Search This Blog

Thursday, October 27, 2011

BRYAN ROBSON KUTUA BONGO LEO


Nyota wa zamani wa klabu ya Manchester United na timu ya Taifa ya England, Bryan Robson anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya kufungua kliniki ya kimataifa ya Airtel Rising Stars itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania, Beatrice Mallya, kliniki hiyo itaanza Jumapili ijayo chini ya makocha wa klabu ya Manchester United ambao ni Mark Fagan, Paul Bright na Billy Miller.

Alisema washiriki watatoka nchi za Kenya, Malawi, Sierra Leone na Tanzania.

Kliniki hiyo itakuwa ni hitimisho la michuano ya Airtel Rising Stars 2011, ambayo ilizinduliwa mwishoni mwa Juni mwaka huu na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Andrew Cole.

Cole aliitumikia klabu yake hiyo misimu saba na kuisaidia kutwaa mataji matano kati ya 19 ambayo Manchester United imeyanyakua hadi sasa.

“Airtel Rising Stars ni mpango kabambe wa kutafuta vipaji chipukizi vya soka kutoka ngazi ya chini hadi Taifa,” alisema.

Akizungumzia juu ya michuano hiyo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini, Leodgar Tenga alisema: ”Huu ni mpango muhimu sana kwa maendeleo ya mpira wa miguu hapa Tanzania.

“Na kile ambacho kinafanywa na Airtel Rising Stars kuwa muhimu zaidi ni ule ushirikiano wa kampuni hiyo na Manchester United, ambayo ni moja ya klabu kubwa duniani.

“Hii inaifanya kuwa moja ya kitu kikubwa kutokea katika soka la Tanzania. Tunayo furaha kuwa kwenye ushirikiano huu na tunahaidi ushirikiano wetu zaidi ya hapo,” alisema.

No comments:

Post a Comment