Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam iko katika mikakati ya kuimarisha vitega uchumi wake, ikiwamo kujenga jengo la ghorofa 12 makao yake makuu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuacha kutembeza bakuli.
Katika kuelekea mipango hiyo, tayari wamezungumza na benki mbili tofauti zenye nia ya kupanga kwenye jengo hilo ambapo wanatarajia kuziweka hadharani hapo baadaye.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema klabu hiyo kwa sasa ina mikakati mingi ya kujiweka vizuri kiuchumi, ili kuondokana na ukata, pamoja na kuishi katika jengo ambalo haliendani na hadhi ya klabu hiyo kubwa hapa nchini.
“Katika kufanikisha maendeleo mbalimbali ya klabu, nimeamua kuunda kamati mbalimbali ili klabu kuwa na manufaa na mimi kupunguza majukumu, kwa kuwa sasa nitakuwa na majukumu mawili tu la uwanja pamoja na mikakati ya maendeleo ya klabu,” alisema Rage.
Alizitaja kamati hizo kuwa ni ya Fedha, Mashindano, Ufundi, Usajili pamoja na Kamati ya Nidhamu.
Aliwataja wanaounda Kamati ya Fedha ambayo inaongozwa na Geodfrey Nyange ‘Kaburu’, ni Adam Mgoi, Makamu Mwenyekiti; huku wajumbe wakiwa Saidi Pamba, Kifiri, Zitto Kabwe, Juma Pinto, Abdul Mteketa na Murtaza Mangungu; huku Kamati ya Mashindano ikiwa na Joseph Itang’are (Mwenyekiti), Azim Dewji (Makamu Mwenyekiti), Jerry Ambe, Swedy Mkwabi, Hassan Hassanol, Mohamed Nassoro, Amosi Makala, Richard Ndasa na Suleiman Zakazaka (Wajumbe).
Kamati ya Ufundi ni Ibrahim Masoud (Mwenyekiti), Evans Aveva (Makamu Mwenyekiti), Dan Manembe, Khalid Abeid, Musley Rwekha, Mulamu Ng’hambi, Saidi Tuli, Rodney Chidua na Patrick Rweyemamu (Wajumbe), wakati Kamati ya Usajili wako Zacharia Hans Poppe (Mwenyekiti), Kasimu Dewji (Makamu Mwenyekiti), Francis Waya, Crecensius Magori, Salim Abdallah, Collins Frisch na Gerald Lukumay (Wajumbe).
Rage aliitaja Kamati ya Nidhamu kuwa ni Mwenyekiti, Peter Swai, huku Makamu Mwenyekiti akiwa Jamal Rwambow na wajumbe wakiwa Charles Kenyera, Evody Mmanda na Chaulembo.
No comments:
Post a Comment