Aliyekuwa kocha mkuu wa klabu ya Simba, Moses Basena ambaye juzi ilitangazwa amefukuzwa kazi ndani ya klabu yake na kibarua chake kuchukuliwa na Mserbia Milovan, ameitaka klabu hiyo kuheshimu mkataba alioingia nao Septemba Mosi mwaka huu, kinyume chake wajiandae kumlipa mamilioni.
Uongozi wa Simba kupitia Ofisa Habari wake, Ezekiel Kamwaga ulisema jana kuwa umemsimamisha kazi kwa muda kocha huyo na nafasi yake imechukuliwa na kocha Milovan Cirkovic, ambaye tayari amesaini mkataba wa miezi sita.
Akizungumza kwa simu kutoka Uganda, Basena alisema: "Kama ambavyo mimi nimekuwa nikiheshimu mkataba wangu na klabu, ndivyo uongozi unavyopaswa kuheshimu.
"Awali nilipewa mkataba wa miezi sita, nikamaliza na kupewa mwingine wa miaka miwili kuanzia Septemba Mosi hadi Septemba 2013. Ninachofahamu, mimi bado kocha wa Simba na si vinginevyo," alisema Basena.
Kocha huyo raia wa Uganda ambaye hekaheka za kutotakiwa Simba zilianza mara baada ya kupoteza mchezo na Yanga, alisema endapo klabu yake itakuwa tayari kuvunja mkataba wake hana tatizo na uamuzi huo.
Aliongeza kuwa, iwapo uongozi wa Simba utaamua kuvunja mkataba wake, jambo la kwanza ni kumpa taarifa na pia sababu za kusitisha ajira yake, na mwisho kulipwa haki zake zote ikiwemo fidia ya kuvunjwa mkataba.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, mshahara wa Basena kwa mwezi ni dola 2500 (sawa na shilingi 4.5milioni), na ni miezi miwili tu imepita tangu amwage wino kwenye mkataba huo mpya.
Iwapo Simba watavunja mkataba wake watalazimika kumlipa misharaha ya miezi 22 iliyosalia kwenye mkataba wake, ambayo ni sawa na shilingi 99milioni mbali na fidia ya kuvunja mkataba.
"Leo Simba wakiamua kuvunja mkataba wangu, sina tatizo na mimi sitakuwa wa kwanza kukutana na hali hiyo, ila cha msingi ni kulipwa pesa zangu zote," alisema Basena huku pia akiushangaa uongozi wa Simba kutofanya naye mawasiliano yoyote.
Alipoulizwa ni kiasi gani anastahili kupewa kama mtakaba wake utavunjwa, alisema: "Hii ni siri yangu na uongozi, siwezi kusema ni shilingi ngapi lakini ni mamilioni ya pesa.
"Mimi si lazima nije Tanzania kuvunja mkataba na kudai pesa zangu. Wanaweza kunitumia nikiwa huku (Uganda). Wanitumie kupitia benki, mbona haya mambo ni rahisi sana," aliongeza.
Pia alishangazwa na uongozi wa Simba kutumia muda mwingi kuzungumza hatima yake kupitia vyombo vya habari kabla ya kufanya naye mawasiliano.
"Wewe leo (jana) unaniambie eti nimesimamishwa kazi--mbona mimi sijui? Mwingine akaniambia Simba wamevunja mkataba wangu, hilo pia sifahamu. Kama haya yote ni kweli kwanini uongozi haunipi taarifa mpaka nisikie toka kwa waandishi?," alihoji.
Alisema zaidi kuwa, hana sababu ya kupingana na uamuzi wa klabu ya Simba katika kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi, ila anajivunia kumaliza mzunguko wa kwanza timu ikiwa inaongoza msimamo.
"Sioni baya nililofanya Simba, nimeacha timu kwenye nafasi nzuri, wachezaji, mashabiki na wapenzi walikuwa wakinipa sapoti kubwa, hili ni jambo la kujivunia kwangu," alisema.
Basena alisema kuwa alipaswa kurejea nchini Desemba 6, lakini kwa vile hajamaliza mambo ya msiba, anawasiliana na uongozi ili aongeze muda zaidi kabla ya kuja kuendelea na kazi yake.
Suala la Basena kwa siku za hivi karibuni limekuwa likiteka kurasa za vyombo, huku baadhi ya taarifa zikidai amefukuzwa kazi na zingine zikidai amesimamishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ameshindwa kuwasilisha vyeti vya taaluma yake.
Hata hivyo, kuhusu suala la vyeti, Basena alisema kuwa tayari alishavituma Simba, lakini uongozi wa klabu hiyo uliendelea na mchakato wa kumsainisha mkataba kocha mpya kwa vile vyeti hivyo vilichelewa kufika.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment