Na Baraka
Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
HAKUNA
uchawi katika mpira wa miguu zaidi ya maandalizi ya timu na soka ni mchezo
unaochezwa hadharani na matokoe hupatikana kutokana na ubora wa timu moja dhidi
ya timu nyingine.
Ubora
ninaousemea hapa ni kuwa na uwezo wa kutumia kila nafasi unayoipata ndani ya
uwanjani na kuibadili kuwa goli.
Kuna wakati
timu bora inaweza kupoteza mechi mbele
ya timu yenye udhaifu mkubwa katika kikosi chake.
Kuna maneno
mengi yanayoendelea kwa wadau wa soa kuwa zipo timu ambazo hucheza mechi mara
mbili, kwa maana ya nje ya uwanja na ndani ya uwanja.
Binafsi
imani yangu imejengwa katika soka la ndani ya uwanja. Hii michezo michafu ya
nje ya uwanja, naamini ni kuua soka la
nchi.
Mshindi wa
mechi lazima apatikane hadharani kwa kuonesha kiwango bora na mipango mizuri ya
uwanjani.
Makocha
wanafanya kazi muda mwingi kuwafua vijana wao. Huwa wanawapa mbinu mbalimbali
za kuwafunga wapinzani..
Kwa maana
hiyo, kama Simba wanajiandaa kucheza na Yanga, nao Yanga wanajiandaa kucheza na
Simba.
Kama Yanga
wanamuomba Mungu wawafunge Simba, nao wekundu wa Msimbazi wanamuomba Mungu
wawafunge Yanga.
Nasikia kuna
watu wanapiga dua za kusaidia timu zipate matokeo mazuri. Ni ngumu kujua hizo
dua zinaelekezwa kwa Mungu yupi, kwasababu kuna Mungu na Miungu.
Kama
wanapiga dua kwa miungu au waganga wa kienyeji, ni juu yao kwani hiyo ni
sayansi inayoaminiwa na baadhi ya watu, lakini huwezi kuiona kwa macho ya
kawaida.
Endapo mpira
ni uchawi na maombi, basi watu wanaosifika kwa uchawi na maombi wangekuwa na
timu nzuri kuliko zote duniani.
Kuna maeneo hapa
nchini yanasifiwa kwa uchawi, lakini hakuna soka hata kidogo na kuna timu za
kubabaisha tu.
Kwasababu
hiyo, nashindwa kuamini sayansi hii ya uchawi katika soka.
Lakini suala
la michezo michafu ya nje ya uwanja, kwa
maana ya kuhonga wachezaji, makocha na viongozi wa timu pinzani, naweza kuamini
kuwa kuna baadhi ya watu wanafanya biashara hiyo.
Imani yangu
inajengwa kulingana na mazingira ya soka letu kwasababu zipo changamoto nyingi
kuanzia uendeshaji wa ligi na klabu kwa ujumla.
Viongozi wa
soka si wepesi wa kufanya tafiti pale `figisu figisu` za rushwa zinaposemwa na
watu.
Nilishawahi
kuandika na kulaani vikali tabia ya kula hongo ili kupanga matokeo.
Sababu yangu
ilikuwa moja tu, ambayo ni kurudisha maendeleao ya soka letu kitaifa na
kimataifa.
Hakuna maana
ya kupeleka timu katika mashindano makubwa wakati ubingwa wake imeupata kwa
kuhonga timu pinzani.
Hapa katika
rushwa, wanahusishwa watu wengi sana,
hata waamuzi ni watuhumiwa wakubwa wa suala hili.
Lakini
nasisitiza kuwa suala la rushwa ni gumu kulijua katika hali ya kawaida
kwasababu huwa linafanyika kwa siri kubwa mno.
Labda
wahusika wenyewe wavujishe taarifa hizo, au wawepo watu makini wa kufuatilia
suala hilo.
Watu
wanawasiliana kwa mawasiliano yao binafsi na hawakutani ana kwa ana. Labda ugague
mawasiliano yao kwa kushirikisha mitandao wanayotumia ili uwabaini.
Ili
kuyafanya haya, lazima uwe umejipanga na kuwa na nia ya dhati.
Kwa
utaratibu wetu wa kupotezea mambo muhimu
kama haya, kila mtu anasikia na kuliacha kama lilivyo kwa kutumia maneno mepesi
kuwa ni uvumi tu.
Uvumi ni
msimgi wa kufuatilia ukweli. Unaposikia watu wanasema jambo fulani baya, kama
ni mtu mwenye dhamana jipange kufuatilia.
Nimesikitishwa
sana na taarifa ya Jana ya Mbeya City kwa vyombo vya habari ambayo ilikuwa
inahusu kukanusha kwa tuhuma nzito juu yao kwamba wamehongwa na Azam fc ili wafungwe mchezo wa jumapili na kuwapa
ubingwa wana Lambalamba hao.
Tuhuma hizi
zinahusu mambo makubwa matatu ambayo ni kuahidiwa kununuliwa basin a klabu na Azam
fc, kocha Juma Mwambusi kujengewa nyumba chamazi na wachezaji wa Mbeya City
kuhongwa pesa ili wacheze chini ya kiwango.
Kila mtu
anafahamu kuwa Mbeya City wameleta changamoto kubwa katika soka la Tanzania
kwasasa.
Mipango yao,
juhudi zao zimewafikisha hatua waliyopo sasa tofauti na timu nyingine
walizopanda nazo ligi kuu.
