Search This Blog

Saturday, October 1, 2011

KOCHA WA AZAM AWAONYA WAGHANA


Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amewatetea Waghana Nafiu Awudu na Wahabu Yahya akisema kwamba bado kabisa hawajaimudu Ligi Kuu Bara wala hawastahili lawama lakini akakiri atawaangalia mpaka wakati wa dirisha dogo.

Azam ilisajiliwa Waghana hao ambao wamo katika kikosi cha vijana cha timu ya taifa ya Ghana U-23 kutoka klabu ya Kings Faisal wakaungana na kipa Mserbia Obren Curkovic, Muivory Coast Kipre Tchetche na Mkenya Ibrahim Shikanda.

Katika mechi zake, Stewart amekuwa hawatumii wachezaji hao wa kigeni akiwemo Nafiu ambaye ni beki wa kati aliyefanikiwa kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Moro United waliyoshinda bao 1-0 na baada ya hapo akaanza kumtumia Said Morad ambaye ni Mtanzania.

Wahabu anayecheza kama straika amemtumia dakika za mwishoni kwa mechi ya Moro United na African Lyon na kwa mara ya kwanza alimwanzisha mechi iliyopita dhidi Coastal Union, Tanga aliyocheza dakika 70 akatoka kumpisha Zahoro Pazzi.

Kocha huyo alisema; "Kulingana na mechi nilizowatumia, Waghana hawako sawa, ligi imekuwa ngumu kwao, hawaendani na kasi ya wengine, lakini naendelea kuwaangalia dirisha dogo nitakuwa nimepata jibu kamili."

"Wahab nilikuwa namtumia kama wa akiba, mechi iliyopita nilimwanzisha, lakini sikuona mabadiliko kwa hiyo siwezi kumchezesha kama hayuko sawa na wenzake kama ilivyo kwa Nafiu,alisema Stewart ambaye anaondoka Novemba kwenda Zanzibar kuinoa Zanzibar Heroes itakayokuwa ikijiandaa na mashindano ya Kombe la Chalenji.

Akimzungumzia Obren aliyedaka mechi tatu ambazo ni Moro United, African Lyon na JKT Oljoro alisema: Obren aliumia kiganja cha mkono kama mwezi, akawa amejitonesha naendelea kumwangalia.Kipre ni mgonjwa pia,

lakini hadi mechi ijayo atakuwa amepona kabisa na Shikanda ni hali ya mchezo, kulingana na ushindani wa namba, alisisitiza Stewart raia wa Uingereza ambaye habari za chini ya kapeti zinasema huenda akasitisha mikataba ya wachezaji wawili wa kigeni na kuziba nafasi zao na tayari ameshaueleza uongozi kuhusu hilo.

No comments:

Post a Comment