Na Dixon Busagaga,Moshi.
TIMU ya mchezo wa mpira wa magongo (HOCKEY) ya Magereza Tanzania
imeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya Nyerere Cup yanayo
fanyika katika uwanja wa Hindul Mandal ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu
ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Mashindano hayo ambayo yalianza ijumaa iliyopita yanashirikisha jumla
ya vilabu saba kutoka mikoa mbalimbali huku yakitaraji kufikia tamati
leo na mgeni rasmi anatazamiwa kuwa mkuu wa wilaya ya Moshi Musa
Samizi.
Katika mchezo wa kwanza timu ya Magereza Tanzania iliichapa timu ya
Moshi Casa B kwa jumla ya mabao 2 kwa 0 kabla ya kuishushia kichapo
timu ya Twiga ya Arusha kwa jumla ya mabao 4 kwa 2.
Katika mchezo mwingine timu ya Magereza iliadhibu bila huruma timu ya
Kili vijana ya mkoani Kilimanjaro kwa jumla ya mabao 6 kwa 0 na
kufanikiwa kucheza hatua ya nusu fainali.
Akizungumzia ushindi huo afisa msaidizi wa michezo wa Magereza Matilda
Mrawa alisema timu yake imejiandaa kuchukua ubingwa wa mahindano hayo
ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka.
Alisema timu ya Magereza imekuwa ikifanya mazoezi kwa muda mrefu huku
ikiongeza wachezaji wapya ambao watasaidia kuipatia ubingwa mwaka huu.
"Hivi sasa huu mchezo una kua ,kwa sababu kila mwaka tunaposhiriki
tunakutana na upinzania mkubwa kutokana na kwamba timu nyingi zimepata
vijana wengi ambao kwa sasa wameanza kuujua vizuri mchezo huu."alisema
Mrawa.
Alisema timu yake ina historia nzuri ya mchezo huo ambapo mwaka jana
walifanikiwa kushika nafasi ya pili huku wakiibuka mabingwa katika
mashindano ya muungano yaliyofanyika mwezi januari mwaka huu jijini
Dar es salaam.
Kwa upande wake mwandaaji wa mashindano hayo Inderjeet Rehal alisema
mashindano hayo yameendelea kukua siku hadi siku na kwamba mategemeo
yake mwaka ujao mashindano hayo yashirikishe timu kutoka nje ya nchi.
Alisema mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atajinyakulia zawadi
ya kikombe na kila mchezaji atapatiwa zawadi ambayo itakuwa kumbukumbu
huku mshindi wa pili akiondoka na kikombe pamoja na medali kwa kila
mchezaji.
Timu zinazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Magereza Tanzania na
TPDF kutoka jijini Dar es salaam,Hulks ya jijini Tanga,Moshi Casa
A,Moshi Casa B na Kili vijana za mkoani Kilimanjaro
No comments:
Post a Comment