Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
GHARIKA!. Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka
Tanzania bara wameshusha mvua kubwa ya mabao 5-1 dhidi ya JKT Ruvu katika
mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uliomalizika jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Yanga waliuanza mchezo kwa kasi na iliwachukua
dakika 8 tu kutikisa nyavu za JKR Ruvu kupitia kwa winga wake machachari,
Mrisho Khalfan Ngasa `Anko`.
Dakika ya 15 ya kipindi hicho, Ngasa alitia
tena mpira kambani na kuandika bao la pili kwa wanajangwani waliokuwa na uchu
wa ushindi.
JKT Ruvu wakiwa doro muda mrefu waliendelea
kuoneshwa ufundi na Yanga na katika dakika ya 39 Mrundi, Didier Kavumbagu
aliipatia Yanga bao la tatu kufuatia kutumia vyema pasi ya Mrisho Ngasa.
Bao hili lilifungwa kirahisi kwasababu mabeki
wa JKT Ruvu walizembea kwa kudhani Kavumbagu ameotea.
Yanga waliendelea kushambulia na kutawala
mchezo, lakini mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, walikuwa
mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Yanga walianza mpira kwa
kulishambulia lango la wapinzani wao ambapo dakika ya 49 Mrisho Ngasa alifunga
bao lake la tatu na `kukamilisha hat-trick` kwenye mchezo wa leo.
Dakika tatu baadaye, Hussein Javu aliandika bao
la tano na kukamilisha karamu hiyo ya mabao.
JKT Ruvu walipata bao lao la kufutia machozi katika dakika ya 82 kupitia kwa mshambuliaji
wake, Idd Mbaga baada ya kupewa pasi nzuri na Damas Makwaya.
Baada ya mechi hii, Mrisho Ngasa alipewa mpira
wake na kuudunda dunda uwanjani, huku mashabiki wa Yanga wakimshangilia nyota
huyo.
Baada ya mchezo wa leo, Yanga wamefikisha
pointi 49 katika nafasi ya pili baada ya kushuka dimbani mara 23.
Azam fc wanaendelea kuwa kileleni kwa tofauti
ya pointi 4 na Yanga, lakini kizuri sasa timu hizi mbili zimelingana michezo.
Jumatano ijayo, timu zote mbili zitakuwa
uwanjani, ambapo Yanga wataumana na Kagera Sugar uwanja wa Taifa, wakati Azam
fc watakuwa wageni wa Ruvu Shooting uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Kwa ujumla Yanga walitawala mchezo wa leo ndani
ya dakika zote 90.
JKT Ruvu walipoa sana na kuonekana kukosa mipango ya aina yoyote.
Toka mwanzo walikuwa wamezidiwa katika idara
zote na kuwafanya Yanga kucheza kama watakavyo.
Si kawaida ya Kocha Fredy Felix Majeshi Baba
Isaya Minziro kutulia muda mwingi pale timu yake inapofanya vibaya, lakini leo
hii muda mwingi wa mchezo alitulia tuli.
Matokeo ya leo ni mabaya kwa Minziro kwani
anaendelea kubakia nafasi ya 9 kwa pointi 28, huku wakibakiza mechi mbili tu.
Sasa watahitaji kushinda mechi zote mbili
walizosaliwa nazo kibindoni ili kujinusuru kushuka daraja.
Kwa upande wa Yanga imewapa unafuu mkubwa
katika harakati zao za kutetea ubingwa wao.
Yanga na Azam fc wanachuanoa kuwania ubingwa,
na kila klabu inahitaji kushinda mechi zote ili kujiweka mazingira mazuri ya
kutwaa taji.
Azam fc wanahitaji kushinda mechi zote tatu ili
kuwazuia Yanga kubeba mwari .
Hata hivyo kama Azam fc atashinda mechi mbili
kati ya tatu alizosaliwa nazo na kufungwa moja, watafikisha pointi 59.
Wakati huo huo, Yanga wakishinda mechi zote tatu walizosaliwa
nazo watafikisha pointi 58 ambazo Azam fc atakuwa amevuka.
Kwahiyo Kama Azam fc atapata pointi 6 tu katika
michezo mitatu iliyosalia, rasmi Yanga
watakuwa wamevuliwa ubingwa wao kwasababu hawataweza kufikisha pointi 59 hata
kama watashinda kwa mabao 100 mechi zote.
Mchezo mwingine wa ligi kuu umepigwa katika
dimba la CCM Mkwakwani jijini Tanga ambapo Coastal Union walioneshana kazi na
Mgambo JKT.
Dakika 90 za mchezo huo zimemalizika kwa
maafande wa Mgambo JKT kuendelea kujisafishia njia ya kubaki ligi kuu msimu huu
baada ya kushinda mabao 2-1.
Ushindi wa Mgambo unakuwa sawa sawa na ule
walioshinda dhidi ya Yanga mechi iliypita uwanja huo huo wa Mkwakwani.
Baada ya mchezo huo, Afisa habari wa Coastal
Union, Hafidh Kido amesema kuwa mchezo ulikuwa wa kawaida sana, lakini Mgambo
walipata nafasi mbili wakazitumia na wao wakapata moja na kuitumia.
“Sasa mambo yamekuwa magumu kwetu. Mpaka sasa hatujafikisha pointi 30. Tumebakiza
mechi ngumu na Kagera Sugar na JKT Ruvu. Tunakaa na wachezaji wetu ili kupanga
mikakati ya kushinda michezo miwili iliyosalia. Ligi imekuwa ngumu , aaah! Naambiwa
nao JKT Ruvu wamekula mabao 5-1”. Alisema Kido.
Kwa matokeo ya leo, Mgambo wanapanda hadi nafasi
ya 10 na kuishusha Prisons baada ya kufikisha pointi 25 kibindoni, huku
wakisaliwa na mechi mbili tu.
Wajelajela wamaendelea kuonja joto la jiwe
baada ya kulala mabao 2-1 dhidi ya JKT Oljoro katika dimba la CCM Shk. Amri
Abeid Kaluta jijini Arusha.
Matokoe hayo yanawafanya Prisons waporomoke kwa
nafasi moja na sasa wanakalia nafasi ya 11 kwa pointi 22 baada ya kucheza mechi 24.
JKT Oljoro baada ya ushindi wa leo wamefikisha
pointi 18 katika nafasi ya 13, lakini bado matumaini ya kubakia ligi kuu
yanaonekana kuisha kabisa.
Ashanti United na Prisons zinafungana kwa pointi , hivyo vita inaendelea baina yao na
Mgambo JKT ambao angalau wamesogea mbele kwa pointi.
JKT Oljoro na Rhino Rangers wana asalimia kubwa
ya kushuka daraja, huku Mgambo, Ashanti
na Prisons mmoja wapo akijiandaa kuungana nao.
Tayari timu tatu zimeshapandaligi kuu ambazo ni
Stand United ya Shinyanga, Polisi Morogoro ya Morogoro na Ndanda fc ya Mtwara.
Mchezo mwingine ulipigwa dimba la Ali Hassain
Mwinyi, ambapo Rhino Rangers wameona jua baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0
dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kwa matokeo hayo, Rhino wanafikisha pointi 16
katika mechi 24 walizocheza, lakini wanaendelea kuburuza mkia.
Dhahiri inaonekana Rhino Rangers wameshashuka
daraja msimu huu, kwani wamebakiwa na mechi mbili tu ambazo wakishinda zote
watafikisha pointi 22 zilizopitwa na timu nyingine.
No comments:
Post a Comment