Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TIMU tatu mpya zitakazocheza ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015 tayari zimeshajulikana na kinachosubiriwa ni kupata timu tatu za kushuka daraja ili kuwapisha wageni.
Watu wa Shinyanga msimu ujao watafaidi uhondo wa wa ligi kuu baada ya vijana wao wa Stand United kupanda daraja msimu huu.
Nao wazee wa Ndanda fc kwa `roho safi` kutoka mkoani Mtwara watafurahia mitanange ya ligi kuu baada ya timu yao kupanda daraja.
Timu ya tatu ni Polisi Morogoro ambayo ilikuwepo msimu wa mwaka jana, lakini ilishuka na kupanda msimu huu tena.
Wakati wanashuka pamoja na Africa Lyon, na Toto Africans ya mwanza, Polisi Morogoro waliahidi kurudi ndani ya mwaka mmoja na kweli wamefanikiwa.
Lyon na Toto zimeshindwa kurudi ligi kuu kwasababu ya kushindwa kuhimili mikikimikiki ya ligi daraja la kwanza msimu huu.
Wakati timu hizi tatu zikishuka msimu wa mwaka jana, ziliwapisha Mbeya City, Rhino Rangers, na Ashanti United.
Timu tatu zilizopanda msimu huu, ni Mbeya City yenye uhakika wa kusalia ligi kuu kwa asilimia 100.
Ashanti United wapo katika hali ngumu zaidi ambapo wanachuana na Prisons, Mgambo JKT na JKT Ruvu kukwepa kushuka daraja.
Rhino Rangers tayari walishakata tiketi ya kuporomoka daraja, huku nao JKT Oljoro wakionekana kuungana na safari hii ya kushuka daraja. Hakuna miujiza juu ya hili.
Kinachosubiriwa kwa hamu ni kuona kati ya timu mpya tatu zilizopanda, nani atarithi mikoba ya Mbeya City, Rhino Rangers na Ashanti United kwa maana ya ushindani ndani ya ligi kuu msimu huu.
Wadau wa mikoa ambayo timu hizi tatu zimeshapanda ligi kuu wamekuwa wakisikika kuwa wataziunga mkono timu zao kama wafanyavyo watu wa Mbeya.
Mbeya city fc imejizolea umaarufu mkubwa na mashabiki lukuki, hivyo kuwa gumzo katika klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam fc.
Mpaka sasa City ipo nafasi ta tatu kwa pointi 45, huku ikiwa na miwili mkononi.
Kwa msimu wao wa kwanza, haya ni mafanikio makubwa sana na wakijipanga zaidi kwa kuanzia watakapofikia msimu huu basi wanaweza kuwa timu bora na yenye ushindani wa hali ya juu msimu ujao.
Imekuwa jambo safi kusikia watu wa Mtwara na Shinyanga wakiwa na mikakati ya kuzipiga chini Simba na Yanga na kurudisha uzalendo kwa timu zao za nyumbani.
Kwa hili Mbeya City fc lazima wapewe sifa zao kwasababu wamekuwa mfano kwa mikoa hii na kama kweli wataweza kufanya kama watu wa Mbeya, basi tutegemee timu nyingine bora kati ya Stand United na Ndanda fc ya Mtwara.
Watu wa Mtwara wamefika mbali zaidi kwa kuanzisha falsafa yao ya Ndanda fc `kwa roho safi`, wakimaanisha kila kitu ni timu yao, wengine pembeni.
Ni vizuri kuwaiga Mbeya City fc, lakini stand United, Ndanda fc na Polisi Morogoro wanatakiwa kuwa na mipango mizuri ili kufikia mafanikio ya Wagonga nyundo wa Mbeya.
Kwanza wahakikishe wanasajili vizuri kwa kutozingatia majina ya wachezaji.
Wakae chini kusaka vijana wadogo wenye vipaji na wenye umri mdogo ambao wanaweza kuwekwa pamoja na kufundishika kirahisi.
Waepukane na siasa katika mpira, wawaache walimu wao wafanye kazi yao na watengeneze mazingira mazuri kwa wachezaji wao kuanzia posho na mishahara.
Pia wakae na wachezaji wao kuwapandikiza `Sumu` ya kuwa wazalendo na timu yao.
Wajiandae kiuchumi ili waweza kusafiri na timu zao kwenda mikoani kama wafanyavyo watu wa Mbeya City.
Tayari timu tatu zimeshapatikana, swali la msingi ni, je, timu gani tatu zinashuka daraja kuzipisha timu hizi mpya?.
Mtandao huu unafanya uchambuzi wa kina ili kuona ni timu gani zinashuka daraja.
Kwanza tuangalie msimamo wa timu za mwisho kuanzia nafasi ya 9 katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara mpaka sasa.
Nafasi ya 14 mkiani, Rhino Rangers wameshapiga kambi yao baada ya kucheza mechi 24 na kujikusanyia pointi 16 tu.
Hata hivyo maafande wa Rhino wamebakiza mechi mbili ambazo wakishinda watafikisha pointi 22 pekee.
Nafasi ya 13 wapo JKT Oljoro wenye pointi 18 baada ya kucheza mechi 24, huku wakibakiwa na michezo miwili na kama watashinda yote watafikisha pointi 24.
