Ligi kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea leo machi 19 mwaka huu kwa mechi kali
ya vuta ni kuvute kati ya mabingwa watetezi, Young Africans dhidi ya makamu
bingwa Azam fc , itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30
jioni.
Shirikisho la soka Tanzania kupitia kwa Afisa habari
wake, Boniface Wambura Mgoyo limesema tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza
kuuzwa saa 2 asubuhi katika magari maalumu .
Vituo vilivyotajwa ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Ubungo
Terminal, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Samora/Ohio, OilCom Ubungo, Buguruni
Shell, Dar Live- Mbagala, kituo cha daladala Mwenge na Uwanja wa Taifa.
Wambura aliongeza kuwa baada ya saa 6 mchana mauzo yote yatahamia
Uwanja wa Taifa ambapo milango kwa ajili ya mechi itakuwa wazi kuanzia saa 7.30
mchana.
Pia afisa habari huyo alibainisha viingilio katika mechi hiyo kuwa ni sh.
30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati viti vya rangi ya chungwa,
bluu na kijani kiingilio ni sh. 7,000.
Wambura alimtaja mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam kuwa
ndiye atakayechezesha mechi hiyo, huku
akisaidiwa na Anold Bugado (Singida), Florentina Zablon (Dodoma) na Lulu
Mushi (Dar es Salaam).
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa ni Emmanuel Kavenga
kutoka Mbeya wakati mtathimini wa waamuzi ni Alfred Rwiza wa Mwanza.
Wakati mechi hiyo ikisubiriwa kwa hamu, kuna baadhi
ya mambo yanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tatu.
Siku za karibuni mashabiki wa klabu za Simba na
Yanga wamekuwa wakifanya vurugu ndani ya uwanja wa Taifa, huku wengine
waking`oa viti kuashiria kupinga baadhi ya mambo yakiwemo maamuzzi ya waamuzi.
Mashabiki wa timu hizi kubwa wamekuwa wakikosa
ustaraabu na uvumilivu pale timu zao zinaposhindwa kupata matokeo.
Pia maamuzi ya waamuzi yamekuwa chanzo cha vurugu
hizi ambapo mashabiki huwa wanawalaamu marefa kuvurunda.
Kuna wakati kweli waamuzi wanakosea kwa sababu za
kibinadamu, kwani hakuna aliyeumbwa
mkamilifu.
Linapokuja suala la baadhi yao kufanya maamuzi nje
ya sheria 17 za soka, hapo inakuwa ngumu kutafsiri kwanini inakuwa hivyo.
TFF wanatakiwa kuwakumbusha waamuzi kuwa mechi ya
kesho ina uzito mkubwa mno katika harakati za ubingwa wa Tanzania bara.
Yanga wanahitaji kushinda ili kupunguza pengo la
pointi baina yao na vinara Azam fc.
Mpaka sasa Yanga wao nafasi ya pili kwa pointi 39
nyuma ya Azam waliopo kileleni kwa pointi 43.
Kama Azam fc atashinda kesho inawezekana ikawa mguu
ndani- nje kutafuta ubingwa wake wa kwanza tangu kuingia ligi kuu msimu wa
2008/2009.
Kwa upande wa Yanga kushinda kutawafanya warudi
katika hadhi yao ya kutetea ubingwa msimu huu.
Kama watapoteza, watakuwa katika mazingira magumu
kuwachomoa Azam fc waliopo kwenye reli kwasasa.
Kwa mazingira hayo, mchezo wa kesho una uzito mkubwa
mno kwa wachezaji wa Yanga, Azam fc, viongozi na mabenchi ya ufundi na
mashabiki kwa ujumla.
Mashabiki wa Yanga wanahitaji kuona timu yao
inashinda, nao wa Azam fc wanahitaji kuona wanaendelea kutesa kileleni.
Kiuhalisia Yanga wana mashabiki wengi zaidi kuliko
Azam fc, lakini kuna kundi la wapinzani linaweza kuingia uwanjani kwa
kuwashangilia wana Lambalamba.
Kutokana na uzito wa mchezo huu, waamuzi wanalo jukumu
kubwa la kuhakikisha amani inatawala uwanjani na nje ya uwanja.
Machi 10, mwaka 2012, Israel Mujuni Nkongo alipigwa
na wachezaji wa Yanga kwa sababu ya kutoridhishwa na maamuzi yake.
Nao mashabiki walifanya vurugu uwanjani kuashiria
kuunga mkono maamuzi ya wachezaji wako
kumshambulia Nkongo.
Kwa haya yaliyowahi kutokeo nyuma, ndio maana
waamuzi wanaaswa kulinda sheria 17 za mchezo wa soka ili kutowaamusha mashabiki majukwaani kufanya
vurugu.
Vurugu pia zimewahi kushuhudiwa katika mechi ya
Coastal Union dhidi ya Yanga uwanja wa Taifa, pamoja na ile ya Simba dhidi ya
Kagera Sugar.
Viti vingi viliharibiwa na kuitia hasara serikali, hivyo kuilazimu
kuchota kodi za wananchi kufanya matengenezo.
