Search This Blog

Tuesday, July 5, 2011

Simba ilivyocheza dhidi ya Bunamwaya…



Michuano ya Kagame Castle Cup imeendelea tena leo hii na watanzania wametoka uwanjani wakiwa na roho nyeupe baada ya moja ya wawakilishi Simba Sports Club kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwafunga Bunamwaya toka Uganda kwa mabao 2-1.
Kwa mawazo ya haraka watanzania na wanasimba wote kwa ujumla wana kila sababu ya kuwa na raha kwa ushindi huo ambao unamaanisha kuwa timu ya Tanzania imejihakikishia angalau nafasi ya kufika hatua ya nusu fainali kwa vilabu vyetu viwili vya Tanzania.
Ila kwa jicho la tatu ambalo linatazama mbali zaidi ya michuano hii ya Kagame kikosi cha Simba kina mapungufu kadhaa ambayo kama yasipotatuliwa mapema basi huenda hata michuano yenyewe ambayo Tanzania ni mwenyeji inaweza kuota mbawa na kuwaacha watu wakishuhudia Kombe likipanda ndege na waliojipanga.

Simba kwenye mchezo wa leo walianza na kikosi cha wachezaji Juma kaseja akiwa golini , Juma said Nyoso , Derrick waluhya , Kevin Yondani na Amir Maftah wakiwa mabeki . Viungo walikuwajerry Santo, Patrick Mafisango , Mohamed Banka , Ulimboka mwakinge na Musa Hassan Mgosi akicheza kama kiungo mshambuliaji anayetokea upande wa kushoto na kwenye nafasi ya ushambuliaji alikuwepo Haruna Moshi Boban .
Kwenye kiungo…. Mafisango was Super!
Ukitazama kuanzia nafasi ya kiungo sehemu ya chini ya uwanja ambako alikuwepo Jerry Santo kurudi hadi golini Simba walikuwa vizuri kwa sababu kila idara imetimia kwa watu ambao wanacheza kwenye nafasi zao za asili japo kulikuwa na dosari kwa upande wa beki ya kulia ambako alilazimika kucheza Derick waluhya ambaye baadaye aliumia na Said Nassor Cholo alichukua nafasi yake na upande wa beki ya kushoto Amir Maftah alikuwa anajisahau kwa kupanda sana na kuchelewa kurudi kutimiza jukumu lake la kukaba . ukija kwa viungo wa upande wa juu wa uwanja kuanzia kwa Patrick Mafisango na wenzie wawili waliokuwa wanacheza pembeni Ulimboka Mwakingwe na Mgosi nako hakukuwa na tatizo sana kwani Mafisango ambaye sasa anaonekana kuzoeana na wenzie alicheza ipasavyo akitoa mipira ambayo ilikuwa haipotei mara kwa mara , alikuwa akimiliki na kuchia mipira kama nafasi yake inavyohitaji labda mwishoni tu alionekana kuwa na mbwembwe kupita kiasi ambapo mara moja au mbili alipoteza mipira kizembe , vivyo hivyo kwa Mgosi na hata Ulimboka .


kwenye idara ya ushambuliaji..
Shida kubwa ilikuwa ni ile ile ambayo imekuwa ikiwanyima wanasimba usingizi tangu mwanzo wa michuano hii nayo ni sehemu ambayo kwa asilimia kubwa ndio sehemu muhimu kuliko zote uwanjani nayo ni sehemu ya ushambuliaji ambako leo hii namba tisa alilazimika kucheza Haruna Moshi na mshambuliaji wake wa pili alikuwa Mohamed Banka na walikuwa wakibadilishana nafasi hizo mara kwa mara kuendana na ‘movement’ ya mpira . Eneo hili la ushambuliaji limekuwa tatizo sugu kwa Simba kwa sababu ambazo binafsi nashindwa kuzielewa . Simba haina mshambuliaji asili na hilo pekee ndio tatizo kubwa . Tazama timu iliyoanza na utagundua kuwa hakuna mchezaji yeyote kati ya kumi na moja walioanza na hata wale walioingia kina Cholo , Shija Mkina na Salum Machaku ambaye anabeba jukumu la ufungaji magoli . kuanzia kwa Banka , Mafisango , Mgosi , Boban , Ulimboka hakuna yoyote kati ya hawa ambaye ni mshambuliaji asilia .
Wanasimba mtakubaliana na mimi kuwa Simba hii ya leo si ile ambayo iliwahi kutwaa kombe la muungano huku ikitoa wafungaji bora watatu Emanuel Gabriel , Nteze John na Joseph Kaniki kwenye michuano hiyo hiyo .
Kocha mkuu wa Simba Moses Basena hakubaliani na ukweli huu , inawezekana ameshindwa kutambua tatizo hili lakini anajaribu kulikwepa .
Kipindi cha usajili kilikuwepo lakini Simba iliishia kuwasajili kina Boban , Ulimboka , na wengineo iliyowasajili lakini haikusajili mtu aliyezaliwa kufunga .

Haruna Moshi kuchezeshwa nafasi ya ushambuliaji…
Kwenye mechi dhidi ya Bunamwaya,Simba ilipata nafasi mbili za wazi, ya kwanza aliipata Haruna Moshi kwenye kipindi cha kwanza, alichohitaji kufanya kilikuwa ni kusogea na mpira na kulitazama lango na kuukwamisha mpira wavuni , kama angekuwa mshambuliaji asili angefanya hivyo lakini Haruna Moshi si mshambuliaji maskini ya Mungu , Haruna ni kiungo ambaye akili ya soka lake iko kwenye ufundi wa kumtengenezea mtu mwingine ndio aje afunge , alichofanya Haruna ni kutuliza mpira na kutazama mbele na kutoa pasi kwa Banka , kwa bahati mbaya pasi haikufika na nafasi ya goli ikapotelea hapo .



Viungo wasiokua na uwezo wa kufunga…
Kipindi cha pili wakati Simba wakionekana kukata tamaa huku mashabiki wakililia goli,Ulimboka alipata mpira karibu kabisa na lango tena mabeki walikuwa wamejisahau wakidhani Uli amejenga kibanda , Uli alipiga shuti lakini alimlenga kipa na nafasi ikapotea hapo . Baadae Simba walipata goli lililofungwa na Jerry Santo, bao lililotosha kuwapa ushindi lakini pengine wangeweza kupata ushindi wa uhakika zaidi ya huo wa mabao mawili kwa moja .
Kuna wakati kwenye mchezo huo wachezaji wa Simba walikuwa wanacheza kama Barcelona au Arsenal , wakipiga pasi kwa madaha na uhakika wa hali ya juu , na hili walikuwa wanafanikiwa kwa sababu unategemea nini zaidi ya pasi za visigino unapokuwa na Mafisango , Banka , Boban , Ulimboka , Mgosi ,Machaku na wengineo ila pungufu ni moja tu nalo ni ‘end product’ au matokeo ya pasi za visigino ambayo ni magoli kwani hadithi kwa Simba imekuwa ni pasi tamu za visigino halafu mwisho wa siku anatokea mtu anapaisha mpira .
Kama viongozi wa Simba wakiendelea kulifumbia macho tatizo la ufungaji basi mwaka huu wanaweza kuyasikia mafanikio kwenye bomba kwa sababu watani zao wana washambuliaji wanne ambao wanaweza kufunga na kwenye mechi za Yanga tumeshuhudia kuwa tatizo la ufungaji si kama la Simba kwani walau wastani wa mabao mawili kila mechi unatia matumaini.

No comments:

Post a Comment