Search This Blog

Wednesday, November 30, 2011

MIAKA 50 YA UHURU : KOMBE LA GOSSAGE

BAADA ya vita vikuu ya pili vya Dunia (W.W.II) hadi Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961, mafanikio pekee ya Tanganyika katika michezo kwa ujumla na hasa mpira wa miguu ilikua ni katika michuano ya Kombe la Gossage iliyokua ikishindaniwa na makoloni ya Uingereza ya Afrika Mashariki.

Mwanzo wa miaka ya 1950 (1952-53) Tanganyika ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mara mbili kwa msaada wa mshambuliaji wake mahiri, William Nashon.
Nahodha wa Kenya Joe Kadenge akipokea Kombe la Gossage kwenye miaka ya 60
Baada ya hapo, Kombe la Gossage lilikuwa likitwaliwa na Uganda na Kenya kwa miaka mingi. Uganda ilikuwa na wachezaji hatari sana, hasa Kalibala na kipa wao Aggard. Lakini Kenya pia ilikuwa na nyota kadhaa wakiwemo Peter Orange, Elijah Lidonde, Shem Chimoto, Ali Kajo, Joe Kandege aliwahi kumvunja kipa mkono katika mechi iliyochezwa kwenye mvua na mipira ya kizamani ilikuwa inanyonya maji, hivyo shuti lake lilimvunja kipa mkono. Kandege alikua anaogopwa na makipa wengi.

Tanganyika pamoja na kuwa na wachezaji wenye vipaji kama Mwemba, Washokera na kipa bora Afrika Mashariki wakati huo Miraji, haikuweza kuhimili vishindo vya Wakenya na Waganda. Kutambiana kati ya Kenya na Uganda bado kunaendelea hadi leo.

Zanzibar mbali na kuwa ndiyo timu iliyokuwa ikiisumbua sana Uganda, ilibaki kuwa timu ya kupatia mabao na kuwafurahisha watazamaji kwa pasi zao za chini chini na kuvutia.

Hali hii iliendelea mpaka Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961. Baada ya uhuru, kocha kutoka Yugoslavia aitwaye Celebic alipewa jukumu la kuifundisha Tanganyika. Haikuchukua muda kwa Celebic kugundua kuwa, Tanganyika ilikuwa inazidiwa na Kenya na Uganda.

Kuzidiwa huko kwa Tanganyika hakukuwa kwa vipaji au akili pekee, bali hata nguvu ya mwili. Baada tu ya michuano ya Kombe la Taifa iliyokusanya mikoa yote katika Uwanja wa Ilala (Karume), Celebic alichagua wachezaji wengi wapya baadhi yao kutoka mikoa ambayo haikuwahi kutoa wachezaji wa timu ya taifa wakiwemo Kama Chuma na Dini kutoka Mtwara.

Baada ya kuwasuka vizuri, kazi ikaanza. Matokeo yake Tanganyika ilichukua Ubingwa wa Afrika Mahariki mara tatu mfululizo hadi Celebic alipoondoka. Hadi leo hajatokea kocha kama yeye hapa nchini.

No comments:

Post a Comment