Machi mosi mwaka huu, pia sinema ya vurugu
iliendelea baada ya mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba kufanya vurugu dhidi ya
mashabiki wa Yanga ambao walilazimika kukaa jukwaa moja wakati wa mechi ya ligi
ya mabingwa barani Afrika dhidi ya National Al Ahly ya Misri kwasababu sheria
za CAF zinawataka wenyeji kukaa kushoto na wageni kulia mwa uwanja.
Kwa sheria hiyo, Yanga walitakiwa kuondoka kulia mwa
uwanja wa Taifa na kwenda kushoto ambako ni ngome ya mashabiki wa Simba siku zote. Hapo ndipo zengwe likaibuka.
Kimsingi vurugu hizi hazikuchangiwa na mpira wa
uwanjani, bali ni uhasama usiokuwa na miguu wala kichwa baina ya Simba na
Yanga.
Viti vingi vilinyofolewa, na machi 10 mwaka huu Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) lililaani vikali fujo na uhabirifu wa mali unaofanywa
na washabiki viwanjani wakati mechi mbalimbali zikiwemo zile za kimataifa na
ligi za hapa nchini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, TFF waliiomba radhi Serikali kwa uharibifu wa viti uliotokea kwenye
mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga ya Tanzania na Al Ahly ya Misri .
Kwa mujibu wa TFF, uharibifu ule wa viti ulisababisha hasara ya sh. milioni 15
kwa wamiliki wa uwanja huo ambao ni Serikali.
TFF walisema watalipa fedha hizo kwa
Serikali kutokana na uharibifu huo.
Kwa mujibu wa Serikali, katika mechi
hiyo, viti kumi viling’olewa na kutupwa ovyo ovyo uwanjani wakati vingine 40
viliathirika kutokana na vurugu za watazamaji hao.
Aidha, TFF walikazia zaidi kwa kusema, kwa
vile sasa baadhi ya washabiki, wapenzi na wanachama wa klabu mbalimbali nchini
wanataka kufanya suala la uharibifu kuwa la kawaida na mazoea, Serikali
inakusudia kuchukua mapato yote ya mchezo husika endapo kutatokea uharibifu.
Taarifa hii ya TFF ilionesha jinsi gani wameguswa na
suala la uharibifu wa viti uwanja wa Taifa.
Si kwamba mashabiki wote wanafanya vurugu hizo, bali
kuna kundi fulani la mashabiki wanaokosa uunngwana na kuwashawishi wenzao
kufanya uovu huo.
Tayari mtihani mwingine upo kesho, kama mambo
hayataangaliwa kwa umakini tunaweza kuona mambo mabaya.
Hatuombei, lakini hatuachi kutoa tahadhari kwa TFF
kuwa hatua za mapema zichukuliwe kutokana na uzito wa mchezo wenyewe.
Kama mashabiki kwa asilimia zote wamejiandaa kupata
ushindi na kusahau kuwa mpira wa miguu una matokeo matatu, kushinda, kufungwa
na kutoa sare au suluhu, basi tunaweza kuona vurugu endapo matokeo yatakuwa
tofauti na matarajio yao.
TFF wawasiliane na jeshi la polisi mapema ili kupanga mikakati ya kudhibiti hali ya mambo uwanjani.
Walishatangaza kuwachukulia hatua kali mashabiki wanaofanya
vurugu kwani tayari wameshaingia hasara ya milioni 15.
Pesa hizi zingetumika kufanya mambo mengine, lakini
kwasababu ya upuuzi wa baadhi ya watu, zinafidia uharibifu wa viti.
Hatua kali zianzie kesho endapo kutatokea
sintofahamu. Japokuwa hatuna imani kama vurugu zitatokea.
Mashabiki wa Yanga na Azam watambue kuwa soka ni
mpira wa ajabu ambao hutegemea zaidi umakini uwanjani.
Ni mchezo wa nafasi, endapo ukipata nafasi na
kuitumia unafaidika, lakini kama unapata nafasi na kuichezea, unajutia.
Mashabiki wafahamu kuwa kufungwa kupo na lazima
ukubali matokeo.
Pia wakumbuke waamuzi ni binadamu, kama kuna makosa watafanya,
viongozi wanajua taratibu za kufuata ili kupata haki.
Kupigana, kuvunja viti hakusaidii kitu zaidi ya
kuilipisha klabu faini zisizokuwa na kichwa wala miguu.
TFF msikubali kulipa milioni 15 kwasababu ya
wachache. Kamwe msione kama fedha hizo ni chache. Wachukulieni hatua kali
watakaohusika kwa uharibifu kama mlivyotangaza.
Mshabiki nendeni uwanjani mkashangilie mpira kwa
amani bila kujihusisha na utovu wa nidhamu.
Wachezaji chezeni mpira bila kutegemea maamuzi ya
waamuzi. Unesheni ufundi wenu na kuwakosha watazamaji watakaofurika kesho
uwanja wa Taifa.
Kila la kheri Yanga na Azam fc kuelekea ngwe muhimu
ya kesho.
No comments:
Post a Comment