Mwaka 1988 ulikuwa ni mwaka wa wagosi kwa sababu mwaka huo timu zote mbili za Tanga zilizokuwa kwenye ligi kuu zilifanya vizuri.Coastal union walikuwa mabingwa wa bara na African sports walishika nafasi ya tatu nyuma ya yanga.
Nafasi ambayo iliwawezesha kushiliki ligi ya muungano.Walipokwenda kwenye muungano African Sports walikua mabingwa na Coastal walishika nafasi ya pili hivyo timu hizo za Tanga zikapata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa (klabu bingwa Africa na kombe la washindi wakati huo).
Kwenye ligi ya bara kulikua na msisimko wa hali ya juu kiasi kwamba ilikua ngumu kutabiri nani atakua bingwa,hadi mechi za mwisho ndipo bingwa alipofahamika.Uthibitisho wa hayo ni jinsi timu tatu za juu yaani Coastal,Yanga na A/sports kutofautiana magoli ya kufunga.Kwani zote zilikua na point 26.Coastal alikua na magoli ya kufunga 27,Yanga 24 na
” wanakimanumanu” A/Sports 23.
Hivyo bingwa alipatikana kwa kuangalia timu iliyokua na magoli mengi.Kabla ya mechi za mwisho za siku hiyo Coastal na Yanga zilizokua zikiongoza,zote zilikua tayari na point hizo 26 lakini zote zikapoteza mechi zao kwa kufungwa na mahasimu wao.Coastal alipigwa
2-0 na Africa Sports na na yanga alifungwa 2-1 na Simba(Simba akaokoka kushuka daraja).
*Kwenye mechi hiyo ya Tanga iliyotoa dira kwamba mwaka huu ni mwaka wa wagosi.Timu hizo mbili zilikutana tarehe 23/07 ndani ya uwanja wa mkwakwani.Hii ilikua siku ya jumamosi ,siku ambayo watani hao ambao wako jirani sana huko Tanga kuliko hata walivyokaribiana simba na yanga hapa Dar kwani wao wametofautishwa na majengo au nyumba zisizozidi 10 kwenye barabara ya 11 na 12.
*Hii ndio siku ambayo Coastal Union walitwaa ubingwa wa Tz bara kwa mara ya kwanza na ya mwisho licha ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu wao “wanakimanumanu”,mechi hii ndio ambayo inadhaniwa kuingiza watazamaji wengi kuliko mechi nyingine yoyote ya kimashindano iliyochezwa ndani ya uwanja wa mkwakwani.Katika mechi hii A/sports iliwashangaza watazamaji kwa kuvaa jezi za njano tofauti na rangi ya jezi zake zilizozoeleka nyeupe na bluu.
*Licha ya siku hii kukumbukwa na wagosi kwa kuchukua ubingwa pia ndio siku ambayo wanaikumbuka kwa kucheka huku wakiwa wamenuna na pia kutokea kwa tukio la ajabu na la kushangaza.Tukio la kupasuka mpira ukiwa hewani,mpira ulipasuka hewani baada ya shuti kali la nahodha wa coastal Yassin Napili,shuti ambalo lilionekana kuwa lingezaa bao.
Hakuna mchezaji aliekuwa anamkaba Napili wakati akipiga shuti hilo,wengi waliamini kuwa ingeweza kuwa bao kama mpira huo ungefika langoni ukiwa na nguvu zake kwani baada ya kupasuka ukiwa angani ulidondoka chini na kuelekea moja kwa moja hadi kwa golikipa wa A/sports ambae aliuokota ukiwa hauna upepo.
*Ilikuwa ni katika dakika ya 25 mpira huo ulipopasuka bila kutarajiwa,wakati huo hakukua na timu iliyokua imepata bao.Beki namba 3 wa Coastal Douglas Muhani aliambaa na mpira upande wa kushoto akamuwekea pande Yassin Napili ambae alikuwa amepanda na move hiyo,akiwa katika nafasi nzuri Napili alijikunja na kujikunjua, kufumba na kufumbua kishindo kikubwa kikasikika uwanjani, mpira umepasuka, namna gani mpira huo ulipasuka hakuna alieweza kumuelezea mwenzake,ilibidi uletwe mpira mwingine.
Kipindi cha pili A/sports ambao walielemewa sana kwenye kipindi cha kwanza walianza kucheza vizuri na kufunga mabao mawili yaliofungwa na Juma Burhan”kakoko”kunako dakika ya 71 akiunganisha kwa shuti kali cross ya marehemu Abbas Mchemba na bao la pili lilifungwa dakika 87 na mfungaji bora wa mwaka huo (marehemu)Victor kefa mkanwa ambae alimzidi mbio beki Abdallah Tamimu “mdaula”.Baada ya bao hilo hali ndani ya uwanja wa mkwakwani ilikua ni vurugu tupu kwani muda huo huo kwenye uwanja wa Taifa simba nao walipata bao la pili (kupitia matangazo ya moja kwa moja ya Redio Tanzania)habari hiyo iliwapa nguvu mpya mashabiki wa Coastal waliokua tayari wameanza kununa na kupata nguvu mpya zilizo wawezesha kuimba Bingwa,Bingwa,Bingwa.
Timu zilipangwa kama ifuatavyo
Coastal Union
1. Mohamed Mwameja
2. Said Kolongo
3. Douglas Muhani
4. Abdallah Tamimu(mdaula)
5. Yasin Abbu Napili
6. Ally Maumba “white Horse”
7. Idrisa Ngulungu
8. Kassa Mussa
9. Juma Mgunda
10. Hussein Mwakuluzo
11. Razak Yusuf
Kocha: Zakaria Kinanda (marehemu)
A/SPORTS
1. Salim Waziri
2. Fransis Mandoza
3. Bakari Tutu(marehemu)
4. Hassan Banda
5. Mhando Mdeve (marehemu)
6. Raphael John
7. Juma Burhan “kakoko”
8. Abbas Mchemba(marehemu)
9. Victor kefa Mkanwa(marehemu)
10.Mchunga Bokari(marehemu)
11. Said Seif
Kocha: Sillersaid Mziray ( Marehemu )
TUZO ZILIZOTOLEWA BAADA YA MASHINDANO @ shs 10,000/= KWA WANAMICHEZO WAFUATAO
1. Kocha bora -‘’Arigo Sachi’’(marehemu)Zakaria Kinanda wa coastal
2. Mchezaji mwenye nidhamu na ambae pia alikua mchezaji bora - Yassin Napili wa coastal
3. Mfungaji bora – Victor Kefa Mkanwa wa African sports
4. Kipa bora - Joseph Katuba wa Sigara
5. Mchezaji mwenye umri mdogo aliengara - Athuman Abdallah ‘’China’’ wa Yanga
6. Mchezaji mwenye umri mkubwa – John Simkoko wa Reli morogoro
Ukimtaja Razak Yusuf bila kuweka Careca ni kama humtendei haki..teh teh teh Kimanumanu, wagosi wa kaya zinakumbusha watu mbali kaka shafii
ReplyDeleteHiyo ndio Tanga ya enzi hizo,Tanga KUNANI
ReplyDelete