Search This Blog

Tuesday, November 22, 2011

SIMBA YAITANDIKA 5-2 OLJORO, YATINGA NUSU FAINALI UHAI CUP


Timu za Simba na Toto African zimetinga nusu fainali ya michuano ya vijana wenye chini ya miaka 20.
Simba iliyokuwa ikicheza kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana iliifumua Oljoro JKT kwa mabao 5-2, wakati Toto African ikiisambaratisha JKT Ruvu mabao 4-3 kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.

Toto African na Simba zitakutana kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza kesho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji Miraji Athuman aliifungia Simba mabao matatu kati ya matano na kuondoka na mpira huku jingine likifungwa na Rashid Ismail na la kujifunga kwa beki Adelayun Seif wa Oljoro.Kocha wa Simba Seleman Matola aliwasifu vijana wake kwa kuonyesha soka zuri na kupata ushindi waliostahili katika mechi hiyo.

Alisema sasa wanajipanga kwa mechi ya leo ambayo amesema wachezaji wake watapambana kufa na kupona ili kupata ushindi na kuingia fainali.

"Tumejiandaa vizuri kwa mechi ya leo, tunafahamu kwamba tunacheza na moja ya timu nzuri kwenye mashindano, lakini azma yetu ni kushinda mechi hii," alisema Matola mchezaji wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars.

Mabao ya Oljoro yalifungwa na Hans Mwaisela ambaye anaongoza kwa kuzifumania nyavu akiwa amepachika mabao matano na Salehe Ally aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

Kocha wa Simba, Seleman Matola alisema baada ya mchezo huo kumalizika kuwa vijana wake wamecheza kwa kujituma na nakufuata maelekezo yake.

“Tumecheza vizuri toka mwanzo wa mchezo mpaka mwisho naamini sisi ndio timu bora kwenye mashindano haya,” alisema Matola.

Alisema nguvu na akili wanazielekeza kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Toto African iliyowafunga hatua ya makundi kwa bao 1-0 na kuhakikisha wanalipiza kisasi na kutinga fainali ya michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment