Search This Blog

Monday, April 30, 2012

Azam FC yaifunga Toto Afrika na kufikisha pointi 56


Azam FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu kwa kufikisha pointi 56 baada ya kuifunga Toto African 3-1 huku mshambuliaji John Bocco akiwa amejihakikishia nafasi ya kuondoka na kiatu cha dhahabu msimu huu kwa kufikisha magoli 17 na kuvunja rasmi rekodi ya klabu kwa magoli kwa mchezaji kwa msimu.
Mchezo huo uliovutia hisia za mashabiki wengi wa soka ulichezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Chamazi ulishuhudia kandanda safi kutoka kwa wachezaji wa Azam FC na kuwaacha midomo wazi wapinzani wa Azam FC.
Mshambuliaji Kipre Tchetche alikuwa wa kwanza kufungua kalamu ya magoli kwa kufunga goli la kwanza kwa kichwa katika dakika ya 10 akimalizia kazi nzuri ya Mrisho Ngassa.
Goli hili liliichanganya safu ya ulinzi ya Toto Africa na kupelekea Azam FC kutumia nafasi hiyo kupata bao la pili katika dakika ya 19 lililowekwa wavuni na Kipre aliyecheza vizuri na Bocco.
Dakika ya 33 Bocco alifunga bao la tatu baada ya mabeki wa Toto pamoja na kipa wao Mustafa Mbarouk  kupoteana.
Bocco amefikisha mabao 17 na kuzidi kupaa mbele ya wafungaji wengine wa ligi kuu, vile vile ameivunja rekodi ya msimu uliopita iliyowekwa na Ngassa aliyemaliza akiwa na mfungaji bora kwa kuwa na mabao 16.
Baada ya kipigo cha 3-0 dakika ya 35 Toto walifanya mabadiliko alitoka golikipa Mustafa Mbarouk nafasi yake ikachukuliwa na Sunga Ramadhan ambaye hakufungwa hadi mchezo kumalizika.
Kipindi cha pili Azam FC walicheza kwa kutulia wakiwa wako mbele kwa 3-0, walitumia muda huo kucheza mpira wa kiwango cha juu huku wakifanya mashambulizi.
Wachezaji Abdi Kassim na Gaudence Mwaikimba waliingia kuchukua nafasi za Ibrahim Mwaipopo dk 61 na Bocco dk 78, Toto African walitoka Emmanuel Swita na Kamana Salum nafasi zao zikachulikuliwa na Phabian James na Tete Kanganga.
Mabadiliko hayo yaliimarisha timu ya Toto na kupata bao la pekee katika dk ya 87 kupitia kwa Anyina Darlington, na kumaliza mchezo Azam FC wakipata ushindi wa 3-1.
Kwa ushindi huo Azam FC wanafikisha pointi 56 na kuwa ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu chini ya Simba SC inayoongoza kwa kuwa na pointi 59 endapo Azam FC wataifunga Kagera katika mchezo wa mwisho na Simba ikapoteza mchezo wao kwa Yanga, Azam FC anayo nafasi ya kutwaa ubingwa huo.

Azam FC, Mwadini Ally, Waziri Salum, Agrey Morris, Luckson Kakolaki, Erasto Nyoni, Michael Bolou Kipre, Ibrahim Mwaipopo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Kipre Tchetche, Bocco na Ngassa.

source: azamfc.co.tz

No comments:

Post a Comment