Akizungumza mjini Dar es Salaam, Poulsen alisema kama TFF itampa taarifa ya kumtaka kuachia ngazi, basi atafanya hivyo mara moja.
“Mimi siwezi kulazimisha kufanya kazi Tanzania kama sitakiwi, ila ukiona bado nipo basi fahamu kwamba mwajiri wangu ananihitaji. Siku wakiamua niondoke, basi nitafanya hivyo mara moja," alisema Poulsen na kuongeza:
“Mimi ni mwajiriwa wa TFF, siyo Kamati ya Utendaji na TFF haijanipa barua ya kuacha kazi, kwa mantiki hiyo mimi bado ni mwajiriwa halali wa TFF.”
Kamati ya Utendaji ilitaka kocha huyo aondoke na moja ya sababu ni kushindwa kuleta mabadiliko katika soka la Tanzania badala yake amekuwa akichangia kiwango cha Tanzania kushuka.
Akijibu tuhuma hizo Poulsen, alisema kamwe hawezi kufanya kazi kwa matakwa ya baadhi ya watu, na kwamba yeye ndiye kocha anafahamu saikolojia ya wachezaji pamoja na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
“Tatizo la Tanzania ni suala la Samata kutoitwa kwenye kikosi cha Stars, hilo mimi halinipi shida ila ukweli ni kwamba siwezi kuacha kazi kwa sababu ya matakwa ya baadhi ya watu,” alifafanua Poulsen.
Poulsen alirithi mikoba ya Mbrazil, Marcio Maximo mwaka juzi na tangu kuwapo kwake kazini soka ya Tanzania imekuwa ikishuka siku hadi siku, kiasi cha Watanzania kumkumbuka Mbrazil aliyeipeleka Stars katika fainali za kwanza za CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
No comments:
Post a Comment