Search This Blog

Wednesday, November 30, 2011

NINI MAANA YA MCHEZAJI KUHAMA KWA MKOPO ?

Wakati dirisha dogo la usajili wa bongo likiwa linafungwa usiku wa leo,nimeona si vibaya kuandika juu ya utaratibu wa mchezaji kuhamishwa kwa mkopo kutoka klabu moja kwenda nyingine unavyofanyika.
Nimeamua kufanya hivi baada ya kugundua utaratibu wa kuhamisha wachezaji kwa mkopo hapa bongo unafanyika kiholela sana.
Kwenye soka mchezaji kuondoka kwa mkopo maana yake ni kwenda kuichezea timu nyingine ambayo hana mkataba nayo kwa muda maalum. Mikataba ya mikopo huwa inakuwa ya muda husika kama vile wiki kadhaa hadi wakati mwingine msimu mzima.
Wachezaji wanaweza kupelekwa timu nyingine kwa mkopo kwa sababu kadhaa na mara nyingi wachezaji wachanga hupelekwa sehemu nyingine kwa mkopo ili wapate uzoefu na hatimaye watumike baadaye kwenye timu zao .
Katika mfano huu timu ya mchezaji inaweza kuendelea kulipa mshahara wa mchezaji au vinginevyo kuendana na makubaliano yaliyopo baina ya pande tatu husika na baadhi ya timu huweka mazingira maalumu baina yake na baadhi ya vilabu ambapo timu ndogo hutumika kama timu ya kulea wachezaji kwa mkopo yaani feeder club , mfano Man United wana makubaliano na Royal Antwerp ya Ubelgiji na Arsenal wana makubaliano na Beveren.


Mkopo pia unaweza kutumiwa katika mazingira ya kusubiri muda wa dirisha la usajili kufunguka ambapo makubaliano maalum yanaweza kuwekwa ili kuipa timu fursa ya kumsajili mchezaji husika kwa muda mrefu.
Klabu inaweza kumchukua mchezaji kwa mkopo kama haina fedha ya kutosha kufanya usajili lakini wanaweza kulipa mishahara kwa muda na pia wachezaji huchukuliwa kwa mkopo kama mbadala wa wachezaji wanaoumia au kufungiwa kwa muda mrefu.
Klabu ya kwanza ya mchezaji husika inaweza kuhitaji fedha kutumika kama ada ya uhamisho wa mkopo au inaweza kuwapa wanaohitaji mchezaji wake masharti ya kuwalipa wachezaji walioko kwa mkopo huku pia wachezaji hutolewa kwa mkopo endapo kuna wachezaji waliokuwa wameumia wamerejea au kama timu haina fedha za kutosha na inataka kupunguza gharama.
Kuna baadhi ya wachezaji wengine hutolewa kwa mkopo kwa kuwa hawana furaha kwenye klabu walizopo au wameingia kwenye mazingira ya ugomvi na viongozi wao na hakuna klabu inayowahitaji kwa muda mrefu na hapa kuna mifano ya akina Henri Camara akiwa Wolves na Craig Bellamy akiwa na Man City na kabla ya hapo Newcastle United.
Kwenye Ligi kuu ya England wachezaji wanaocheza kwa mkopo hawaruhusiwi kucheza dhidi ya timu zao za msingi au timu zenye usajili wao(hii ni kwa mujibu wa sehemu ya 7.2 ya sheria ya m.6) ambapo hii inamaanisha kuwa klabu kubwa yaweza kumtoa mchezaji wake kijana kwenye timu ndogo huku ikifurahia kushuhudia anachofanya dhidi ya timu nyingine kubwa ambazo ni wapinzani wake huku wakiwa hawaruhusiwi kuidhuru timu ya msingi .
Hata hivyo wachezaji walioko kwa mkopo wanaweza kucheza dhidi ya timu zao kwenye michezo ya vikombe .

1 comment:

  1. Je Mkopo wa wachezaji ualipwaje, ni mkopo wa aina gani, Clab/ timu ya machzaji inafaidika vipi na kmopo huo? samahani nikipata jibunitashukuru (Facebook: matiaskabyemela)

    ReplyDelete