WAKATI timu zinazotarajia kushiriki katika michuano ya Klabu Bingwa afrika Mashariki na Kati zinatarajiwa kuwasili leo, Shirikisho la Kandanda Nchini, TFF bado halijalipa deni la hoteli za Tansoma na Tanso la sh. Milioni 35.
Deni hilo linatokana na TFF kuandaa mashindano ya Chalenji yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana na sasa ni miezi saba tokea kumalizika kwa mashindano hayo.
Meneja Mwendeshaji wa hotel ya Tansoma (Paradise Express), Mohamed Hussein alisema kuwa jumla ya timu tatu, Sudan, Rwanda na Ivory Coast zilikaa katika hotel hiyo pamoja na watu wawili walioteuliwa na TFF kwa ajili ya kuzisimamia timu hizo.
Hussein alisema kuwa baada ya kulipa kiasi cha fedha, hotel hilo ambayo ilitoa punguzo la nusu bei kwa kila chumba bila kujali hadhi ya vyumba kwani hata chumba cha dola 135 kiliuzwa kwa dola 60.
“Vyumba vyetu vinaanzia dola 90 kwa chumba kimoja wakati chumba chenye vitanda viwili kinauzwa dola 105 na kile cha ‘suit’ dola 135, kwa vile lengo letu ni kusaidia mashindano kufanyika, vyote tuliuza kwa bei moja, yaani dola 60, hata hivyo hatulipwa mpaka sasa,” alisema Hussein.
Alisema kuwa TFF walitanguliza kulipa dola 25,000 kabla na kubaki dola 14, 629 ambazo wanazisotea mpaka sasa.
Mbali ya deni la hotel ya Tansoma, Hussein alisema kuwa vile vile wanawadai TFF sh. Milioni 13 zikiwa gharama za waamuzi kulala katika hotel yao ya Tanso ya Karikoo iliyokuwa inatumiwa na waamuzi na baadhi ya makocha wa timu.
Alisema kuwa gharama zima ya kulala katika hotel hiyo ni Sh. Million 18.7 TFF ilitanguliza sh. Million 5.6 na tangu walipe kabla ya huduma hiyo kufanyika, mpaka leo hawajalipa.
“Inatuvunja nguvu kibiashara, hatuwezi kuendelea hivyo maana tangu tuanze kufuatilia ni miezi mingi sana sasa, fikiria hii ni biashara gani tunafanya, inatuweka katika hali ngumu,” alisema Hussein.
Alisema kuwa waliwasiliana na Kayuni (Sunday) ambaye wakati huo alikuwa kaimu Katibu Mkuu, lakini mpaka sasa bado mambo magumu pamoja na kupewa majibu ya matumaini.
“Tuliwasiliana na katibu wa sasa, Angetile Osiah, lakini bado mambo ni magumu mbali ya kumpigia Rais wa TFF, Leodegar Tenga ili kupata fedha zetu, bado tukambiwa tusubiri,” alisema.
Alisema kuwa kutokana na hali kuwa mbaya kwetu, tuliwasiliana na wakili wetu, kampuni ya Marando, Mnyele & Co. Advocates na kuwapelekea barua Mei 31huku tukitoa sku saba tulipwe, lakini mpaka sasa kimya.
“Tunafanya mpango wa kuchukua hatua za kisheria, pamoja na kwenda mahakamani, suluhu la suala hili ni kulipwa fedha zetu,” alisema.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alithibitisha sakata hilo na kusema kuwa watalipa deni hilo bila tatizo.
“Tansoma ni wadau wetu, vile vile tunampango wa kuweka timu hizi kwa ajili ya michuano ya Kagame, tutawalipa, kudaiwa ni jambo la kawaida kwa taasisi yoyote duniani,” alisema Osiah.
Mwandishi:Majuto Omary
No comments:
Post a Comment