Search This Blog

Friday, November 4, 2011

PESA ZA ZAWADI ZA MOSHA ZATAKA KULETA KASHESHE JANGWANI


Zoezi la kuwatuza wachezaji wa Yanga kutokana na kuwafunga mahasimu wao Simba kutoka kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davies Mosha, nusura liingie dosari baada ya uongozi kujaribu kuzuia zoezi hilo.

Uongozi wa wanajangwani ulitaka fedha hizo zipitie kwao tofauti na mpango wa Mosha aliyetaka kuwatuza moja kwa moja, kupitia mwakilishi wake, Abek Mcharo, aliyetoa kitita cha sh mil. 10.

Mosha alitoa kiasi hicho cha fedha ili kutimiza ahadi yake aliyoitoa kwa wachezaji wa Yanga baada ya kuwafunga watani wao wa jadi, Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyopigwa kwenye dimba la Taifa Dar es Salaam, Jumapili iliyopita.

Fedha hizo zilikabidhiwa na mwakilishi wa Mosha, Abel Mcharo, kwa Kocha wa Yanga, Kostadin Papic, katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, jijini.

Katika salamu zake kwa wachezaji wa timu hiyo, Mosha alisema kwamba kama mwanachama wa Yanga hana budi kutekeleza ahadi aliyoitoa kabla ya mchezo huo ambao alishindwa kuushuhudia kutokana na kikazi nje ya nchi.

“Nasikitika kwamba sikuweza kuhudhuria katika pambano hilo kutokana na kuwa nje ya nchi, nimerejea jana (juzi) lakini kwa kuwa muungwana ni vitendo nikaona nitekeleze ahadi yangu,” alisema.

Mosha alionya kuwa tukio hilo lisitafsiriwe tofauti na dhamira yake, kwa kuwa yeye wakati akijiuzulu nafasi ya makamu wa mwenyekiti wa Yanga, aliahidi kuendelea kutoa mchango wake wa hali na mali kila inapobidi kwa manufaa ya klabu hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa klabu hiyo, mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi, Ali Mayai, alimshukuru Mosha kwa kitendo hicho na akawataka wadau wengine kuungana naye ili kuzidi kuwapa morali wachezaji.

No comments:

Post a Comment