Ni moja ya
timu inayosifiwa kucheza kitimu na ukiwa uwanjani utagundua kirahisi kuwa timu
hii inacheza kwa kuhitaji kitu fulani.
Wachezaji ni
wapambanaji ndani ya dakika zote na yanapotokea matokeo mengine mabaya kwao ni
suala la kimpira.
Ukija upande
wa Azam fc ni dhahiri kuwa wamekuwa bora zaidi msimu huu kwasababu wamecheza
mechi 24 bila kufungwa.
Si kazi
nyepesi kufikia mafanikio hayo, lakini kwanini mechi na Mbeya City watuhumiwe
kucheza mchezo mchafu?.
Kama ndio
njia yao ya kupata matokeo, je, wamefanya hivyo kwa mechi zote 24 ambazo
hawajafungwa?.
Kwa akili ya
kawaida, si rahisi kuhonga katika mechi 24, bali ni mipango mizuri na
maandalizi yao.
Hivi soka la
Azam fc katika mechi hizo 24 ni baya?. Hapana!, wamecheza vizuri sana na kuwa
makini na nafasi wanazopata.
Kwa aina ya
wachezaji walionao, nadhani wanastahili kuwa hapo walipo na si haya
yanayosemwa.
Sikatai kama
hawawezi kufanya hivyo, lakini sidhani kama kuna mtu yeyote anayeweza kutoa
ushahidi wa moja kwa moja kama kweli Azam fc wanahonga.
Kama yupo
atufahamishe na wengine tusiojua jambo hilo na pengine inaweza ikawa msingi mzuri
wa kulitatua suala hili.
Ukifautilia
kwa makini maneno ya Mbeya City, utagundua kuwa wamejenga hoja zao kwa kusikia
maneno ya watu na mitandao ya kijamii.
Maneno
wasemayo watu si sababu ya kuamini kama jambo fulani lipo, cha msingi uyatumie
kutafuta ukweli hata kwa kutafiti kwa muda mfupi.
Mitandao ya
kijamii ndio chanzo kibovu zaidi kwasababu waliowengi wanaandika na kuchapisha
habari kwa wafikiriavyo bila kujali kama
kuna ukweli au la.
Hakuna
wahiriri mbali na mwenye mtandao au akaunti yake. Sasa unajengaje hoja yako kwa kusoma maneno ya facebook, Twita na mtandano
mingine?.
Lakini
usinielewe vibaya, ipo mitandao ambayo inafanya kazi nzuri ya kuwahabarisha
watu taarifa za ukweli.
Cha msingi ,
lazima uwe makini kuangalia kwa kina ili ujue ukweli wa taarifa na chanzo chake.
Kwa mtazamo
wangu, ni kweli mechi ya jumapili ni ngumu kwa timu zote mbili.
Azam fc
wanahitaji matokeo ambayo yanaweza kuamua ubingwa mwaka huu.
Wanaweza
kupata matokeo ya ushindi kama watakuwa na mipango mizuri ya uwanjani.
Wana
wachezaji ambao wanaweza kuwapata matokeo mazuri ndani ya dakika 90.
Watu kama
Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Agrey Moris, David Mwantika,
Michael Bolou, Himid Mao,Salum Abubakar `Sure Boy` Guadence Mwaikimba, John
Bocco, Kipre Tchetche na wengineo, wanashindwaje kuwapa matokeo bila hata
kuhonga?.
Nadhani wana
kikosi kizuri ambacho kinaweza kiifunga Mbeya City yenye watu muhimu kama Hassan
Mwasapili, Deogratius Julias, Yohana Moris, Steven Mazanda, Paul Nonga, Mwegane
Yeya na wengine wengi wanye vipaji vya juu.
Timu zote
mbili zina wachezaji wazuri, hivyo kila klabu inaweza kushinda mchezo huo ndani
ya uwanja.
Mbeya City
kushinda ni haki yao na Azam fc wana haki kama hiyo hata bila kuhonga.
Cha kuwashauri
Mbeya City, waachane na maneno ya mitaani kwani hayana msingi wowote.
Bila shaka
hata mtu aliyeanzisha propaganda hizo hawamjui pamoja na malengo yake.
Inawezekana
ni kutaka kuwatoa mchezoni ili waingie kwa
presha kubwa kuhofia kupoteza mechi.
Manake
wakifungwa watawafanya watu waamini kuwa kweli wamehongwa.
Ili kucheza mechi hiyo kwa ufanisi wanatakiwa
kuendelea na mambo yao.
Azam fc
wanaendelea na mambo yao ya maandalizi, nao Mbeya City waendelee na maandilizi
yao.
Waachane na
maneno haya yasiyo na kichwa wala miguu.
Lakini kama wana ushahidi wa hayo na mtu
aliyesema wafike katika vyombo husika.
Hakuna sheria
inayosema lazima Yanga, Simba lazima wachukue ubingwa. Na ndio maana timu kama
Coastal Union, Tukuyu Stars, Mtibwa Sugar ziliwahi kutwaa ubingwa mbele ya Simba
na Yanga.
Kwanini Azam
fc wasemwe kuwa wanahonga, kwani hawana
haki ya kuchukua ubingwa?.
Tupunguzeni
maneno yasiyokuwa na msingi katika soka.
Kila la
kheri Azam fc na Mbeya City katika mchezo wenu wa jumapili uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya.
wanaovumisha ni watu wa yanga wao wakishinda saba tano uwezo wakifungwa wamehujumiwa tubadilike
ReplyDelete