Search This Blog
Tuesday, June 14, 2011
MAN UTD KWELI INABEBWA? USHAHIDI HUU HAPA!
mwamuzi Howard Webb ni kweli anaipendelea Man Utd?
Na Geofrey Lea
Ujumbe wa Twitter uliotumwa na Ryan Babel aliyekuwa mchezaji wa Liverpool kipindi hicho ambao ulikuwa umesindikizwa na picha ya kutengenezwa iliyokuwa inamuonyesha mwamuzi Howard Webb akiwa amevalia jezi ya Man United ni moja ya kelele zisizoisha dhidi ya Man United toka kwa wapinzani wake wanaodai kuwa klabu hii hubebwa na waamuzi pamoja na ukweli kuwa takwimu zinaonyesha kinyume cha yale ambayo wengi wanadhani .
Mashabiki wengi wa soka hasa wale wanaofuatilia kwa karibu ligi kuu ya England wamejenga imani kuwa Manchester United ni klabu inayopendelewa na waamuzi wanaochezesha mechi zao . Imani hii si kwa mashabiki tu bali imehamia hata kwa waandishi wa habari za michezo hususani soka na wachambuzi wa mechi za ligi kuu ya England ambapo utawasikia wakisema kwa lugha ya kiingereza kuwa ‘YOU DON’T GET THOSE AT OLD TRAFFORD ‘ yaani huwezi kupata hizo Old Trafford wakimaanisha kuwa timu pinzani hazipati penati Old Traford , wengine utawasikia wakisema kuwa ‘IF THAT WAS DOWN AT THE OTHER END IT WAS A PEN’ yaani ‘ kama hii ingetokea kwenye upande wa pili ingekuwa penati bila wasiwasi ‘ na wengine wakiubatiza ule muda wa nyongeza wa dakika za majeruhi kwa jina la ‘Fergie Time’ yaani muda wa fergie . Lakini swali la kujiuliza ni moja , je tuhuma hizi kwa waamuzi na kwa Man United zina ukweli wowote ndani yake ? Takwimu zinasema si kweli .
Msimu huu wakiwa wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi baada ya michezo 29 huku wakiwa wamefuzu kwa hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa na nusu fainali ya kombe la FA,Manchester United wamezawadiwa jumla ya penati tano katika michuano hii yote wanayoshiriki , wakiwa Old Traford dhidi ya Liverpool kwenye kombe la FA , Old Traford tena kwenye EPL dhidi ya Arsenal , na dhidi ya West ham pia kwenye EPL , na ugenini wamepata penati dhidi ya Fulham kwenye EPL na dhidi ya Rangers kwenye ligi ya mabingwa. Katika penati hizo zote zilizotajwa United wamefanikiwa kufunga penati tatu tu , hii ikimaanisha kuwa penati zimechangia kwa asilimia 3.8 % ya magoli yaliyofungwa na Manchester United msimu huu na katika penati hizi ni penati moja tu ambayo United walipewa dhidi ya Liverpool ambayo unaweza kusema walipendelewa .
Kwa wapinzani wa United ambao wengi ndio wanaongoza hizi nyimbo za kuwa marefa wengi ni wanazi wa Mashetani wekundu , Arsenal wamezawadiwa penati 14 msimu huu huku nyingi kati ya hizo zikiwa za utata hasa pale anapohusika Mmorocco Marouane Chamakh . Kati ya penati hizi arsenal wamefanikiwa kufunga kumi na hii inamaanisha asilimia 11.8% ya mabao yote ambayo Arsenal imefunga yamechangiwa na penati . Kwa upande mwingine Chelsea wamezawadiwa penati 10 ambazo wamefunga 8 na kukosa 2 na ikiletwa kwenye mahesabu ya asilimia utagundua asilimia 9.5 ya mabao yaliyofungwa na Chelsea yametokana na matuta . Matajiri wa Manchester City wamepata jumla ya penati 9 ambazo wamefunga 7 na kukosa mbili kwa asilimia ya 9.3 ya mabao yao yote . Liverpool nao wamepewa penati 8 ambazo wamefunga 6 huku wakiwa na asilimia 11.8 ya mabao ya penati .
Takwimu hizi zinawatia aibu wale wanaodai United inapendelewa hasa kwa kutumia kigezo cha penati wanazopata . Ukiwatazama Arsenal wamepewa penati ambazo ni zaidi ya mara tatu ya zile walizopata United huku timu zingine zilizotajwa hapo juu nazo zikiwa zimezidi United sana tu kwa penati ambazo waamuzi wanatoa , na hata ukitazama asilimia ya mabao ambayo timu inafunga kupitia penati utaona kuwa United ndio yenye asilimia chache kuliko wenzie , sasa kwa penati tu ni nani mwenye faida ya kupendelewa na marefa ? hiyo nawaachia wasomaji .
