WACHEZAJI saba wa timu ya soka ya Waandishi wa Habari za michezo nchini (Taswa FC) wanakabiliwa na adhabu kali baada ya kukacha mechi maalum ya kufunga mwaka 2011 dhidi ya Lebanon FC.
Mechi hiyo ilifanyika Desemba 31 kuanzia saa 4.00 usiku na wachezaji hao walishindwa kuheshimu makubaliano yaliyofanyika asubuhi yake na kukacha mchezo huo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary.
Majuto alisema kuwa tabia hiyo imewasikitisha sana kwani imeonekana wazi kuwa ni hujuma kwani taarifa ya kuwepo kwa mechi hiyo ilitolewa asubuhi na wengine kupewa katika mechi ya kirafiki baina ya Simba SC na Mtibwa Sugar iliyofanyika kwenye uwanja wa Chamazi jijini.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Sweetbert Lukonge, Wilbert Molandi, Jimmy Haroub, Mohamed Akida, Fred “Chuji” Mbembela, Shedrack Kilasi na Calvin Kiwia. Majuto alisema wachezaji hao wamepewa barua na uongozi huo kujibu kwa nini wasichukuliwa hatua za kinidhamu kwa kiendo hicho.
Kwa mujibu wa Majuto, wachezaji hao wanatakiwa kujibu barua hizo kabla ya Januari 6 ambapo kikao cha kamati ya utendaji kwa kujumuisha na makocha kitafanyika Ijumaa kwenye mgahawa wa Hadees kwa ajili ya kutoa maamuzi. Kwa mujibu wa kanuni za Taswa FC, wachezaji hao wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kati ya mwezi mmoja, mitatu na mwaka.
Wakati huo huo Taswa FC inaanza mazoezi rasmi ya kujiandaa na safari ya Tanga na Zanzibar jioni hii kwenye uwanja wa Chuo Cha Posta, Kijitonyama. Majuto aliwataka wachezaji wote kufika kwa wingi ili kufanikisha mazoezi hayo.
No comments:
Post a Comment