Search This Blog

Wednesday, March 28, 2012

MATCH REVIEW: CHELSEA 1-0 BENFICA - KOCHA JORGE JESUS ALIPOZIDIWA MBINU NA KIJANA DI MATTEO.




Chelsea inaweza kuwa sio nzuri kama ilivyokuwa hapo awali kama asemavyo Lampard lakini pamoja na kupanga kikosi cha kwanza kisichotarajiwa bado ilikuwa na ubora wa kutosha kuifunga Benfica ugenini  na kujiweka karibu na nafasi ya kufuzu nusu fainali .

Saa chache kabla ya mchezo Didier Drogba alisema kuwa Benfica ni timu ambayo hawawezi kuiogopa eti kwa sababu imeitoa United na mchezo ambao Benfica iliuonyesha ulidhihirisha ukweli uliokuwemo kwenye maneno ya Drogba kwani ilikuwa wazi, Benfica walicheza hovyo kuliko siku zote walizowahi kucheza kwenye robo fainali.
Kamari aliyojaribu kucheza Roberto Di Matteo ya kuwapumzisha wachezaji sita wa kikosi cha kwanza, wakiwemo wakongwe ambao walipambana kuitoa Napoli ilionekana kulipa baada ya Salomon Kalou aliyepangwa kwenye nafasi ya Didier Drogba kuipa Chelsea bao pekee la ushindi.

Mchezo huu kati ya Benfica na Chelsea ulikosa kasi ambayo Benfica walikuwa nayo kwenye raundi za mwanzo za michuano hii kwenye michezo ya nyumbani. Hata hivyo haukukosa matukio kadhaa ikiwemo kadi ya njano aliyopewa Raul Meireles ambaye alimchezea hovyo Nicolas Gaitan aliyekuwa anaelekea kuidhuru Chelsea. Tukio hili lilionekana kuleta uhai kwenye mchezo kwa ujumla kwani baaada ya hapa Benfica waliamka na kuanza kushambulia kwa kasi. Muda mfupi baadaye Chelsea walijikuta hatarini tena safari hii Bruno Cesar akipiga pasi ya juu ambayo ilimpita John Terry ambaye hata hivyo aliweza kufanya recovery ambayo ilimzuia Oscar Cardozzo aliyekuwa anaenda kumuona Petr Cech.

Benfica waliuanza mchezo wakitumia mfumo wa 4-2-3-1. Pablo Aimar alicheza karibu kabisa na Oscar Cardozo huku Alex Witsel akisaidiana na Javi Garcia katikati ya uwanja. Huu ulikuwa mfumo ambao karibu kila mtu akiwemo kocha wa Chelsea Roberto Di Matteo walitegemea kuuona toka kwa Benfica . Di Matteo naye aliteua mfumo ambao ulikuwa sahihi kuikabili Benfica. Alitumia viungo wakabaji wawili John Obi Mikel na Raul Meireles. Ramirez alielekezwa kufanya kazi kwenye upande wa kulia ili kumbana Emerson.

Wakati wa kipindi cha kwanza hakuna timu yoyote iliyoweza kuumiliki mchezo kwa nafasi zote, hata hivyo hali hii ilibadilika kwenye dakika za mwisho za kipindi hiki ambapo Chelsea walionekana kuja juu baada ya kuongeza kasi ya mashambulizi yao hasa kutokea pembeni mwa uwanja. Matokeo ya bila kufungana kipindi cha kwanza  yalionekana kumridhisha Di Matteo kwa kuwa hakutaraji kuona Benfica wakijibu mapigo kwenye kipindi cha pili.
Wenyeji walikuwa karibu kufunga baada ya mapumziko ambapo Benfica walishambulia lakini David Luiz aliokoa kwa kuondosha hatari kwenye mstari wa goli. Kabla mchezo haujaendelea sana Chelsea walikuwa hatarini kusababisha penati ambayo Benfica waliamini wameonewa baada ya John Terry kuonekana kuwa amenawa lakini mpira ulimgonga .

Mchezo ulibadilika sana baada ya hapa , hasa baada ya kufanya mabadiliko ya kumuingiza Frank Lampard kwenye nafasi ya Raul Meireles. Jorge Jesus kocha wa Benfica naye aliwabadili Pablo Aimar na Bruno Cesar na kuwaingiza Nemanja Matic na Rodrigo. Kosa kubwa alilolifanya Jesus ni kuingiza kiungo mkabaji wa pili akiamini kuwa anafanya hivyo kuua mashambulizi ya Chelsea.


Kuingia kwa Nemanja Matic kulimlazimu Alex Witsel kucheza pembeni kulia na hapo nguvu yote ya Benfica ikaondoka kwani walitawaliwa sana kwenye eneo la kati ya uwanja ambapo Chelsea walikuwa wakiingia ndani zaidi kutafuta nafasi. Chelsea ilipata bao lake ililostahili kwenye dakika ya 75 baada ya Ramires kukimbia pembeni na kumpa pasi Torres ambaye alimtafuta Salomon Kalou alipokuwa na kumpa pande safi alilo-finish kwa wepesi.

Baada ya mechi kocha wa Benfica alisema kuwa timu yake haikustahili kupoteza mchezo huu . Alikuwa sahihi lakini timu hii ya Ureno haikustahili kushinda pia . Chelsea walsafiri kwenda Lisbon huku wakiwa na mawazo ya sare vichwani mwao na Benfixca hawakuweza kuumiliki mchezo kwa njia ambayo ingeweza kuwapa ushindi. Di Matteo alifanya majaribio ambayo kwa upande wake yalikuwa na faida na kocha wa Benfica anaweza kuwa na hatia ya kuigharimu timu yake kwa kushindwa kuusoma mchezo vyema.

Kwa mchezo wa marudiano Benfica hawana budi kujaribu mfumo tofauti. Kumchezesha Rodrigo pembeni ya Cardozo kwenye safu ya ushambuliaji inaweza kuwa suluhisho . Alex Witsel ana uwezo mkubwa hilo halina ubishi ila tatizo kubwa ni jinsi anavyoua kasi ya mashambulizi na ili kupata ushindi London Benfica lazima wacheze mchezo wa kasi.

Nicolas Gaitan kwa upande wake amekuwa kwenye wakati mgumu ambao amekuwa akicheza chini ya kiwango lakini mechi dhidi ya Chelsea alicheza vizuri kiasi chake na kama Benfica watahitaji ushindi itabidi Gaitan aonyeshe uwezo wake wote.

No comments:

Post a Comment