Tukiwa hapa hapa kwenye mjadala wa penati hebu turudi nyuma na kutazama idadi ya penati ambazo timu mbalimbali za EPL zimepewa tangu mwaka 2003 ambapo takwimu hizi zilianza kutunzwa .
Liverpool – 36
Arsenal – 35
Chelsea – 30
Aston Villa – 27
Fulham – 24
Tottenham – 23
Blackburn – 22
Man City- 22
Everton 21.
Pamoja na kuwa timu inayoshambulia zaidi kwenye ligi kuu ya England Manchester United imefunga mabao machache kupitia penati kutofautisha na wapinzani wake wakuu kwenye ile big four ambao ni Arsenal , Liverpool na Chelsea , United wamefunga mabao machache kwa penati kuliko hata Aston Villa , Fulham na Tottenham . Penati zimewapa United jumla ya asilimia 5.1 ya mabao yao kulinganisha na Liverpool , Arsenal na Chelsea ambao wamepata asilimia 9.1% , 7.5%, na 6.6% .
Tukiangalia upande wa pili wa penati ambazo zimepewa kwa timu ambazo zimecheza na United utagundua kuwa penati 13 zimegawiwa kwa wapinzani wa United huku wenzie kina Liverpool wakiwa wameshuhudia wapinzani wakipewa penati 15 , Arsenal 17, na Chelsea 12. Hii inamaanisha kuwa mabao ambayo United imefungwa kwa njia ya penati ni sawa na asilimia 7.2 % , huku Liverpool wakifungwa sawa na asilimia 7.4 ya mabao kupitia penati huku Arsenal na Chelsea wakiwa wamefungwa sawa na asilimia 8.1 ya mabao kupitia kwa mikwaju ya penati . Takwimu hizi kwa upande mmoja zinafanana .
Kama tukifananisha asilimia zote hizi za jumla ya mabao yote ambayo timu zimefunga na zimefungwa kupitia kwa penati ambapo United wamefunga asilimia 5.1 na wamefungwa 7.2 ukiongeza namba hizi utapata – 2.1 /% utagundua kuwa United wanaonekana kuwa na wastani mbaya kuliko wenzie ambao ni Liverpool ( wakiwa wamefunga 9.1% na wamefungwa 7.4% na ukuzidisha unapata wastani wa jumla wa +1.7% na Arsenal wao wamefunga 7.5% na wamefungwa 8.1% wanapata wastani wa kuzidisha ambao ni -0.6 na mwisho Chelsea ambao wamefunga 6.6% na wamefungwa -1.5% .
Kwa faida tu ya wale wanaopenda rekodi za takwimu hizi kati ya timu kubwa nne za England ( United , Chelsea , Liverpool na Arsenal ) ni Liverpool pekee ambao wameonekana kufaidika sana na maamuzi ya penati toka mwaka 2003 kuliko timu zingine , cha kuchekesha ni jinsi mashabiki hawa hawa wa Liverpool ambao wanaongoza kelele za kusema kuwa United inapendelewa na waamuzi . Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa tangu mwaka 99 Liverpool wamezawadiwa jumla ya penati 53 tofauti na United ambao wamezawadiwa 46 . N takwimu zingine zinaonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwa Premier league mwaka 92 hadi leo hii Manchester United wamezawadiwa jumla ya penati 88 ambazo ni sawa na wastani wa 4.7 kwa kila msimu na kati ya hizo wameweza kufunga 66 na kukosa zilizobaki na hii inamaanisha kuwa United wamefunga asilimia ndogo ya 4.7% ya mabao ya penati kati ya mabao yote waliyofunga tangu kipindi hicho . Kwa kukifananisha kiwango hiki cha muda wote na viwango vya msimu huu tu vya timu nyingine tunaweza kufikia muafaka kuwa United imepata faida ndogo sana ya penati toka kwa waamuzi kwa kulinganisha na wenzie tangu kuanzishwa kwa ligi kuu ya England .
Tuziache penati kando na tutazame maamuzi mengine ya uwanjani . Hapa ndio kwenye utata zaidi kwani ushahidi unajidhihirisha wenyewe kwa kuyatazama matukio mbalimbali yanayotokea ambayo ndio hasa kiini cha kelele za kuwa United wanafaidika na maamuzi ya upendeleo toka kwa marefa .
