Search This Blog

Tuesday, October 11, 2011

Nashukuru tumetolewa… Sasa Tuondokane na fikra za kutegemea kufuzu kwa miujiza..


Kwanza ningependa kuwapongeza Taifa Stars kwa kazi nzuri waliyoifanya.Kiwango cha soka cha timu ya taifa kinaonekana kimeongezeka na hiyo inaonekana sana kwenye baadhi ya matokeo ya timu yetu.
Tumetoka kule ambako tangu mechi ya kwanza tunajua ni miujiza pekee itakayoweza kutupeleka kwenye fainali za kombe la mataifa ya bara la Afrika, na sasa tupo pale ambapo katika mechi ya mwisho tunaamini miujiza pekee ndio inayoweza kutupeleka kwenye AFCON.
Huu ni mwaka wa nne au watano ambao tumekwama kwa kutegemea miujiza ya mechi ya mwisho.
Ingawa kama Mtanzania ningefurahi miujiza itupelekee kwenye AFCON, kwa upande mwingine nashukuru kwamba hatukufanikiwa maana naamini hiyo ingetupa mtizamo ambao sio wa ukweli.
Kutolewa kwetu ni changamoto kwa Taifa letu kuachana na kutegemea miujiza itufikishe mbali. Kutokana na hilo inabidi tujijenge kwa kuweka mipango ambayo itatuwezesha kuwa na uwezo wetu binafsi pasipokutegemea miujiza ili kumpa Mtanzania imani ya kwenda CAN au kwenda kwenye fainali za Kombe La Dunia bila kutegemea miujiza ya mwanzoni au mwishoni.
Tukiangalia kalenda yetu ya taifa kwa miaka mitano ijayo
2012 – Tumekosa AFCON
2013 – Tulikuwa na nafasi ndogo ya kwenda CAN kutokana na mfumo wa kuingia
2014 – Tuna nafasi ndogo sana ya kwenda kombe la dunia kutokana na kundi tulilopangiwa.
2015 – Hakuna AFCON
2017 – AFCON ipo
2018 – Kombe la Dunia
Draw ya kufuzu fainali za kombe la dunia mwaka 2014 ilivyotoka tulipiga yowe la ndani,maana tulijua kufika Brazil ilibidi tupitie njia ndefu inayokutana na miamba kama Ivory Coast.
Kama kawaida yetu,wanahabari na wadau walirudia tena kusema “huwezi jua, mpira ni wa duara na unadunda kwa hiyo lolote linaweza kutokea na tukapita”. Hapo tunarudia tena kusubiria miujiza kabla hata ya kucheza mechi yetu ya kwanza.
Kwa imani yangu kutokana na mpira wetu ulivyo kwa sasa mashindano ya karibu ambayo tunaweza kuondokana na mategemeo ya kufuzu kwa miujiza ni yale ya CAN 2017 huko Libya lakini ambayo ni ya uhakika zaidi ni fainali za kufuzu AFCON 2019 na kama ni kufuzu fainali za kombe la dunia ni za mwaka 2022.
Tuna kama miaka 5 ya kujiandaa kwenda Libya bila kutegemea miujiza. Kwa hiyo la maana kabla ya yote ni kwa taifa kukubali kwamba tusijipe imani ya kucheza mashindano yoyote makubwa kwa miaka 5 ijayo.
Kutimiza hayo inabidi tufanye maamuzi magumu sana kwa siku hizi za mbeleni. Maamuzi magumu yanalipa lakini yanahitaji uvumilivu, na uvumilivu uanze kwa yule shabiki wa kawaida wa mpira mpaka kwa wale wanaotuwezesha kwa hali na mali.
Kwanza ninawashukuru wachezaji wa sasa wa Timu ya taifa, sanasana wale waliotupa miaka yao mingi sana kulitumikia taifa letu. Jasho lenu na nguvu yenu tumezitambua na mmetusogeza mbele hilo tunalitambua.
Lakini Ukweli ni kwamba ukiangalia kiwango kilichooneshwa kwenye mchezo dhidi ya Morocco utangundua , kiwango chetu kilikuwa chini sana kulinganisha na cha wenzetu Moroccou,Pale ndipo uwezo wetu ulipokomea.
Ili kulenga huo mwaka 2017, inabidi tuistaafishe timu yetu ya sasa Inabidi pia tuwashukuru na kuwaaga wachezaji wasasa wa Taifa Stars. Tuunde timu mpya ya vijana (U-23) timu ambayo itashiriki katika mashindano ya kufuzu World Cup 2014 na CAN 2013.
Hivyo basi naamini si timu itakayotupeleka CAN kwa uwezo wao lakini ni timu itayojenga misingi ili sasa wale wa chini yao tuwakuze na kuwalea ili kuhakikisha wanafikia kwenye level ya kutupeleka tunapotaka kwa miaka mingine mingi ijayo.
Hatuna jinsi inabidi tuanzie chini kabisa, tujenge mfumo mpya wa kucheza soka ikiwa ni pamoja na mfumo wa kuibua vipaji na kutengeneza vijana wapya hasa timu timu yetu ya U-17, tujenge na kuimarisha mashindano ya soka la watoto, kuanzia mashuleni sana sana ( Hii ni topic tofauti na ina muda wake ).
La maana sana ni kwanza tukubaliane kufanya maamuzi magumu ya kutoa kabisa tegemeo la kwenda South Africa 2013 au Brazil 2014. Tukikubaliana hilo inamaanisha taifa litakuwa tayari kutekeleza mikakati ya kujenga mpira wetu kuanzia chini.

