999. Kizota aliingia kwa makeke, safari hiyo hakuwa kiungo, bali alihamia kwenye nafasi ya ushambuliaji na kufanikiwa kuipeleka Yanga kileleni kwa mabao yake.
Hata hivyo, viongozi wa timu yake baada ya kuona kimya kimezidi, walimtaka haraka sana kurejea. Alitumiwa ujumbe wa simu ya maandishi (Fax) ambao aliupuuza, lakini baadaye alifuatwa na viongozi hao walioondoka naye kurejea Abu Dhabi.
Kizota aliondoka nchini akiwa anaongoza kufunga mabao na Ligi imefikia ukingoni, huku Yanga ikihitaji pointi chache tu kutangaza ubingwa, jambo ambalo liliwezekana, licha ya yeye kuondoka na vijana wa Jangwani kurejesha taji walilopokonywa na Coastal Union ya Tanga mwaka 1988.
Kizota aliishi Uarabuni hadi mwaka 1991, aliporejea kupumzika na kuikuta Yanga ikiwa katika hali mbaya, soka ya Tanzania inatawaliwa na watani wao wa jadi, Simba, ambayo mwaka huo wakati anarejea (Simba) ilikuwa imetangaza ufalme wa soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame.
"Kama nilivyokwambia naipenda sana Yanga, nikaamua kubaki, lakini jamaa (Al-Jazira) walikuwa wakinitaka nirejee haraka sana, nikawadanganya naumwa, wakati wananitumia fedha za matibabu, kumbe mie niko safi kabisa," aliniambia Kizota, aliyehitumu elimu yake ya msingi mwaka 1981 katika shule ya Mabatini, Tabora alikozaliwa.
Kizota aling'ara Yanga tangu mwaka huo, akiiwezesha kutwaa Kombe la Kagame mwaka 1993, kufika fainali ya michuano hiyo mwaka 1992, Nusu Fainali nchini Sudan mwaka 1994, kabla ya 1994 kuhamia Simba.
Aliporejea Yanga 1996, alicheza kwa misimu miwili zaidi kabla ya mwaka 1998 kutimkia Al-Nasar ya Oman. Alikaa huko msimu mmoja tu, kabla ya kurejea nchini katikati ya msimu wa Ligi Kuu na kujiunga na timu iliyokuwa Daraja la Kwanza, Kariakoo United ya Lindi, ambako akiwa na wakongwe wenzake kama Mustafa Hoza waliipandisha Ligi Kuu.
Baada ya kuipandisha timu hiyo, Kizota alirejea Yanga ambako aliiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame tena Uganda mwaka 1999, ingawa kutokana na umri wakati huo, alirejea kucheza nafasi ya ulinzi. Hadi anafariki dunia, Kizota alikuwa mume wa Tosha na baba wa watoto wawili, Hamim na Rabii.
imeandikwa na Mahmoud Zubeiry - http://bongostaz.blogspot.com/
Mwenyezi Mungu akulaze mahali pea Kizota
ReplyDelete