Kwa kuutazama kwa jicho la kiufundi mchezo kati ya Yanga na Azam kuna kila sababu ya kusema kuwa mbinu za kocha wa Yanga hazikuwa sahihi.
Kwa kuitazama Yanga iliyoanza mchezo dhidi ya Azam ilikuwa na washambuliaji wawili Davis Mwape na Kiiza Hamis,basi utagundua hakukuwepo na uhusiano wa kuwapanga wote pamoja na ndiyo maana kocha Timbe alilazimika kumtoa mapema Mwape.
Pointi B ndio mahala alitakiwa awepo mshambuliaji wa Yanga lakini matokeo yake krosi zote za Shamte Ally zilikuwa zinapita tu kama unavyoona kwenye mchoro hapo juu, Mwape na Kiiza mara nyingi walikuwa 'OFF POSITION '.
Zamani ukisikia namba 9 basi jukumu lake lilikuwa ni kusimama mbele huku namba 10 akiwa na jukumu la kumkaba namba 8 wa timu pinzani ili kumfanya namba 8 wenu kuwa huru ili aichezeshe timu,
Siku hizi mpira umebadilika sana hasa mbinu za kucheza uwanjani,mifumo imekuwa ikitumika sana siku hizi kuliko wachezaji kujipanga kwa namba kama ilivyokuwa zamani.
Ili kupata mfumo husika basi huna budi kufahamu tabia za wachezaji wako wawapo nje na ndani ya uwanja,kuwachezesha Mwape na Kiiza kwa wakati mmoja hakukua na tija kwa aina ya viungo waliokuwa wanawazunguka hasa hasa Shamte Ally.
Tatizo ni kwamba mipira yote ya Shamte haikukutana na mtu yoyote kati ya Kiiza na Mwape na hivyo haikuwa na madhara yoyote kwa wapinzani ( kumbuka aina ya mabao aliyokuwa akiyafunga Boniface Ambani )
Ndiyo maana nasema Timbe hakumtendea haki Shamte kwa kumpangia Mwape na Kiiza,
Kwa jinsi walivyopangwa ilionekana kama Kiiza na Mwape wanacheza kama ‘mapacha’ ambao walikuwa wanatakiwa kusaidiana wao kwa wao. Ingeleta maana kama Mwape angesimama mbele kama mshale na Kiiiza angecheza nyuma yake kidogo lakini haikuwa hivyo.
Mwape ni mshambuliaji mwenye nguvu ambaye anatakiwa kucheza kwenye eneo la 18 na si zaidi ya hapo .
Hakuna anayeelewa kwanini Mwape huwa anaelekezwa kucheza nje ya eneo la hatari . Kimsingi mwape akiwa nje ya eneo la hatari utamlaumu tu kwa kuwa hana ‘first touch’ nzuri na zaidi ya hapo hana mahesabu ya ‘dribbling’ yaani hajui ni mara ngapi mchezaji anatakiwa kuendesha mpira kabla hajatoa pasi na ndio maana Mwape ataonekana kuwa mzigo akiwa nje ya 18.
Kwa jinsi Shamte Ally alivyocheza hakuna shaka Yanga walihitaji sana huduma ya Jerry Tegete kwa kuwa aina ya mipira ambayo ilikuwa inatumwa kwenye mchezo wa Azam ni mipira ambayo Jerry Huwa anafunga.
Haya yatabaki kwa Viongozi wa Yanga lakini ukweli ni kwamba Yanga watakosa huduma ya mabao ya Tegete ( si kwasababu ya kufungiwa tu bali hata kwa namna ambavyo walikuwa wanamtumia akicheza zaidi nje ya box wakati yeye ni ‘Goal pocher’ ).
Pius Kisambale kwa upande wake alikuwa na umuhimu sana kwa timu yake lakini hilo halikuwa linaonekana na benchi la ufundi . Kisambale alikuwa anawa-occupy mabeki wa Azam hususan Erasto Nyoni ambaye muda mwingi alikuwa analazimika kuondoka kwenye eneo lake na kumkaba Kisambale.
Pengine makocha wa Yanga walikuwa wanaona kuwa Kisambale hana msaada kwa kuwa Yanga walikuwa wanashambulia sana kupitia upande wa Shamte ambao kimsingi ulikuwa unasaidiwa na wachezaji watatu Shamte,Niyonzima na Nsajigwa.
Kama wachezaji wa Yanga wangekuwa na mlengo tofauti wangeona umuhimu wa Kisambale na kuutumia lakini haikuwa hivyo .
Mwisho wa siku Kisambale baada ya kuonekana hana faida alitolewa nje.
Tatizo moja kwenye soka la Tanzania ni kuwa na maamuzi yasiyozingatia ufundi,Makocha wengi hupenda kufanya mabadiliko kwa kusikiliza presha za mashabiki na nadhani ndio kilichotokea kwa Kisambale.
Nafasi ya Kisambale ilichukuliwa na Rashid Gumbo ( nilicheza naye pale Temeke,kwahiyo namfahamu vizuri Chidy Gumbo ) kimsingi si mchezaji wa pembeni bali kiungo wa kati tena akiwa na sifa kubwa ya kupiga mashuti na pia kutoa pasi za mwisho.
Kwa wenzetu duniani huko ambao wachezaji wao ni mahiri hili sio tatizo kwa kuwa mchezaji amejengwa kuwa na mazingira ya kucheza nafasi zaidi ya moja kuendana na mechi na mifumo mbali mbali. Alipoingia Gumbo hakuwa anacheza pembeni kama Kisambale na ni kama alishurutishwa kucheza nafasi ile nafasi ambayo si yake . Gumbo alikuwa akilazimika kugeuka na kuuleta mpira kwenye mguu wake wa kulia aliouzoea na pia alikuwa akiingia kati alikozoea badala ya kucheza pembeni kama mchezaji anayetokea pembeni.
Ingekuwa busara kwa kocha kufanya ‘tactical switch’ ya kumpeleka Gumbo katikati na kumleta Nurdin Bakari/Haruna Niyonzima pembeni kwa kuwa wana uwezo wa kucheza huko.
Matokeo yake upande wa kulia ukafa kabisa kwa kukosa huduma na matokeo yake Shamte Ally akaonekana amepwaya,akatolewa na nafasi yake akaingia Godfrey Taita mchezaji ambaye ana mentality ya ulinzi na si ushambuliaji.
Ubovu wa mabadiliko haya ulikuwa kwenye ukweli kuwa Yanga walikuwa nyuma na walikuwa wakihitaji bao ili kuokoa mchezo.
Kimsingi mchezo kwa Yanga uliishia hapo na ndio walipofungwa. Kama Yanga wataendelea kucheza kwa ufundi mbovu kama hivi hali itakuwa ngumu sana kwa wao kutetea ubingwa wao hasa ukizingatia ukweli kuwa wanaendelea kuangusha pointi kila leo.
Kwa upande wa Azam sio kwamba walicheza vizuri sana lakini walitengenezewa mazingira ya kupata ushindi na jinsi Yanga walivyocheza hovyo.
No comments:
Post a Comment