8 comments:

  1. tujifunze tuache kutegemea miujiza ni sawa na kwenda comoro na mtumbwi

    ReplyDelete
  2. huo ndio ukweli shafii mi hii ni laana kwa tff kuwadhalau wachezaji waliokua wanatamba zamani mi nahisi hao wangekua na nafasi nzuri ya kuwapa mbinu na ujanja wchezaji wetu hatutafika popote kama hatutawashirikisha

    ReplyDelete
  3. tanzania tusuubir miujiza bila mipango mpaka tunajuta kuzaliwa tz.

    ReplyDelete
  4. Kaka ahsante kwa info. nzuri kuhusu team yetu ya Taifa. Mimi na mwanangu mpendwa (Mourinho), tunaipongeza sana team yetu ya Taifa kwa hatua iliyofikia na ilivyoweza kutolewa. Kipekee tunampa pongezi za dhati Juma K. Juma kwa kuweza kupunguza idadi ya magoli ambayo tungeweza kufungwa. Tatizo sio team yetu hapa ni uongozi wa TFF. Tafadhalini TFF kuweni na moyo wa uzalendo na Taifa letu. Tunaipenda sana Tanzania na rasilimali zake.

    ReplyDelete
  5. Dauda, nimekuelewa sana inabidi tufanye maamuzi kama hayo, TFF wakae chini watengeneze mpango mkakati wa kutupeleka kwenye mashindano makubwa baada ya miaka mitano hivi, ikibidi watushirikishe wadau tutoe maoni yetu, then njinsi ya ku moblise funds kwa ajiri ya mkakati huo ufanyike, soka la vijana wadogo ni fundamental(academies zenye maana zianzishwe watu waandike proposols then kuna watu wana pesa wanaweza kutoa funds kuwakuza watoto), ligi yetu iboreshwe iwe na ushindani wa kweli na timu ziwe na timu za watoto wadogo wanotunzwa vizuri, viwanja vyetu ni vibovu virekebishwe wachezaji hawachezi kwa viwango vyao kwa ajiri ya ubovu wa viwanja na kuogopa kuumia. TFF mi siwaelewi kabisa nafikiri wameshidwa ku-focus kabisa sielewi tatizo liko wapi, hawana pesa? wanakosa watu wenye uchungu na mpira wetu? au plan zao zina matatizo?. nafikiri ukianzia serikalini tuna plans nzuri sana kwenye makabrasha lakini tatizo limekuwa ni utekelezaji(implementation). INAUMA SANA NI HAYO KWA LEO.

    ReplyDelete
  6. majibu mepesi kwa maswali magumu ndo yamelifikisha taifa letu hapa tulipo. sekta ya michezo ni taswira ya sekta zote TZ. umesema ukweli Shaffih mafanikio hayaji kwa miujiza tena kwa kuongezea miujiza huwa inasababishwa you don't sit down and wait for a miracle, you work for it!

    ReplyDelete
  7. Mi naunga mkono mapinduzi ya soka,lakini pia siamini kama wachezaji aliowachagua huyu kocha wa kigeni ndio bora,wapo wengi wenye uwezo anawapotezea,amekariri Simba na Yanga tu,mi hata sina imani naye,afukuzwe.wapewe wabongo wachape kazi,anatuibia pesa yetu tu ya kodi,

    Watu wazunguke,waone watu wanaocheza kwa nguvu,ari na utaalam,wapo wengi tu,kuna wachezaji wameshazoea kufungwa tu hapo Stars ndo maana hawaoni ajabu kufungwa kila siku,wanacheza tu kukamilisha ratiba na wanajua hawataachwa na huyo kocha aliyekariri wao tu

    Nina uchungu sana na nashindwa kuelewa kwa nini watz tu vipofu wa yanayotokea

    ReplyDelete