Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara,
Dar Young Africans wameibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera
Sugar katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uliopigwa jioni hii uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam.
Yanga walikuwa wa kwanza kuliona lango la Kagera
Sugar katika dakika ya 3 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Mganda Hamis Kiiza `Diego` kufuatia kumalizia krosi nzuri iliyochongwa na winga machachari, Mrisho Khalfan
Ngasa.
Yanga waliandika bao la pili katika dakika ya 34
kupitia kwa mshambuliaji wao raia wa Burundi, Didier Kavumbagu.
Kagera Sugar walifunga bao la kufutia machozi katika dakika ya 63 kupitia
kwa Daudi Jumanne baada ya beki wa pembeni wa Yanga, Oscar Joshua kuzembea
kuosha mpira katika eneo lao la hatari.
Kwa matokeo hayo, Yanga wanafikisha pointi 52 baada
ya kucheza mechi 24, pointi moja nyuma ya vinara Azam fc walioshindwa kucheza
mechi yao ya 24 leo hii dhidi ya Ruvu Shooting baada ya mvua kubwa kunyesha na
uwanja wa Mabatini mkoani Pwani kuwa katika hali mbaya.
Mchezo wa leo ulikuwa muhimu kwa Yanga, hivyo
wamepambana nadani ya dakika zote 90 kutafuta ushindi, ingawa Kagera Sugar
walionekana kuwa imara kwa kiasi kikubwa.
Kosakosa kwa timu zote zimeshuhudiwa ndani ya uwanja
wa Taifa, na dakika za lala salama Kagera walikuwa wanawashambulia Yanga
kutafuta bao la pili la kusawazisha, lakini mabeki walikuwa makini kuzuia hatari
hizo.
Hata hivyo, yanga wangepata mabao mengi zaidi kama
isingekuwa uzembe wa washambuliaji wake, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu, Mrisho
Ngasa na Hussein Javu.
Kwa nyakati tofauti, washambuliaji hawa walipata
nafasi za kufunga, lakini walipungukiwa maarifa ya kumtungua kipa wa Kagera
Sugar, Agaton Antony.
Sasa Yanga wamebakiza mechi mbili dhidi ya JKT
Oljoro mwishoni mwa wiki hii katika uwanja wa Shk. Amri Abeid jijini Arusha, na
watafunga msimu na Simba aprili 19 mwaka huu uwanja wa Taifa.
Hali ya uwanja wa Mabatini ilikuwa namna hii leo
Ili kutetea ubingwa wao, Yanga wanatakiwa kushinda
mechi zote mbili, huku wakiwaombea dua mbaya Azam fc wenye michezo mitatu
mkononi.
Endapo Yanga watashinda mechi zao mbili
walizobakiza, watafikisha pointi 58
ambazo Azam fc wataweza kuzivuka kama watashinda mechi mbili tu kati ya tatu
walizosaliwa nazo.
Nafasi ya ubingwa bado ni wazi na mpaka sasa huwezi
kutabiri nani atatwaa ndoo msimu huu.
Mechi nyingine ilitakiwa kupigwa katika dimba la
Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani baina ya
wenyeji wa uwanja huo, Maafande wa Ruvu Shooting dhidi ya Vinara Azam fc,
lakini mechi hiyo imeahirishwa mpaka kesho baada ya mvua kubwa kunyesha na
kuharibu mandhari ya uwanja huo na sasa mechi hiyo atachezwa hapo kesho.
Licha ya Yanga kushinda leo, Azam fc bado wapo
kileleni kwa pointi moja zaidi ya Yanga, lakini wana michezo mitatu mkononi.
Kama watashinda mchezo wao wa 24 hapo kesho, basi
watakuwa wanahitaji pointi tatu tu katika mechi mbili zitakazobaki ili
kujitangazia ubingwa msimu huu.
Mechi ya kesho itakuwa na ushindani mkubwa kwa Azam
fc kutokana na rekodi ya Ruvu Shooting katika dimba la Mabatini ambapo wanaonekana
kuwa wagumu na hutoa ushindani mkubwa zaidi.
Baada ya mechi ya kesho, Azam fc mwishoni mwa wiki
watasafiri kwenda Mbeya kuwafuata wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City katika
dimba la Sokoine jijini humo.
Hii itakuwa mechi ngumu zaidi kwa kocha Joseph
Marius Omog wa Azam fc kwasababu Mbeya City wapo katika ushindani wa nafasi ya
pili msimu huu.
Pia hawana rekodi ya kufungwa katika dimba lao tangu
kuanza kwa msimu huu.
Si Yanga wala Simba aliyetoka na pointi tatu katika
uwanja huo mgumu kwa timu vigogo.
Baada ya Mbeya, mechi ya mwisho kwa Azam fc itakuwa
aprili 19 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi, aprili 19 mwaka huu.
kesho mpira fitna tupo mlandizi tuone hao azam washinde wanafungwa moja tu hawarudishi hapa ndio bongo mpira unachezwa ndani na nje uwanja
ReplyDeleteKweli Watanzania tumeathirika kifikra na kiakili,ubabaishaji umekuwa kila kona kuanzia serikalini hadi ktk jamii.Hivi mpira fitna ndiyo nini?Tumekuwa wagumu wa kukabiliana na changamoto za Dunia ya mageuzi ktk kila sekta,badala yake tumejikita kwenye mbinu chafu za kuwadhuru wapinzani wetu,ndiyo tumeona hata wenye mamlaka wanavyohangaika na kutumia nguvu kubwa ikibidi hata kuuwa ili kuwazima wapinzani.Zama za kuhujumiana hazina nafasi ktk dunia ya leo,kama yanga mmejipaga kuihujumu azam ili ifungwe kama ulivyocoment hapo juu,unafikiri hujuma zina tija gani ktk soka la kileo?Pambana uwanjani ktk kusaka mafanikio,siyo kujibanza ukutani na kuandaa mikakati ovu kwa mpinzani wako.Soka lichezwe uwanjani na aliyejiandaa vizuri ashinde,tuache kuiga mikakati ovu ya watawala ya kuwafanyia fitna wapinzani wao,mara ugaidi,mara hawamalizi mwaka watakufa,mara wawalipue kwa mabomu na kusema wamejilipua wenyewe basi ilimradi wachafue taswira yao njema.Maendeleo ya kweli katika sekta yoyote yawe ya kijamii,kisiasa,kiutamaduni au kimichezo huletwa kwa mikakati thabiti na mapinduzi ya kifikra iliyojikita kwenye uwajibikaji wa pamoja,siyo kwa fitna na majungu.Tuamke.
ReplyDelete