Wachezaji Amri Kiemba, Salum Kanoni na Shija Mkina ni miongoni mwa nyota wa ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba walioondolewa rasmi kwenye kikosi chao kitakachomalizia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, imefahamika.
Wachezaji hao, pamoja na washambuliaji Shija Mkina na Mohamed Kijuso, wameondolewa Simba kwa kutolewa kwa mkopo na kuuzwa jumla kupitia dirisha dogo la usajili lililofungwa juzi saa 6:00 usiku na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa Kiemba amepelekwa kwa mkopo katika klabu ya Polisi Dodoma, Mkina (Kagera Sugar) na Kanoni (Moro United) na Kijuso ameuzwa jumla kwa klabu ya ‘maafande’ wa Ruvu Shooting.
Kamwaga amesema kuwa katika kujiimarisha zaidi, wamemrejesha Derick Waluya waliyetaka kumjumuisha mwanzoni mwa msimu lakini ikashidikana baada ya beki huyo wa kimataifa kutoka Uganda kuumia.
Simba pia wamewapandisha wachezaji watano kutoka katika kikosi chao cha Simba B ambao ni Abdalah Seseme, Miraji Said, Frank Selule, Hassan Rajabu na Ramadhan Seme.
Katika hatua nyingine, kiungo Ramadhani Chombo ‘Redondo’ wa klabu ya Azam ataendelea kuitumikia timu yake na wala sio Moro United kama ilivyokuwa ikivumishwa.
Taarifa zaidi zimedai kuwa Redondo atabaki Azam baada ya kugonga mwamba kwa jaribio la kumtoa kwa mkopo kutoka katika klabu yake kwenda Moro United.
No comments:
Post a Comment