Soka la kimataifa lina sifa moja nayo ni umakini , kinachomtofautisha mchezaji wa daraja la chini , daraja la kawaida na daraja la juu ni umakini .Kila kitu kinachofanyika uwanjani kinahitaji umakini na unapokuwa makini utafanya kazi yako kwa ufasaha .
Mchezaji wa daraja la juu anahitaji nafasi moja kufanya yale yanayotarajiwa toka kwake na mchezaji wa kawaida huhitaji nafasi tano kufanya jambo moja la hatari na mchezaji wa daraja la chini kabisa ndio anaweza kupata nafasi kumi na asitumie hata moja.
Hii ndio ilikuwa tofauti kubwa kati ya Yanga na Zamalek Sc wakati timu hizi zilipokutana kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano ya Orange CAF Champions League kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.Kwenye kipindi cha kwanza Yanga walianza mchezo kwa kasi ya chini lakini walienda wakiongeza kasi kadri mchezo ulivyokuwa unaendelea kwa staili ambayo kwa lugha ya kigeni tunaweza kusema ‘they grew into the game’. Kasi ilikuwa ikiongezeka taratibu na Yanga wakawa wanatengeneza nafasi nyingi huku hali ya kujiamini kwa wachezaji ikizidi kupanda juu.
Zamalek wao walikuwa kama wanaisoma Yanga huku wakipanda mbele kwa kushtukiza. Zamalek walikuwa na mtu mmoja tu mbele huku wakiwa wamejaza wachezaji wengi kwenye eneo la kiungo na Razack Omotoyosi ambaye alikuwa ameachwa mbele peke yake alikuwa akiibia kwa kushambulia kwa kushtukiza huku akingojea mipira ya kupitishiwa juu au ile ya pasi za kukatiza katikati ya mabeki yaani ‘through ball’. Kuna wakati almanusra mshambuliaji huyu toka Benin alete madhara baada ya mabeki wawili wa Yanga Nadir Haroub Canavaro na Athuman Idd Chuji kuwa wanakabia ndani sana karibu kabisa na eneo la katikati ya uwanja huku na Omotoyosi alikuwa anapata sana nafasi ya kukimbia nyuma ya mabeki.Yanga walizidi kushambulia bila woga ila washambuliaji Keneth Asamoah na Davis Mwape hawakuwa makini kwani wangeweza kuipa Yanga faida ya mabao zaidi lakini ni Hamis Kiiza peke yake ambaye aliweza kufunga bao ambalo liliipa Yanga faida ya kwenda half time wakiwa wanaongoza .Kiungo Haruna Niyonzima kama kawaida yake aliiunganisha vilivyo safu ya ushambuliaji akitengeneza nafasi nyingi ambazo washambuliaji hawakuzitumia. Haruna alikuwa anawasumbua sana viungo wa Zamalek na hasa kiungo Mcameroon Alexis Mendong ambaye alikuwa na kazi ya ziada kumkaba.Haruna alikuwa aki-link vyema na kiungo aliyecheza nyuma Juma Seif Kijiko ambaye kimo chake na uwezo wa kumiliki mpira vilikuwa na faida sana kwa Yanga Kwa jinsi ambavyo Yanga walimiliki mpira kwenye kipindi cha kwanza na kuingia kwenye eneo la hatari la Zamalek walistahili kupata zaidi ya bao moja .Mabeki wa pembeni Stephano Mwasika na Shadrack Nsajigwa walicheza vizuri sana kipindi cha kwanza , walikuwa wanapandisha timu vizuri sana wakipiga krosi kila muda na kama isingekuwa kukosa umakini kwa washambuliaji Mwasika na Nsajigwa wangemaliza mchezo wakiwa na ‘assist’ za mabao mengi .Kipindi cha kwanza kiliisha kwa Zamalek kufanya mabadiliko ya kumuingiza Mohamed Abdelshaffi Sayed aliyechukua nafasi ya Islam Awad Ismael ambaye aliumia . Mabadiliko haya hayakuwa na madhara makubwa kwani muda mfupi baada ya kufanyika muda wa mapumziko ulifika .Kipindi cha pili kilianza kwa hali tofauti na ile iliyokuwa kwenye kipindi cha kwanza. Zamalek waliingia wakiwa wanacheza kwa kutafuta goli zaidi na hii ilimaanisha kuwa wao ndio walikuwa wanamiliki asilimia kubwa ya mpira . Yanga bado waliendelea kutengeneza nafasi zaidi na hadithi ile ile ya kukosa umakini wa kubadilisha nafasi kuwa magoli iliendelea. Zamalek walifanya mabadiliko zaidi kwa kumtoa Ahmed Fathi abdelsamea na kumuingiza Amr Zaki. Mabadiliko haya yalileta uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya Zamalek na dakika tatu tu baada ya kuingia Zaki aliyafanyia kazi makosa ya mabeki wa Yanga waliosimama wima wakidhani ameotea na Zaki aliwapita na kufunga kwa staili ya kutoa pasi kwenye wavu kwa mpira uliompita mlinda mlango wa Yanga Shaban Kado.