Wengi wanarejea kwenye matukio yaliyotokea kwenye michezo baina ya United na Stoke City na West Bromwich Albion ambapo wanadai kuwa United wana bahati kuongoza ligi kwani kwani Gary Neville alinusurika kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwenye michezo yote hii miwili kwa matukio tofauti yanayofanana huku West Brom wakinyimwa penati iliyoonekana dhahiri kabisa .
Wakati kukiwa na ukweli thabiti kabisa kwenye kesi ya West Brom kunyimwa penati kuna kitu kilichotokea kwenye mchezo huu ambacho wengi aidha wamekisahau , hawakukiona au wanakifumbia macho kwa unafiki wa kishabiki . Man United nao walinyimwa penati na mwamuzi huyu huyu aliyewanyima West Brom tena kwenye mchezo huu huu baada ya mchezaji wa West Brom kuunawa mpira kwenye eneo la hatari baada ya mpira uliopigwa na Fabio . Wakati wengi wanasema Neville ambaye kwa sasa amestaafu alinusurika kutolewa kwa kadi nyekundu wanasahu kuwa kadi ya njano ya kwanza iliyoonyeshwa kwa Neville haikuwa sahihi kwani hakucheza rafu bali aliucheza mpira . Pengine tunaweza kutofautiana kwa tafsiri ya kipi ni rafu na kipi si rafu lakini yaliyo wazi yanaonekana bila ubishi .
Tukio lingine ambalo ningependa kuukumbusha ulimwengu ni bao la kusawazisha alilofunga Lee Bowyer wakati United ilipomenyana na Birmingham City bao ambalo lilifungwa kwenye dakika ya mwisho ya mchezo . Bao hili kimsingi halikupaswa kukubaliwa kama bao halali kwani kulikuwa na matukio manne (4) tofauti yaliyotokea yanapelekea bao hili kutokuwa halali . Kulikuwa na nyakati mbili ambazo zilitokea haraka haraka ambapo mshambuliaji wa Birmingham Nikola Zigic aliwaparamia mabeki wa United mabegani kwa kutumia mikono yake , ukiacha hilo kulikuwa na tukio la mchezaji wa Birmingham kuunawa mpira na mfungaji Lee Bowyer alikuwa ameotea , haya yote yalitokea ndani ya sekunde zisizopungua 50 ambapo Birmingham walifunga bao la kusawazisha . Hakuna shabiki wa United , mchezaji , kocha wala kiongozi aliyesikika akilalamikia bao lile .
Tukio lingine wanalosahau wengi ni mechi mbili baina ya United na Chelsea pale Old Trafford mwishoni mwa msimu uliopita na kule Stamford Bridge mechi ambazo ukiangalia kiundani ziliigharimu United kuweka rekodi ya kutwaa taji la nne mfululizo la EPL . Mechi ya kwanza ambayo timu hizi zilicheza ilikuwa pale Stamford Bridge ambapo Chelsea walishinda kwa bao moja bila , bao lililowekwa wavuni na John Terry kwa kichwa . Bao hili la Terry halikuwa halali . Didier Drogba akiwa kwenye nafasi ya kuotea alimn’ga’ngania WesBrown na kumwangusha chini na kwa kufanya hivyo akamtengenezea Terry Mazingira ya kufunga . Tukirejea mechi iliyochezwa Old Traford ambapo matokeo yalikuwa ushindi wa mabao 2-1 kwa Chelsea utagundua kuwa bao la ushindi lililofungwa na Didier Drogba halikuwa sahihi kwani Didi alikuwa ameotea kwa takribani robo tatu nzima ya mita na hivyo hivyo Chelsea wakatwaa ubingwa wa EPL . Swali kwa wale wanaopiga kelele juu ya kupendelewa kwa United , ni lini United iliwahi kutwaa taji kwa kuwa na faida ya maamuzi ya refa kama walivyopoteza msimu uliopita .
Maamuzi ya marefa hayajaiuma United kwenye EPL pekee bali hata kwenye ligi ya mabingwa . Mashetani wekundu walikuwa njiani kuelekea kwenye ushindi dhidi ya Bayern Munich msimu uliopita mpaka pale beki Rafael alipoonyeshwa kadi mbili za njano na hivyo kutolewa nje kwa kadi nyekundu , sawa kabisa lakini mwamuzi hakuona faulo aliyochezewa Rafael sekunde mbili zilizopita kabla na pengine rafu ile ndio iliyomnkera Rafael na kumpelekea kucheza rafu iliyomtoa yeye huku aliyemchezea akibaki uwanjani . Mwaka 2003 , bao la Paul scholes kwenye mchezo dhidi ya Fc Porto lilikataliwa kwa madai kuwa aliotea wakati alikuwa kwenye eneo ambalo hakuwa ameotea tena wazi kabisa , bao hili lingeipa United faida ya bao moja zaidi na hata lile bao la Costinha lililoipa Porto faida na kuitoa United lisingekuwa na maana .
