Search This Blog

Wednesday, March 14, 2012

Mkimbizi toka Burundi anayefanya mambo makubwa huko Coventry City.

Maajabu hutokea sana duniani na huwa yanatokea pale ambapo mtu hategemei.
Moja ya vitu ambavyo vimeiwasha Ligi daraja la kwanza nchini England maarufu kama The Coca Cola Championship ni kijana toka nchini Burundi Gael Bigirimana ambaye anachezea klabu ya Coventry City.
Hadithi ya Gael Bigirimana ilianzia kwenye Supermarket moja kwenye jiji la Coventry ambako alikwenda na kaka yake kununua vitu vya kutumia nyumbani. Wakati wakiwa Supermarket Gael alikiona kituo cha kuendelezea vipaji vya wachezaji wachanga cha Coventry na pasipo kusita alikwenda moja kwa moja hadi kwenye kituo hicho.
Siku iliyofuata Gael alikwenda kwenye kituo hicho kuomba kuandikishwa . Makocha wa kituo hicho walimuambia kuwa wana mfumo maalum wa kuandikisha watoto ambapo ni lazima mchakato wa scouting ufuatwe . Gael hakukata tamaa , alichofanya ni kuwapa makocha hao maelekezo ya shule anayosomea huku akiwa na matumaini kuwa watakuja kumtazama , wakati anaondoka mmoja wa makocha alimuuliza kama amekuja na vifaa akawaambia ndio japo alikuwa akiwadanganya.

Siku iliyofuata walimpa Gael nafasi ya majaribio na majaribio ya siku moja yalitosha kuwaridhisha juu ya uwezo aliokuwa nao na tangu wakati huo mpaka hii leo Gael amekuwa mchezaji wa Coventry City.  Baada ya miaka 7 , Gael Bigirimana akiwa na umri wa miaka 18 alipata nafasi ya kuichezea Coventry kwenye mchezo wake wa kwanza na hadi sasa ameshacheza michezo 21 akiwa kwenye kikosi cha kwanza.

 Msimu huu Gael amepewa tuzo ya mchezaji kijana bora wa mwaka baada ya kuisaidia Coventry kwa uwezo wake mkubwa akicheza nafasi ya kiungo .Gael Bigirimana ni raia wa Burundi na alienda England na familia yake kama wakimbizi . Mwenyewe anasema alianza kucheza soka nyumbani kwao huko Bujumbura na jijini Kampala ambako aliwahi kuishi kwa muda .Tangu alipocheza mechi yake ya mwisho mwezi Januari mambo yalianza kumwendea vibaya baada ya kurudishwa kwenye kikosi cha vijana walio na umri chini ya miaka 19.

Kwa mtu mwingine angeweza kuchukulia hili kama pigo lakini Gael ambaye ni muumini wa dini ya kristo anaamini kuwa wote huu ni mpango wa Mungu uliolenga kumjenga zaidi kwenye maisha .Tangu akiwa mdogo ilikuwa inajulikana kuwa angeishia kuwa mcheza soka kutokana na kipaji alichokuwa nacho na wakati anaifuata familia yake nchini England mwaka 2004 alijua kuwa hiyo ndio nafasi pekee ya kutimiza ndoto zake na hakuangalia nyuma pale alipopata nafasi yake.

No comments:

Post a Comment