Bao la Zaki pamoja na kuingia kwake kwa ujumla viliipa Zamalek uhai mkubwa na wakawa wanashambulia zaidi . Amr Zaki hakuwa anasimama kwenye sehemu moja, alikuwa akihaha kwenye pembe zote za eneo la hatari la Yanga hali ambayo iliwachanganya mabeki wa Yanga wasijue la kufanya kumdhibiti. Zamalek walifanya mabadiliko zaidi kwa kumuingiza winga wa timu ya taifa Hazem Mohamed Abdelhamed. Hazem alimpa wakati mgumu sana beki wa kushoto wa Yanga Stephano Mwasika ambaye alishindwa kabisa kumzuia na alikuwa akimpita kama anavyotaka .Chenga za Hazem kwa Stephano zilimlazimu kocha wa Yanga Kostadin Papic kumbadili na kumuingiza Oscar Joshua ambaye kidogo aliweza kumdhibiti Hazem .Yanga nao walifanya mabadiliko ya kumtoa Davis Mwape ambaye nafasi yake ilichukuliwa na winga Shamte Ali.
Mabadiliko haya yalileta mabadiliko uwanjani kwenye mfumo ambao Yanga ilikuwa inacheza ambapo Hamis Kiiza aliingia kati toka pembeni alikokuwa anacheza na Omega seme alitoka upande wa kulia na kuhamia kushoto ili kumruhusu Shamte ashambulie toka kulia . Mabadiliko haya yaliipa Yanga uhai uliopotea kipindi cha kwanza na kuwafanya kuanza kumiliki mpirra tena lakini bado nafasi hazikutumiwa .Mabadiliko yaliyofanywa na Hassan Shehata yaliwapa wakati mgumu mabeki wa pembeni wa Yanga ambao walishindwa kupandisha timu kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza.Mchezo ulivyokuwa unaenda ukingoni Zamalek walikuwa wanacheza kwa kuridhika baada ya kuwa wamepata faida ya bao la ugenini ambalo kwao lilikuwa muhimu sana na walicheza kwa tahadhari ya kulinda bao hilo .Kimsingi yanga wamechezea bahati waliyokuwa nayo kwani kama washambuliaji hasa Keneth Asamoah na Davis Mwape wangekuwa makini Yanga wangeweza kupata japo ushindi wa tofauti ya bao moja au hata mawili kwa kuwa walitengeneza nafasi ambazo zingewafanya wafunge.Yanga wanaenda kucheza ugenini ambako mchezo hautakuwa kama ulivyokuwa hapa nyumbani , bado nafasi ya kufanya mabadiliko inaweza kuwepo lakini mchezo wa ugenini utakuwa na sura tofauti na ile iliyokuwa nao hapa . Benchi la ufundi la Yanga linapaswa kufikiria kuwapa nafasi washambuliaji kama Jerryson Tegete na Pius Kisambale na hata Idrissa Rashid ambao wanaweza kuleta uhai kwenye safu ya ushambuliaji.
No comments:
Post a Comment