Kwenye kombe la Carling msimu uliopita wakati United inapambana na Manchester City kwenye hatua ya nusu fainali City walizawadiwa penati isiyo sahihi kwa rafu aliyochezewa Carlos Tevez nje ya eneo la hatari lakini United walienda na kushinda mchezo huo , hivyo wakati mashabiki wa Man City wakilalama juu ya muda wa ziada ulioongezwa juu ya ule wa majeruhi wa dakika nne ambapo Michael Owen alifunga bao la ushindi wanasahau kuhusu penati waliyopewa lakini kwa United issue ya penati aliyopewa Tevez imesahaulika kwa mashabiki wa United , kwanini? Kwa kuwa United hawakuruhusu suala lile liwadhuru walijinyanyua kama wanavyofanya siku zote na kuyendelea na kazi iliyokuwa mbele yao na wakaitimiza kwa kumfunga City mabao 3-1 kwenye mechi ya marudiano na wakaelekea kutwaa kombe hilo . Na ni sababu hii ambayo inafanya maamuzi ambayo yanaiuma United yasahulike haraka kwa kuwa ni timu ya washindi ambao mara nyingi hawaruhusu kunyimwa ushindi na masuala madogo kwani mara nyingi maamuzi hayawadhuru kwani huendelea na kazi na kushinda mwishowe na hivyo kuondoa maana ya maamuzi mabovu dhidi yao .
Moja ya vitu ambavyo mashabiki wengi hutaja kama ushahidi wa United kupendelewa ni ule muda unaoongezwa zaidi ya zile dakika 90 yaani Stoppage Time ambao kule England hivi sasa mashabiki wameupachika jina la Fergie Time wakidai kuwa mara nyingi United inapofungwa marefa huongeza dakika za kuwatosha United kufunga bao aidha la kusawazisha au hata la ushindi . Wengi hurejea matukio kama lile lililotokea mwaka 1993 kwenye mchezo kati ya Man United na Sheffield United ambapo dakika 7 za ziada ziliongezwa dakika ambazo United wakiwa nyuma waliweza kusawazisha na kufunga bao la ushindi na tukio la hivi karibuni ambapo United walifunga bao kwenye sekunde ya 88 baada ya dakika nne za nyongeza kuwa zimeisha . Wanachosahau watu wengi ni kuwa kwenye tukio la kwenye mechi ya United na Sheffield refa aliumia na hivyo alibadilishwa na hii ilikuwa baada ya kuwa amehudumiwa uwanjani kwa muda wa dakika tano ambazo ukiaongeza na zile za kufidia kuumia kwa wachezaji na mabadiliko utaona kuwa hata dakika 7 zilizoongezwa hazikuwa zinatosha bali ilibidi ziongezwe dakika zaidi . Tukija kwenye tukio la hivi karibuni tena Baada ya muda kuwa umeongezwa wa dakika 4 Manchester City walipata bao la kusawazisha ambapo walitumia dakika zisizopungua mbili kushangilia na kurejea uwanjani wakiamini kuwa wamepata walau sare , baada ya hapo Sir Alex Fergusson alifanya mabadiliko ambapo alimuingiza Michael Carrick hivyo utagundua kuwa dakika moja na sekunde 27 zilizoongezwa juu ya ule muda wa dakika 4 ni sahihi kabisa na wala hakuna upendeleo .
Kwa hali ya kawaida mafanikio hujenga hisia za chuki inayotokana na wivu walio nao wale ambao hawajafanikiwa . Kama zinavyoonyesha takwimu kelele zote ambazo United wanapigiwa juu ya kupendelewa sio sahihi . Sio kwa suala la Penati wala maamuzi ya kawaida tena ukiingia ndani zaidi utaona kuwa United ndio wanaopaswa kulalamika kwa sababu wanaonekana kugharimiwa na maamuzi mengi yasiyo sahihi yaliyoenda dhidi yao . Kokote pale uendako timu yenye mafanikio ndio inayochukiwa sana na wapinzani , ilikuwa hivyo Enzi za kina Kenny Dalglish na Kevin Keegan na Liverpool yao iliyokuwa inatesa England ,ilikuwa hivyo kwa Juventus italia miaka ya 90 , na hata Bayern Munich pia . Kikubwa ni kuwa United hairuhusu maamuzi kuwazuia na mara nyingi yale ambayo yameenda kwa upande wao ndio yanayoonekana kuliko yale yanayoenda dhidi yao kwani si mara nyingi huwa yanawadhuru
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment