Search This Blog

Wednesday, March 28, 2012

COASTAL UNION: YANGA WANABEBWA NA T.F.F


Uongozi wa Coastal Union umeilalamikia Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusitisha adhabu za wachezaji wa Yanga na kudai kuwa ina lengo la kuisaidia timu hiyo katika mechi dhidi yao.

Yanga inatarajia kumenyana na Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga Jumamosi hii. Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, Alfred Tibaigana alitangaza kusitisha adhabu za wachezaji watano wa Yanga kwa kutumia mamlaka aliyopewa na kanuni ya 129 ya kanuni za dhabu za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Wachezaji wa Yanga waliofungiwa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa kutokana na kuhusika katika vurugu kwa kumpiga mwamuzi Israel Nkongo wakati wa mchezo dhidi ya Azam wiki mbili zilizopita Stephano Mwasika (mwaka mmoja) na Jerry Tegete (miezi sita).

Wengine ni Nadir Haroub 'Canavaro' (mechi sita), Omega Seme na Nourdin Bakari ambao kila mmoja amefungiwa mechi tatu na watamaliza adhabu yao baada ya mechi ya Coastal.

Akizungumza  jana, Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Coastal Union, Salim Bawazir alisema: "Kanuni za kuendesha ligi ziko wazi wala haihitaji elimu ya chuo kikuu, kamati ya Tibaigana kuwaruhusu wachezaji wa Yanga kuwa huru ni kosa...

"Sheria ziko wazi ukimpiga mwamuzi adhabu iko katika sheria, ukipewa kadi nyekundu ipo sheria na wao wameadhibiwa kwa mujibu wa sheria, katika ligi hii kuna adhabu zimetolewa lakini kamati ya Tibaigana hajasema lakini kwa ajili ya kuisaidia Yanga kucheza na Coastal ndio sababu peke yake lakini sio sheria, keshokutwa, keshokutwa Yanga wakifungwa 2-0 na Coastal kamati ya nidhamu inaweza kuyafuta matokeo hayo kwa siku 14 wajue mabao yamefungwa namna gani kwa kweli TFF itizame sana kamati hizi," alisema.

Aliongeza: "Ndio maana kila siku napiga kelele TFF imewaondoa watu wa mpira eti kwa kukosa vyeti vya kidato cha nne matokeo yake tunashindwa kufuata sheria na maamuzi."

Kwa mujibu wa Tibaigana, ameamuru kusitisha adhabu iliyotolewa na kamati ya ligi kwani chini ya kanuni ya 129, mwenyekiti anayo mamlaka ya kusitisha utekelezaji wa adhabu yoyote ile pale anapoona kwamba ukiukwaji unaolalamikiwa hautaweza kupatiwa ufumbuzi haraka bila kuathiri haki za wale wanaokata rufani.

Alisema usitishwaji wa adhabu hizo ambao utadumu kwa siku 14 kuanzia tarehe ya kusitishwa huko una nia ya kutoa muda kwa sekretarieti ya TFF kuwasilisha rufani ya Yanga pamoja na maamuzi yanayohusiana na rufani hiyo mbele ya kamati, isikilizwe kabla ya kulitolea maamuzi.
 

1 comment:

  1. Inakera kwel make hko syo kuleta maendeleo bali nikuoneshana ubabe kati ya kamat na kamat. Kamat ya nidham imejchafua

    ReplyDelete