Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam
0712461976
AKIWAANZISHA
washambuliaji wake watatu, Gaudence Mwaikimba, Kipre Herman Tchetche na John
Rapahel Raphael Bocco `Adebayor`, kocha wa Azam fc Mcameroon, Joseph Marius
Omog amefanikiwa kuongeza pointi tatu muhimu baada ya kuwafumua maafande wa
Ruvu Shooting mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara, kwenye
uwanja wa Mabatini , Mlandizi mkoani Pwani.
Lengo la Omog
lilikuwa ni kufunga mabao mengi katika mchezo huo ili kuendelea kujiweka
mazingira mazuri ya kuiongoza Azam fc kuandika historia mpya ya kutwaa ubingwa
wao wa kwanza tangu wapande ligi kuu mwaka 2008/2009.
Mipango yake ilianza
kuzaa matunda dakika ya 8 ya mcheza ambapo mshambuliaji wake ambaye mara nyingi
hukalia benchi, Gaudence Mwaikimba kufunga bao la kuongoza.
Azam fc walionekana
kuwa na uchu wa kupata mabao zaidi, na
katika dakika ya 37 kipindi cha kwanza, winga machachari, Himid Mau Mkami alitia
kambani bao la pili kufuatia krosi nzuri
iliyochongwa na beki wa kulia, Erasto Edward Nyoni.
Dakika 45 za kipindi
cha kwanza zilimalizika kwa Azam fc kuwa kifua mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili
kilipoanza, Azam fc walionekana kuendelea kuwepo mchezoni ambapo dakika ya kwanza tu,
Kipre Herman Tchetche aliandika bao la tatu na kuwanyanyua mashabiki
waliofurika uwanjani.
Kwa matokeo hayo Azam
fc wamezidi kujikita zaidi kileleni kwa kufikisha pointi 56, pointi nne mbele
ya mabingwa watetezi Yanga SC katika nafasi ya pili.
Yanga walikuwa
wanaufuatilia mchezo huo kwa makini ili
kujiridhisha kama wataweza kutetea ubingwa wao msimu huu.
Jana wanajangwani
hawa walishinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na kuwasogelea Azam fc
kileleni, lakini leo mambo yamezidi kuwa magumu zaidi kwao kutokana na matokeo
ya Mabatini.
Ili kutetea ubingwa wao,
Yanga wanahitaji kushinda mechi mbili walizobakiza dhidi ya JKT Oljoro na Simba
sc, wakati huo huo wakiiombea mabaya Azam fc ipoteze michezo yote miwili.
Wakati Yanga wakiwa
katika presha kubwa, Azam fc wao wanahitaji pointi tatu tu kuwavua ubingwa
Yanga.
Wakishinda mechi moja
kati ya mbili walizobakiza, wana Lambalamba watafikisha pointi 59 ambazo Yanga
hawataweza kufikisha hata kama watashinda mechi zote walizosaliwa nazo kwa
mabao 50.
Yanga wakishinda
mechi mbili zijazo watafikisha pointi 58 kibindoni ambazo Azam fc wataweza kuzivuka kama
watashinda mechi moja tu kati ya mbili walizonazo mkononi.
Mechi ijayo, Azam fc
watashuka dimbani dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Hii itakuwa mechi
muhimu sana kwa Azam fc, lakini watahitaji kutumia nguvu kubwa kuwafunga
wagonga nyundo hawa wa Mbeya kwasababu ya rekodi yao nzuri ya kutofungwa katika
uwanja huo.
Mbeya City mpaka sasa
wapo nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi
24.
City wameshapoteza
nafasi mbili za juu kwasababu wakishinda mechi mbili zilizobaki watafikisha
pointi 52 ambazo zimeshafikiwa na Yanga, huku wakiwa na michezo miwili mkononi.
Hata kama Yanga
watapoteza mechi mbili zijazo, kama Mbeya City watahitaji kuwa wa pili
watahitaji kushinda mechi mbili zilizobaki kwa ida kubwa mno ya mabao.
Ukiangalia wastani wa
mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga wametia kambani mabao mengi mno zaidi ya
Mbeya City. Hivyo bado nafasi ya pili kwao ni ngumu kuipata.
Hata hivyo kushika
nafasi ya tatu si haba kwao kwasababu ni msimu wao wa kwanza.
Wakati Azam fc
wakijiandaa kwenda Mbeya, tayari zipo tuhumu kwa wenyeji wao Mbeya City kuwa
wamehongwa na wana Lambalamba ili kucheza chini ya kiwango.
Madai ya kuuzwa kwa
mechi hiyo yamesambazwa kuhusu mambo matatu;
ambayo ni Timu ya Mbeya City kununuliwa basi na Klabu ya Azam, Kocha wao Juma Mwambusi amejengewa nyumba maeneo ya Chamazi, na wachezaji wao wamepewa fedha ili waweze kucheza chini ya kiwango dhidi ya Azam.
ambayo ni Timu ya Mbeya City kununuliwa basi na Klabu ya Azam, Kocha wao Juma Mwambusi amejengewa nyumba maeneo ya Chamazi, na wachezaji wao wamepewa fedha ili waweze kucheza chini ya kiwango dhidi ya Azam.
Hata hivyo uongozi wa
Mbeya City umekanusha tuhuma hizo na kusema watu wanaosambaza taarifa hizo
hawana malengo mazuri na klabu yao, zaidi wanawachafua kwa mashabiki wao.
Bingwa
atakayepatikana msimu huu atakuwa ni halali kutokana na ushindani mkubwa uliooneshwa
na timu za juu.
Azam fc, Yanga na
Mbeya City toka mwanzo wa mzunguko wa pili zimefukuziana mno na hatimaye sasa
Mbeya City wamejitoa na kuwaacha Yanga na Azam fc wakiendelea kuchuana.
Sasa Yanga na Azam fc
ni kutegeana tu, atakayepoteza mechi atamnufaisha mwenzake.
Lakini Yanga ndio
watumwa kwa Azam fc kwasababu wanahitaji kutetea ubingwa wao, wakati huo huo
wakihenyeka kutaka kusawazisha pengo la pointi nne dhidi ya Azam fc.
Ligi hiyo itaingia raundi ya 25 Aprili 12 na 13
mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani. Aprili 12 mwaka huu itakuwa
Mtibwa Sugar vs Ruvu Shooting (Manungu, Morogoro), Coastal Union vs JKT Ruvu
(Mkwakwani, Tanga), na Tanzania Prisons vs Rhino Rangers (Sokoine, Mbeya).
Aprili 13 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Kagera
Sugar (Mkwakwani, Tanga), Simba vs Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam), Mbeya City vs Azam (Sokoine, Mbeya) na Oljoro vs Yanga (Sheikh Kaluta
Amri Abeid, Arusha).
No comments:
Post a Comment