Makala yangu ya leo nataka niwakumbushe mbali kidogo, yaani tulipotoka na kufananisha na tulipo leo.
Kilichonishawishi kuandika makala haya ni kuangalia wako wapi wanamichezo wale niliokuwa nikiwaona zama zile na leo siwaoni kama vile Suleima Nyambui, Fillbert Bayi, Gidamis Shahanga, Mwinga Mwanjala, Kilangazi wa Kijibweni, Simkoko katika riadha, Titus Simba(sasa marehemu) Habibu Kinyogoli, Hugo, Lucas Msomba, Nashoni Nyabwa, Mzee Kwimba wa Bandari katika ndondi. Rose Walele, Judith Ilunda, Edna John, Maimuna Mrisha na Rose Temba katika Netiboli; achilia mbali katika soka ambako ndio hasa mahsusi kwa leo.
Najua watu wengi waliokuwepo miaka
ya nyuma wanaweza wakanielewa zaidi nitakapoizungumzia makala yangu ya leo. Nini hasa kilichotukumba hadi watu hao juu siwaoni au hatuwaoni leo.
Suala la elimu, kwa kiasi kikubwa ndio lilichangia sana kuua michezo. Leo, ninapozungumzia elimu nina maana ya kushuka kwa thamani ya mwalimu na kushuka kwa kiwango cha ufundishaji (sio elimu yenyewe) mashuleni.
Zama zile, mtu akiitwa mwalimu au mtoto wa mwalimu, alikuwa anaheshimika sana na ilikuwa si rahisi mwanafunzi wa wakati ule kukaa meza moja na mwalimu kupiga soga tofauti na ilivyo leo. Waalimu wakati huo, walikuwa wanajiheshimu sana kimavazi na kimaadili kwa ujumla. Walimu wa wakati huo walizingatia ule usemi wa wahenga kuwa “ualimu ni kazi ya wito”.
Suala la ufundishaji, namuangalia mwanafunzi wa wakati ule asubuhi akiingia darasani tu anakutana na somo la Hesabu, Kiswahili, Kiingereza halafu tunaenda mapumziko ya dakika kama 25 hivi tukirudi darasani unakutana na somo la Historia, Jiographia, Siasa halafu unatoka mnaenda kupata chakula cha mchana mkirudi mnakutana na Sayansi, Sanaa na maarifa ya nyumbani na kwa wiki mara moja mnakutana na somo la dini. Masomo yote hayo, walimu ni lazima waingie darasani na kufundisha kwa ufasaha na kuwapa na kazi za kufanya nyumbani “Home work”. Ukirudi nyumbani, baba akiangalia kazi nzuri iliyofanywa na walimu hana neno na wewe, hivyo unakuwa huru kuanzia saa kumi hadi saa moja usiku, hivyo unaenda kucheza michezo ikiwemo kandanda au soka.
Mwanafunzi wa leo anapotoka shuleni mzazi ukichukua madaftari yake kuangalia nini alichojifunza machozi yatakutoka; ni masomo hayazidi manne na ndani yake Hesabu na Kiingereza huyakuti, hivyo kwa mzazi mwenye kupenda maendeleo ya mwanao, ni lazima ile saa kumi ya kucheza mtoto atapelekwa kwenye masomo ya ziada yaani “Tuition”.
Hapo ndipo kipaji cha mtoto kinapozidi kupotea kama sio kufa kabisa.
Zama zetu, ile ikifika saa kumi kila mtoto yupo kiwanjani na viwanja vya mtaani vilikuwa vingi sana; lakini hiyo siyo mada yangu leo ya kwa nini leo viwanja sivioni!
Kimsingi, wote tulikuwa viwanjani tukicheza michezo ya aina mbalimbali ambayo iliboresha vipaji vyetu.
Mfano tukicheza mchezo wa kugusa mara moja huku unafunga goli la mwenzako “One touch”. Mchezo huu ulisaidia kupata wachezaji wenye uwezo wa kumiliki mpira na kuachia mara moja kama vile akina Aluu Ally, Method Mogella, Ramadhani Lenny, Jumanne Shengo, Mtemi Ramadhani, Hussen Masha na wengine wengi. Kulikuwa na mchezo unaitwa gombania goli; huo unakuwa na golikipa mmoja na wote mnamfunga yeye, hivyo kila mtu anapigana ili afunge akakae golini, hivyo tuliwapata akina Omary Mahadhi(sasa marehemu), Elias Michael(sasa marehemu), Athuman Mambosasa(sasa marehemu), Iddy Pazi, Juma Pondamali, Moses Mkandawile, Spear Mbwembwe, Kichochi Lemba, Hamis Kinye, Joseph Fungo na wengineo. Pia tuliwapata wafungaji kama vile akina Adam Sabu(sasa marehemu), Zamoyoni Mogella, Abdallah Burhani, Peter Tino, Gibson Sembuli(sasa marehemu), Venance Mwakalukwa “Best maridadi”, Ally Machela na wengineo.
