Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliketi Oktoba 16 mwaka huu pamoja na mambo mengine kutolea uamuzi utata uliojitokeza na kukwamisha mechi ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Polisi Iringa na Small Kids ya Mpanda, Rukwa iliyokuwa ichezwe Oktoba 15 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa. Utata huo ulisababishwa na uuzwaji wa timu ya Small Kids kwa mmiliki mwingine, huku Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kikipinga kuwa haukuwa halali. Hali hiyo ilisababisha ziwepo timu mbili za Small Kids kwenye mechi hiyo dhidi ya Polisi Iringa. Baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa mbele yake zikiwemo za mauzo ya timu hiyo, pamoja na taarifa ya Msimamzi wa Kituo cha Iringa, Eliud Mvella uamuzi wa Kamati ya Mashindano ni kama ifuatavyo; Small Kids iliyouzwa ndiyo inayostahili kucheza ligi hiyo, kwa vile mwenye mamlaka ya kuuza klabu ni mmiliki mwenyewe na si chama cha mpira wa miguu cha mkoa husika au cha wilaya ambacho klabu ina makao yake. Isipokuwa uhamishaji wa umiliki unapofanyika vyama hivyo vinataakiwa kupewa taarifa. Vilevile Kamati ya Mashindano imekubali ombi la Small Kids kuhamisha kwa sasa mechi zake kutoka Mpanda baada ya kupokea vitisho kuwa ikienda kucheza huko itakiona cha mtema kuni. Hivyo Small Kids kwa sasa imeruhusiwa kuchezea mechi zake Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro. Pia mechi kati yake na Polisi Iringa ambayo haikufanyika sasa itachezwa Novemba 1 mwaka huu mjini Iringa. Katika uamuzi mwingine, Kamati ya Mashindano imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasilisha kesi mbele ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi dhidi ya baadhi ya viongozi wa RUREFA waliosababisha mechi ya Iringa isichezwe na pia kutoa maneno ya vitisho kwa viongozi wa Small Kids.
MECHI YA STARS DHIDI YA CHAD
Taifa Stars inatarajia kuingia kambini Novemba 3 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayofanyika Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena. Ili kutoa fursa kwa wachezaji watakaoitwa Stars kuripoti kambini ndani ya muda uliopangwa, mechi za mwisho kumaliza mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Vodacom zimefanyiwa marekebisho. Mechi hizo sasa zitachezwa Novemba 2 mwaka huu badala ya tarehe ya awali ya Novemba 5 mwaka huu. Mechi hizo ni Oljoro vs Villa Squad (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid), Moro United vs Simba (Uwanja wa Taifa), Polisi Dodoma vs Yanga (Uwanja wa Jamhuri), Toto Africans v Azam (Uwanja wa CCM Kirumba), Kagera Sugar vs Coastal Union (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar vs African Lyon (Uwanja wa Manungu) na Ruvu Shooting vs JKT Ruvu (Uwanja wa Mlandizi).
MAPATO YANGA vs KAGERA SUGAR
Mechi namba 58 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Kagera Sugar iliyochezwa Oktoba 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 42,810,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 11,559. Watazamaji 11,787 walikata tiketi kushuhudia mechi namba 62 ya ligi hiyo kati ya Simba na African Lyon iliyochezwa Oktoba 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi hiyo iliingiza sh. 41,800,000. Nayo mechi namba 60 kati ya JKT Ruvu na Azam iliyochezwa Oktoba 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Chamazi iliingiza sh. 909,000 kutokana na watazamaji 303 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Ligi Daraja la Kwanza hatua ya makundi inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaendelea tena kesho (Oktoba 19 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja tofauti. Katika kundi A, Polisi Dar es Salaam itacheza na Burkina Faso ya Morogoro kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani wakati Transit Camp itakuwa mwenyeji wa Temeke United kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Nayo Mgambo Shooting itakuwa mgeni wa Morani katika mechi itakayochezwa mkoani Manyara. Kundi B itakuwa kati ya Small Kids na Tanzania Prisons zitakazocheza mjini Morogoro, Mbeya City itaumana na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine. Kundi C ni kati ya Manyoni FC na Polisi Morogoro itakayochezwa mjini Singida wakati Rhino FC itakuwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. Mechi kati ya Majimaji na Polisi Iringa ya kundi A yenyewe itachezwa Oktoba 20 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea kama itakavyokuwa kwa mechi ya kundi C kati ya 94KJ na Polisi Tabora itakayochezwa Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.
VIINGILIO SIMBA v RUVU SHOOTING
Viingilio katika mechi namba 66 kati ya Simba na Ruvu Shooting itakayochezwa kesho (Oktoba 19 mwaka huu) Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam ni sh. 10,000 kwa VIP n ash. 5,000 kwa mzunguko. Tiketi za mechi hiyo zitauzwa uwanjani Chamazi katika magari maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo. Boniface WamburaOfisa HabariShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment