Search This Blog

Monday, April 2, 2012

Haruna vs Haruna.

Klabu za Simba na Yanga zimekuwa na upinzani ambao unaonekana kuwa tofauti na upinzani wowote ule wa timu za soka hapa Duniani. Tofauti hii inatokana na ukweli kwamba kati ya vilabu hivi hakuna anayekubali kuna klabu yenye kitu kizuri kushinda mwenzake . Mfano Yanga wakiwa na Kocha mzungu, Simba nao watapambana kufa na kupona ili na wao walete kocha mzungu. Ilifikia hatua mpaka Mojawapo kati ya hizi timu ilituma zawadi ya jezi yake kwa waandaji na watangazaji wa kipindi cha Soccer Africa kinachorushwa na televisheni ya Supersports , wenzao walipojua kuwa watani wametuma jezi hawakutaka kubaki nyuma na wao wakatuma fasta . Huo ndio upinzani wa watu hawa.
Upinzani huu uliingia mpaka kwenye majina ya wachezaji msimu huu .


Simba kwa muda mrefu wamekuwa na kiungo anayeitwa Haruna Moshi , Yanga msimu huu wakasawazisha na wao wakamleta Haruna wao , kiungo toka Rwanda Haruna Niyonzima . Haruna Moshi ana jina la utani ambalo wengi wanamfahamu kama Boban ( jina la kiungo wa zamani wa Ac Milan na timu ya Taifa ya Croatia) , Haruna wa Yanga naye analo jina la utani akifahamika kama Fabregas ( jina la Kiungo wa Kimataifa wa Hispania ).
Wachezaji hawa wote ni muhimu sana kwa timu zao  hasa kutokana na sifa moja kuu ambayo inawatofautisha na wenzao , wana akili nyingi sana za mpira pamoja na kuwa na vipaji halisi tofauti na wenzao wengi.
Moja ya mambo ambayo yamekuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa Simba na Yanga ni ubishi  wa Haruna yupi mkali kati ya hawa ,wa Simba au wa Yanga.
Hakuna mwenye uwezo wa kutoa jibu la haraka juu ya nani kati ya hawa aliye bora kuliko mwenzie kwa kuwa wachezaji hawa hawajafanana kila mmoja ana sifa zake zinazomfanya awe tofauti na mwenzie .
Haruna Niyonzima ni mtu mwenye uwezo wa ziada anapokuwa na mpira mguuni kwake kwa maneno mengine ni dribbler mzuri na anasifa zote za kiungo wa kati . Ana composure au kwa lugha nyepesi anapopata mpira hana papara , ana inteligence ambayo ni muhimu kwa viungo wote . Haruna Niyonzima pia ana jicho kali la pasi muhimu jambo abalo limekuwa moja ya sifa zake kuu tangu akiwa na APR ya Rwanda alikotoka . Kikubwa zaidi ya hapo Haruna Niyonzima ni mchezaji wa timu , si mbinafsi na siku zote anatambua kuwa uwanjani yeye ni muunganishaji wa timu hivyo anachezesha kila upande .
Haruna Moshi Boban kwa upande wake ni moja ya wachezaji wachache sana wenye vipaji halisi ambao wanaonekana kwenye ulimwengu wa soka la Tanzania . Kama Niyonzima. Ana akili nyingi sana za mpira kichwani mwake , hana papara wala haogopi kupewa mpira na wenzie na moja ya sifa zake kubwa ni jinsi anavyojua kuulinda mpira ukiwa miguuni mwake ambako ni nadra sana kupoteza mpira akiwa na na pia n nadra sana kwake kutoa pasi ya mkaa. Boban pia ana jicho la ziada la pasi pamoja na magoli ambayo amekuwa akifunga . Haruna Moshi pia ana mawazo ya ziada ya kujua wenzie wanawaza nini na hivyo anafanya kama wanavyotarajia , mfano mzuri ni "one-two" aliyocheza na Emmanuel Okwi iliyopelekea bao la kwanza kwa Simba wakati wa mchezo dhidi ya Es Setif .



Kwa kutazama sifa zao ni vigumu sana kujua nani mkali kati ya hawa viungo wawili .
Hata hivyo , wana tofauti zao kwa maana ya sifa ambazo mmoja anayo na mwingine hana .
Haruna Niyonzima ana sifa ya ziada ya uongozi kuliko Boban. Ukitazama michezo mingi ya Yanga unaweza kudhani kuwa Niyonzima ni nahodha kwa jinsi anavyokuwa akiwaelekeza wenzie cha kufanya wanapokuwa na mpira na hata pale anapokuwa na mpira yeye mara nyingi huwa anawaelekeza jinsi ya kuchukua nafasi ili aweze kuwapenyezea mipira kiurahisi . Hii ni sifa ambayo Boban hakujaliwa . Boban hazungumzi na mtu uwanjani na anapokuwa na mpira ndio wakati pekee ambao anawasiliana na wenzie tena anafanya hivyo kwa ishara na sio kwa mdomo tu.
Kitu cha pili ambacho Fabregas anacho ni kujitolea kwa timu . Haruna niyonzima anacheza kama yuko vitani labda ni kwa sababu yeye ni raia wa Rwanda na watu wa huko wana personality ya kuwa aggressive yaani wapambanaji kutokana na mazingira ambayo wamekulia . Haruna Moshi Boban hana work rate kubwa na mara nyingi huwa anachoka mapema sana . Pamoja na hayo Boban ana tabia ya kuwasusia wenzie pale wanapokuwa wanafanya kinyume na jinsi anavyotaka yeye . Aina ya wachezaji kama Boban huwa na kasumba ya kufikiri kwamba wenzie wana kipaji na uwezo kama alio nao yeye na ndio maana haoni haja ya kuwaelekeza wenzie kufanya kile ambacho yeye ameweza kufikiri.
Ukitazama jinsi wachezaji hawa wanavyochangia kwenye timu zao kupata matokeo mazuri unaweza kugundua tofauti nyingine kubwa ya wachezaji hawa. Haruna Niyonzima amekuwa akilaumiwa kuwa na kawaida ya kutoa pasi zisizo na maana kitaalamu zikifahamika kama pasi mraba au square passes , mara nyingi pasi ambazo zinaenda pembeni na sio mbele ambako timu inaelekea yaani diagonal au penetration passes . Ukimwangalia Boban yeye ana wastani mzuri wa kutoa pasi nzuri za mwisho ambazo zina madhara kwa timu pinzani na mara nyingi amekuwa akitengeneza mabao mengi ya Simba . Hata hivyo Niyonzima hafanyi makusudi kutoa pasi zisizo na madhara , anafanya hivyo kutokana na mfumo ambao Yanga wanatumia . Kiutamaduni Yanga inacheza soka tofautii na wanalocheza Simba , Yanga wana soka kama la Kiingereza au kama la Man United ambao mara nyingi hawana mambo mengi wao ni pasi tatu wameshafika langoni mwako huku wakitumia sana mawinga kama njia muhimu ya kupata mabao na hata washambuliaji walio nao ni aina ya washambuliaji waviziaji ambao mara nyingi hungojea krosi . Hivyo mchezaji kama Niyonzima ndio pamoja na kipaji chake sio mchezaji wa Yanga kihalisia . Boban kwa upande wake yuko mahali sahihi. Kwani Simba wanapenda aina ya soka kama la Arsenal au la kihispania ambalo mara nyingi viungo ndio wanaopewa kipaumbele . Na ndio maana hata ukiangalia kihistoria Yanga imekuwa timu ambayo inekuwa iking'arishwa sana na mawinga kina Lunyamila , Ngasa , Sanifu Lazaro na wengineo huku Simba wao wakitakatishwa sana na viungo mafundi kina Husein Marsha , Boban hii leo , Mtemi Ramadhani miaka hiyo na wengine wengi. Na kingine unachokiona kwa Niyonzima na Boban mara nyingi Simba ina bahati ya kupata wachezaji mafundi ila wavivu na si watu wa kazi tofauti na wenzao Yanga ambao mara nyingi wana Historia ya kupata wachezaji wapambanaji .
Mwisho wa siku hakuna jibu la moja kwa moja linaloweza kujibu ubora wa mmojawapo kati ya Haruna Fabregas na Haruna Boban kwani wote wana sifa za kufanana na pia kila mmoja ana upekee wa aina yake ambao mwenzie hana hivyo Haruna na Haruna wote kwa pamoja ni viungo Bora kwa soka la Tanzania kwa sasa.

3 comments:

  1. unawaza mbali sana kaka ,big up,www.twitter.com/haile19

    ReplyDelete
  2. Kaka umekosa kazi?,kwanini usiombe kazi magazeti ya udaku,yaani unafananisha hilo garasa na Niyo!!!.

    ReplyDelete
  3. Kaka Boban yuko juu sana kuliko Niyonzima hata mafisango alisema Boban yuko juu na huyo ni mrwanda mwezie, huyo anaesema Boban hasara ana chuki binafsi, kiukweli hata mafisango yuko juu kuliko huyo Niyonzima

    ReplyDelete