Kulikuwa na mchezo wa kona, mtu mmoja anapiga kona wengine tunapiga vichwa kufunga, hapo vile vile tuliendeleza vipaji vya kupiga kona. Tulipata watu wapiga kona wazuri sana kama Abdulhamid Juma(sasa marehemu) Mohamed Kajole(sasa marehemu), Yusuph Bana(sasa marehemu), Fred Felix Minziro(sasa marehemu), Kenny Mkapa, Abubakari Kombo na wengineo wengi tu.
Pia tulipata wapiga vichwa wazuri sana kama Kitwana Manara Popat, Abdallah Luo(sasa marehemu), Abeid Mziba, Issa Athuman(sasa marehemu, Riziki Nassoro, Anthony Kifaro na wengine wengi.
Tulikuwa na mchezo unaitwa dobo dunda. Mtu akiingiziwa mpira katikati ya miguu yake, anapigwa magumi hadi akimbie aende akashike mahali ambapo mmepanga; ni mbali kama mita 50 vile. Kwa tukio hilo tulitengeneza wakimbiaji wazuri sana kama akina Willy Mwaijibe(sasa marehemu), Leonard Chitete(sasa marehemu), Sunday Juma, Kingsley Mwalilo na wengineo.
Kulikuwa na mchezo wa kushindana kupiga danadana, mtu anapiga hadi 1000; inakujenga uwezo wa kumiliki mpira kama walivyokuwa nao akina Mbwana Bushiri ‘Director’, Mohammed Hassan ‘Msomali’, Captain John Lymo; Sunday Manara ‘Computer’, Method Andrew ‘Master’, Charles Boniface, Samweli Owu, Ally Maumba, Hamis Thobias Gaga, Maico Paul ‘Nailon’.
Michezo hiyo yote tulikuwa hatufundishwi na walimu, ilikuwa inaanza kabla ya kupiga mtanange wenyewe wa watu 11, yaani ‘full game’.
Michezo hiyo yote hatuioni leo kwa sababu watoto hawana muda na wakati huo wachezaji wote ni lazima watoke mashuleni tofauti na ilivyo leo.
Asilimia 70, ukiacha ule uzao wa Kipingu wa kina Kaseja Juma, Mussa Mgosi, Nico Nyagawa, Haruna Moshi, Fred Mbuna na Wazir Mahadhi, wachezaji wengi baada ya kushindwa masomo na kukaa nyumbani, ndio wakaamua kwenda viwanjani kutafuta maisha katika njia nyingine ya soka. Hapo ndio unawakuta akina Juma Nyoso, Godfrey Taita, George Kavila, Ramadhani Chombo, Athumani Iddy na wengineo ambao wamecheza bila misingi ile ya awali waliyokuwa nayo akina Ahmed Amasha, Raha Msigalla, George Kulagwa, Nichodemus Njohole na Abdallah Mwinyimkuu (sasa marehemu), ambao tulianza kuwaona shuleni hadi ngazi ya juu ya elimu ambayo pia tuliwakuta akina Mwalusako, Leonard Tadeo, Denis Mdoe, Madundo Mtambo na wengineo.
Nasikia serikali leo inataka kurudisha michezo mashuleni, ni jambo zuri, lakini serikali ni lazima itambue tatizo liko wapi ili ifanikishe azimio hilo lililokusudiwa, vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu.
Serikali ni lazima itoe kwanza kipaumbele katika suala la walimu; ni lazima iboreshe mishahara yao ili walimu wasitegemee kuuza visheti na karanga shuleni au kutegemea masomo ya ziada kwa wanafunzi.
Pia serikali ni lazima ihakikishe inawalipa walimu mishahara kwa muda unaotakiwa na kupatiwa vifaa vilivyo bora vya kufundishia.
Walimu pia ni lazima waelimishwe maadili ya ualimu kama wazazi. Wanatakiwa wawe kioo cha jamii; wawe wanajali kulea na kuwafundisha vijana kwa muda wote ili wazazi tusiwapeleke watoto wetu masomo ya ziada na jioni wakajumuike katika viwanja vya soka hapo ndio michezo inaweza ikarudi kama zamani.
E-mail: kennymwaisabula@yahoo.com
KENEDY MWAISABULA
“MZAZI”
Mi naona serikali ni vema iongeze mishahara ili waweze kujituma kusiwe na haja ya wanafunzi kwenda tuition ili kuwapa muda wakushiliki ktk michezo badala ya kwenda tuition
ReplyDelete