Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Mbeya City fc wamejawa na hofu kuelekea katika mchezo wa keshokutwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Nje kidogo ya jiji la Dar es salaam dhidi ya `Wauza Mitumba` wa Ilala, Ashanti United kutokana na mazingira ya wapinzania wao wanaotaka kukwepa kushuka daraja msimu huu.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi amesema kuwa kikosi walichokuja nacho hakina majeruhi hata mmoja na sasa wapo katika mikakati ya kutafuta ushindi.
“Tunajua kila mchezo uliobaki kwetu ni muhimu. Mazingira ya uwanja wa ugenini na mazingira ya timu tunayokutana nayo yanaifanya mechi hii iwe ngumu zaidi, lakini hatuwezi kukata tamaa, mapambano mpaka siku ya mwisho”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi aliongeza kuwa hawezi kuahidi kitu chochote kwa mashabiki wao, lakini anawaomba wazidi kuwaunga mkono ili waweze kufanya vizuri na kuangali mwisho wa ligi watakuwa nafasi gani.
“Ligi ya mwaka huu imekuwa na ushindani mkubwa, angalia timu ya Yanga tunayofuatana nayo tunapishana pointi moja, ingawa wana michezo mkononi. Azam fc yupo nafasi ya kwanza kwa pointi 53, kwakweli kumkimbiza kunahitaji juhudi kubwa sana”. Alifafanua Mwambusi.
Kocha huyo aliongeza kuwa matokeo kwasasa hayatabiriki kirahisi kwasababu timu zote zinafungwa bila kujali ukubwa na ukongwe wao.
“Inahitajika mikakati mingi ya uwanjani kama unahitaji kupata matokeo mazuri. Tunahakikisha tunafikia malengo yetu tuliyojiwekea kwani muda upo na mechi zipo”. Alieleza Mwambusi.
Naye kocha mkuu wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni `King Mputa` ameuambia mtandao huu kuwa wameweka kambi yao Bamba Beach kigamboni jijini Dar es salaam kwa lengo la kutuliza akili za wachezaji wao kuelekea michezo mitatu ya mwisho.
“Tumebakiwa na mechi tatu, tupo hapa Bamba Beach, eneo ni zuri na tulivu. Tunajiandaa kuhakikisha tunashinda mechi tatu zilizosalia ili kujinasua kwenye mstari wa kushuka daraja”. Alisema Kibadeni.
Kibadeni aliongeza kuwa yeye mwenyewe yuko makini pamoja na wachezaji wake kujiandaa na mchezo wa jumamosi dhidi ya Mbeya City.
“Mbeya City wanahitaji ubingwa. Kwa umoja walionao itakuwa ngumu kuwafunga. Lakini nasisi hatuna jinsi zaidi ya kupambana kusaka pointi tatu muhimu kama kweli tunataka kubakia ligi kuu”. Alisema Kibadeni.
Kocha huyo alifafanua kuwa mechi za mwishoni mwa ligi hazitabiriki kwasababu kila timu inajipanga kwa njia zake kutafuta ushindi.
“Tupo Bamba Beach kwa karibu wiki ya tatu. Viongozi wanatumia fedha zao kutugharamia. Lazima nasisi tujidhatiti uwanjani. Kikubwa mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono”. Alisema Kibadeni.
Mpaka sasa Ashanti United wapo nafasi ya 12 wakijikusanyia pointi 21 katika mechi 23 walizoshuka dimbani.
Juu yao wapo Mgambo JKT wenye pointi 22 baada ya kucheza mechi 23.
Wauza mitumba hao wa Ilala wapo katika hatari ya kushuka daraja kwasababu mpaka sasa wapo katika timu tatu za mwisho kwenye msimamo wa ligi kuu.
Timu nyingine mbili za mwishoni ni Rhino Rangers ya Tabora na JKT Oljoro ya Arusha.
Mechi zilizosalia kwa Ashanti ni dhidi ya Mbeya City jumamosi ya wiki hii uwanja wa Azam Complex.
Pia atakuwa na mchezo dhidi ya Simba sc aprili 13 Uwanja wa Taifa, huku kipute cha mwisho kikitaraji kupigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons.
Kibadeni atakutana na Mbeya City yenye uchu wa kutafuta ubingwa wake wa kwanza mwaka huu, kwasababu mpaka sasa wapo nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 45 baada ya kucheza mechi 23, pointi moja nyuma ya Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46.
Mbeya City watakuwa wanahitaji matokeo mazuri ili kuishikilia nafasi ya pili kwa muda, wakati wakisubiri matokeo ya jumapili baina ya Yanga na JKT Ruvu, uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment