Niyonzima amepona na yuko tayari kuanza kazi
Na Baraka Mpenja, Dar E salaam
HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba wachezaji
wake nyota Haruna Niyonzima `Fabregas`, David Luhende, Athuman Idd `Chuji`,
Emmanuel Anord Okwi wanatarajiwa kuungana na wenzao mara baada ya mchezo
uliopita dhidi ya JKT Ruvu.
Taarifa ya Yanga inasema kuwa wachezaji hao walikuwa
wagonjwa na sasa wanaendelea vizuri tayari kwa kuanza kazi ya kuitumikia klabu
hiyo.
Naye mlinzi wa kati, Kelvin Yondani aliyekuwa
akitumikia adhabu ya kadi 3 za njano amemaliza adhabu hiyo na atajiunga na
wenzake muda wowote kutoka sasa.
Mchezo uliopita ambao Yanga walishinda mabao 5-1
dhidi ya JKT ndani ya dimba la Taifa, huku Mrisho Ngasa akipiga `Hat Trick` ,
walikosa huduma za wachezaji hao.
Nafasi zao zilizibwa vizuri na wachezaji wengine
ambapo nafasi ya Yondani ilichukuliwa na Mbuyu Twite, huku Juma Abdul akicheza
nafasi ya beki wa kulia ambayo mara nyingi Twite hucheza.
Nafasi ya Niyonzima kwa mechi kadhaa sasa imekuwa
ikishikiliwa na kiungo kinda, Hassan Dilunga.
Uwepo wa Jeryson Tegete, Hussein Javu, Mrisho Ngasa,
Didier Kavumbagu ulionesha kuwa hata Okwi akikosekana safu ya ushambuliaji
hakuna tatizo katika kufumania nyavu.
Yanga kesho inashuka dimbani kucheza na wakata miwa
kutoka mjini Bukoba, Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara,
raundi ya 24 uwanja wa Taifa.
Kikosi cha kocha mholanzi Hans Van der Pluijm
kitaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 5 - 1
mwishoni mwa wiki dhidi ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa kutoka mkoani Pwani, JKT Ruvu na kufikisha
pointi 49 ikiwa ni pointi nne nyuma ya vinara Azam FC.
Baada ya mchezo wa
mwishoni mwa wiki dhidi ya JKT Ruvu, kikosi cha Yanga jana jioni kiliingia
kambini mjini Bagamoyo na kufanya mazoezi jana na leo asubuhi kwenye Uwanja wa
Boko Beach Veteran uliopo eneo la Boko.
Kocha mkuu wa klabu
hiyo, Mholanzi Hans Van Der Pluijm ameseme vijana wake 20 walioingia kambini
wote wapo kwenye hali nzuri, kiafya, kifikra na morali ya kusaka pointi 3
katika harakati zao za kutaka kutetea
ubingwa.
Katika mchezo wa awali uliozikutanisha Kagera Sugar
na Young Africans, uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, wafungaji wakiwa ni Mrisho Ngasa na Hamisi Kiza
`Diego`.
|
No comments:
Post a Comment