KLABU ya SC ya Dar es Salaam ni miongoni mwa timu za hapa nchini ambayo kwa miaka mingi imebahatika kuwa na washambuliaji mahiri ambao kwa kipindi kirefu wameiletea mafanikio makubwa klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi.
Mmoja wa washambuliaji ambaye alivuma sana kwa kipindi kirefu akiwa na klabu hiyo kati ya mwaka 1981 mpaka 1991 na kuiletea mafanikio makubwa ni mshambuliaji machachari na mwenye chenga za maudhi Malota Soma.
Umahiri wa mchezaji huyu ulitokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kupiga chenga za maudhi, kufunga mabao na kusababisha kupatikana kwa mabao kwa timu yake na kutokana na sababu hiyo wapenzi wa soka nchini walimbatiza jina la ‘Ball Juggler’ wakimaanisha kuwa alikuwa na uwezo wa kuchezea mpira atakavyo.
Malota kwa hivi sasa hasikiki na wala haonekani viwanjani kama zamani, kwa sababu amestaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 1999 akiwa na timu ya Tanzania Stars ambayo inashirikisha wachezaji wa zamani waliostaafu kucheza soka ya ushindani.
Ukilinganisha uwezo wa mshambuliaji huyu Malota Soma na wachezaji wa sasa wa klabu ya Simba ni tofauti kabisa, kwani licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga chenga za maudhi, pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao.
Umahiri wa Malota katika soka ulikuwa mkubwa mno, kwani alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji, kuanzia winga zote mbili saba na kumi na moja na katikati tisa na kumi.
Licha ya uwezo mkubwa aliokuwa nao Malota wa kupachika mabao, pia washambuliaji wenzake wa Simba aliokuwa akicheza nao pia nao walikuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao ulinganisha na safu ya ushambuliaji ya Simba ya hivi sasa.
Katika kipindi hicho wakati Malota Soma anacheza soka katikati kulikuwa na washambuliaji wawili ambao pia walikuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao ambao ni Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’ na Edward Chumila (marehemu) wakati winga ya kushoto kulikuwa na winga machachari na mwenye kasi Sunday Juma.
Washambuliaji wote hawa walikuwa na uwezo wa kupachika mabao kama alivyokuwa Malota Soma ‘Ball Juggler’ na mwiba mkali kwa mabeki wa timu pinzani waliokuwa wakikabiliana nao na hasa Zamoyoni Mogela ambaye wapenzi wa soka nchini walimbatiza jina la ‘Golden Boy’.
Akizungumzia mechi anayoikumbuka zaidi wakati anacheza soka ya ushindani, Malota Soma anaitaja mechi iliyokutanisha timu yake ya Simba dhidi ya National Al- Ahly FC ya Misri, mchezo uliochezwa katika uwanja wa CCM Kirumba Mjini Mwanza mwaka 1985.
Mchezo huo ulikuwa ni wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika na matokeo ni kwamba Simba waliibuka washindi kwa kuwafunga National Al-Ahly ya Misri mabao 2-1.
Mechi hiyo Malota Soma anaikumbuka vizuri mno mpaka leo hii kwa sababu, licha ya yeye kutofunga goli siku hiyo, lakini alicheza vizuri mno na yeye ndiye aliyetoa pasi kwa mfungaji wa bao la kwanza Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’. Bao la pili na la ushindi siku hiyo lilifungwa katika dakika 15 hivi kabla ya mchezo kumalizika na kiungo mahiri Mtemi Ramadhani.
Kwa ushindi huo, Simba waliondoa ile dhana iliyokuwa imejengeka miongoni mwa wapenzi wa soka nchini kuwa timu za Tanzania haziwezi kuzifunga timu za Misri.
Kihistoria Malota Soma alianza kujulikana katika ulimwengu wa soka mwaka 1977 alipomaliza elimu ya Msingi aliposajiliwa na klabu ya daraja la pili iliyojulikana kwa jina la Jogoo FC ya Mjini Morogoro.
Mwaka 1978 Malota Soma alihama timu ya Jogoo FC na kujiunga na Reli FC pia ya Morogoro iliyokuwa inashiriki ligi daraja pili wakati huo. Baadhi ya wachezaji maarufu aliokuwa nao Reli ni kama Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’, Ali Jangalu, Stephen Mdachi, Sospeter Mwaluko na Ayoub Kahewanga.
Mwaka 1979 Malota Soma alihama klabu ya Reli na kujiunga na Tumbaku FC pia ya Morogoro iliyokuwa ikishiriki ligi darala la pili wakati huo. Baadhi ya wachezaji maarufu aliokuwa nao Tumbaku ni John Simkoko, Zamoyoni Mogela, Thobias Nkoma (marehemu), Shabani Mussa, Bona Bruno na Hussein Ngulungu.
Malota akiwa Tumbaku mwaka huo huo wa 1979 alichaguliwa kwa mara ya kwanza timu ya Taifa ya vijana iliyokuwa ikinolewa na kocha mzoefu Mohamed Msomali.
Baadhi ya wachezaji aliokuwa nao timu ya Taifa ya vijana ni Abdul Amasha, Hussein Iddi, Thobias Nkoma (marehemu), Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’, Ayoub Mzee, Sospeter Mwaluko na Juma Kiruzeruze.
Malota Soma alikaa na timu ya Tumbaku miaka miwili ambapo mwaka 1981 alihama timu hiyo na kujiunga na Simba SC ya Dar es Salaam maarufu kama ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Baadhi ya wachezaji aliowakuta Simba na kucheza nao ni Mohamed Kajole ‘Machela’ (marehemu), Daudi Salum ‘Bruce Lee’, George Kulagwa, Sunday Juma, Mohamed Bakari ‘Tall’, Rahim Lumelezi, Abbas Kuka, Nico Njohole, Mussa Kiwhelo (marehemu), Thobias Nkoma (marehemu) na wengine wengi.
Mwaka huo huo wa 1981 Malota akiwa na klabu ya Simba alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya Mkoa wa Dar es Salaam maarufu kama Mzizima United na katika michuano ya Taifa Cup ya mwaka huo Mzizima United ilitwaa taji la hilo.
Malota Soma alikaa na klabu ya Simba miaka 10 mfululizo , kabla ya mwaka 1991 kutimkia nchini Oman kucheza soka la kulipwa katika klabu ya daraja la kwanza Sohari FC.
Alirudi nchini mwaka 1993 na kujiunga na klabu yake ya zamani ambayo safari hii alikaa nayo misimu mitatu ambapo mwaka 1997 alijiunga na timu ya Tanzania Stars ambayo inashirikisha wachezaji wa zamani.
Malota Soma alistaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 1999 na klabu yake ya mwisho kuichezea ilikuwa ni Tanzania Stars. Anasema kuma aliamua kustaafu kucheza soka ya ushindani ili kuwaachia vijana chipukizi waonyeshe vipaji vyao.
Unasahau picha baba
ReplyDelete