MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba SC, Malota Soma ‘Ball Jagller’ amewataka wachezaji wa Simba kuwa na malengo ya kuwafunga mabao mengi wapinzani wao, ESS Setif ya Algeria katika mchezo wa Jumapili, ambao utakuwa wa kwanza wa Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Malota aliyekuwamo kwenye kikosi cha Simba SC kilichoitoa timu nyingine ya Algeria, Al Harrach mwaka 1993 katika Robo Fainali ya michuano kama hii, alisema kwamba wachezaji wa sasa wa timu hiyo wanatakiwa kujitambua na kufanya mambo kwa malengo.
Alisema wanatakiwa wajiwekee dhamira ya kuwafunga mabao angalau matano, ili hata wakipata matatu yatawasaidia katika mchezo wa jumla utakaohitimisha matokeo ya jumla na kuamua timu ya kusonga mbele.
“Sisi wakati wetu tunacheza, tulikuwa tunajiwekea dhamira ya kuwafunga hata mabao matano (Al Harrach), lakini huku tulipata matatu, tukaenda kwenye mchezo wa marudiano wakatufunga mawili kwao, tukawatoa kwa bao moja tu.
Kwa hiyo, nawaasa wachezaji wa Simba, wajitume sana kwenye mchezo huo, kwani wanacheza na timu ambayo ni kali na wasiifanyie mzaha,”alisema.
Mwaka 1993, Malota na nyota wenzake wa Simba enzi hizo kama Mwameja Mohamed, Kasongo Athumani, Twaha Hamidu, Fikiri Magosso, George Masatu, Hussein Marsha, Ramadhani Lenny, Abdul Ramadhan ‘Mashine’, Duwa Said, Michael Paul, George Lucas, Bakari Iddi, Razack Yussuf, Edward Chumila, Thomas Kipese na wengineo, walifikisha Simba fainali ya michuano hiyo na kufungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast 2-0.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Simba kufika fainali ya michuano ya klabu Afrika, ikiwa klabu ya kwanza nchini pia kufanya hivyo na wakati huu ni mwaka wa 19 tangu akina Malota wafanye mambo hayo adimu, klabu hiyo inajaribu kurudia historia, kikosi chake kikiwa na wachezaji ambao mwaka 1993 hata mimba zao zilikuwa hazijatungwa kama Shomari Kapombe, Gerald Mkude na Ramadhan Singano ‘Messi’.
Kapombe alisajiliwa kutoka kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka huu, wakati Mkude na Messi wamepandishwa kutoka timu B ya Simba katikati ya msimu.
Wakati Kapombe amekuwa akianza kwenye kikosi cha kwanza tangu mwanzo wa msimu, lakini Mkude na Messi wamekuwa wakitumiwa zaidi na kocha Mserbia wa Simba, Milovan Curkovic aliyeanza kazi mwishoni mwa mwa mwaka kana.
Nyota hao wamekuwa wakionyesha soka ya kuvutia kwenye kikosi cha kwanza cha Simba na kuna uwezekano wote wakapewa nafasi Jumapili kubeba jahazi la Simba SC.
Wakati huo huo, beki Juma Jabu hayumo kwenye orodha ya wachezaji walioingia kambini Simba hivi leo, kutokana na kuwa ni majeruhi. Zaidi ya hapo, wachezaji wengine wote wapo fiti na wapo kambini- tayari kuua mnyama.
No comments:
Post a Comment