Nafasi ya 12 wapo Ashanti United wenye pointi 22 baada ya kucheza mechi 24. Wauza mitumba hawa wa Ilala wamebakiza mechi mbili na kama watashinda zote watafikisha pointi 28.
Nafasi ya 11 wapo Tanzania Prisons wenye pointi 22 baada ya kushuka dimbani mara 24, na kama watashinda mechi mbili zilizosalia watafikisha pointi 28 kama Ashanti United.
Nafasi ya 10 wapo Mgambo JKT wenye pointi 25 baada ya kucheza mechi 24. Na kama watashinda mechi zao mbili zilizobaki wataweza kufikisga pointi 31.
JKT Ruvu wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 baada ya kucheza mechi 24. Na kama watashinda mechi zote mbili walizobakiza watafikisha pointi 34.
Ukipiga hesabu, kama timu zote za mwisho zitashinda mechi zao, msimamo utakuwa hivi;
JKT Ruvu watakuwa nafasi ya 9 kwa pointi 34. Lakini itategemeana na matokeo ya Mtibwa Sugar na Coastal Union kwani wataweza kuvuka pointi hizo kama wa watashinda mechi zao mbili za mwisho.
Coastal wapo nafasi ya na 8 kwa pointi 29 baada ya kucheza mechi 24, hivyo wakishinda michezo yake miwili watafikisha pointi 35.
Mtibwa wapo nafasi ya 7 kwa pointi 30 baada ya kucheza mechi 24. Na kama watashinda mechi mbili walizobakiza watafikisha pointi 36.
Na ndio maana nafasi ya JKT Ruvu inaweza kuwa ya 9 mpaka mwisho wa msimu au ikawa tofauti.
Nafasi ya 10 Mgambo watakaa kwa pointi 31, huku nafasi ya 11 na 12 zikikaliwa na Prisons, Ashanti watakaokuwa na pointi 28 kila mmoja, lakini utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa yataweza kuwatofautisha.
Nafasi ya 13 watakuwepo JKT Oljoro watakaokuwa na pointi 24, na Rhino Rangers wataburuza mkia kwa pointi 22.
Hivyo ndivyo msimamo wa ligi kwa timu za mwisho utakavyokuwa kama timu zote zitashinda mechi zao za mwisho.
Kwa maana hiyo, Rhino Rangers watakaokuwa na pointi 22, JKT Oljoro pointi 24 na mmoja kati ya Ashanti United na Prisons wataungana na timu hizi mbili kushuka daraja kwa kuangalia wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Rhino na Oljoro wana asilimia zote za kushuka daraja, lakini vita ya Ashanti na Prisons haipimiki kabisa. Huku Mgambo akionekana kuimarika zaidi.
Wakati tunatabiri matokeo hayo, lazima tufahamu timu hizi zimebakiwa na mechi za aina gani.
Rhino wamebakiza mechi dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine Mbeya na mchezo wa mwisho watacheza na Ruvu Shooting uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
JKT Oljoro wamebakiza mechi dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Shk. Amri Abeid jijini Arusha.
Ashanti wamebakiza mechi dhidi ya Simba sc uwanja wa Taifa pamoja na Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine Mbeya.
Prisons wamebakiza mechi dhidi ya Rhino na Ashanti uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mgambo JKT wataumana na Kagera Sugar Mkwakwani na mechi ya mwisho watacheza na Mbeya City sokoine jijini Mbeya.
JKT Ruvu wamebakiza mechi na coastal union Mkwakwani na mechi ya mwisho watacheza na Azam fc uwanja wa Azam Complex.
Ukizipima mechi hizi nje ya uwanja, utagundua kirahisi kuwa timu hizi hazina uwezo wa kushinda mechi zote zilizobaki kirahisi.
Kwasababu kuna baadhi ya mechi watacheza na timu zinazohitaji ubingwa kwa maana ya Yanga na Azam fc.
Pia nyingine kuna mechi dhidi ya Mbeya City wanaohitaji nafasi ya pili na tatu msimu huu.
Kwa maana hiyo mechi hizo zitakuwa ngumu zaidi kutokana na mazingira hayo ya Yanga, Azam fc na Mbeya City.
Tusubiri kuona nani atashuka daraja na nani atatwaa ubingwa.
Lakini kwa ndugu zangu Oljoro na Rhino, kama wameshatoa mkono wa `bai bai` vile.
Prisons na Ashanti wanachuana vikali. JKT Ruvu na Mgambo JKT angalau wanapumua kwa kiasi fulani.
Kwa ubingwa, Yanga na Azam fc ngoma bado nzito. Hawezi kutabiri kirahisi ingawa Azam fc wapo mbele kwa pointi 4 na wameshafungana michezo 23 na Yanga.
Kama Azam fc watashinda mechi mbili zilizobaki na kupoteza mechi moja, basi watawavua rasmi ubingwa Yanga kwasababu watafikisha pointi 59 ambazo Yanga hawataweza kufikia hata wakishinda mechi zote zilizosalia.
Kama Yanga watashinda mechi zote basi watafikisha pointi 58 ambazo zitapitwa na Azam fc.
Kibarua cha ubingwa kinaanza kesho kutwa ambapo Yanga watakuwa na Kagera Sugar uwanja wa Taifa , wakati Azam fc wakiwa na Ruvu Shooting Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment