Wapo
mashabiki wengi ambao kila muda wanajadili soka. Hata hapa Tanzania, ukipita
kwenye vijiwe mbalimbali, baa, ofisi za watu na maeneo mengi ambayo watu
wanakutana kupiga gumzo, hawaachi kuzungumzia kabumbu.
Nchini
Tanzania, klabu za Simba na Yanga zina wapenzi wengi zaidi ya klabu yoyote.
Unapotaja klabu hizi, unagusa hisia za Watanzania wengi.
Ndio
maana kwenye mechi zao, ni rahisi kwa watu kuzirai au kupoteza fahamu pale
matokeo mabaya yanapoikumba timu moja.
Kama
inafika wakati watu wanapoteza fahamu baada ya timu zao kufungwa na wengine
kuamua kujiua, utagundua kuwa timu hizi zina mvuto mkubwa kwa mashabiki wake.
Kama
mtu anaweza kukumbwa na matatizo hayo ya kiafya kwasababu timu imefungwa, lazima
uwe makini unapopewa dhamana ya kuogoza klabu hizi.
Kuwa
kiongozi wa Simba na Yanga, kunahitaji uwe na uelewe mkubwa wa kutambua kuwa nyuma yako kuna watu wengi wenye
mapenzi ya dhati na timu zao.
Unapoleta
mchezo na mambo muhimu yanayohusu klabu, unawaumiza watu bila sababu ya msingi.
Nirudi
kwenye hoja yangu ya msingi iliyonisukuma kuandika makala hii.
Kesho
machi 16 klabu ya Simba itafanya
mkutano wa wanachama wake kwa ajili ya kuifanyia marekebisho Katiba yao.
Kuelekea katika mkutano huo, tayari shirikisho la soka la
Tanzania, TFF limewatakia kila la heri Simba katika mkutano huo ambao ni muhimu
katika kuhakikisha klabu yao inapiga hatua katika maendeleo ya mpira wa miguu
na ustawi wake kwa ujumla.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi katika taarifa yake jana
aliwakumbusha
viongozi na wanachama wa klabu ya Simba kuwa marekebisho hayo ni lazima
yafanyike kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF) na Tanzania (TFF).
Aidha taarifa yake ilisema kuwa waraka wa TFF kwa
wanachama wake wa Februari 7 mwaka huu uzingatiwe kikamilifu katika marekebisho
hayo.
Zaidi Malinzi aliwakumbusha wanachama wa Simba kuzingatia umuhimu wa kudumisha amani na maelewano katika
klabu yao.
Mkutano wa kesho kwa mujibu wa mwenyekiti wa Simba SC,
Ismail Aden Rage utakuwa na ajenda moja
ya marekebisho ya katiba.
Lakini tayari yametokea malumbano ambapo wiki hii viongozi wa matawi ya Simba, walipinga maamuzi ya
Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu wa dharura Jumapili
ukiwa na ajenda moja tu badala yake wametaka kuwe na ajenda tano.
Viongozi hao walikutana na waandishi wa habari katika ukumbi
wa Idara ya habari (MAELEZO) na kumtaka Rage na kamati yake ya utendaji waongeze
ajenda nyingine ili mkutano huo uwe na ajenda tano.
Walisema wanataka kujua uwanja wao wa kisasa unajengwa lini, mauzo ya jezi, kesi
zilizopo mahakamani dhidi ya Simba, pesa
za mauzo ya wachezaji wao na uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti baada ya kujiuluzu
kwa Geofrey Nyange.
Mwanachama machachari wa Simba Bi. Chuma Suleiman alienda
mbali na kueleza kuwa pasipo kuyafanya hayo, wanaamini kutakuwa na vurugu
katika mkutano huo.
Ukifuatalia suala hili, utagundua kuwa Wanachama wana mengi
moyoni mwao ambayo wanataka yajadiliwe katika mkutano huo na kujua hatima ya
klabu yao.
Rage akiwa mwenyekiti anayo mamlaka kikatiba ya kupanga
ajenda za mkutano mkuu wa wanachama.
Kwasababu katiba inamruhusu, basi hakuna jinsi ya kumpinga
kama ameamua kuwepo kwa ajenda moja tu katika mkutano.
Katika maisha ya kawaida, kuna wakati unatakiwa kuwa makini
unapofanya maamuzi. Sipingi hata kidogo kwa Rage kuwa na ajenda moja ya
mabadiliko ya katiba.
Lakini ukitazama kiuhalisia, bado utagundua kuwa Simba
wanayo matatizo mengi ya kujadili katika mkutano huo.
Wanachama wanazo ajenda za kuhoji kwa viongozi wao. Wanataka
kujua mambo mengi, hivyo wanaamini mkutano huo ndio wenye nguvu kufanya
maamuzi.
Nadhani ipo haja kwa kamati ya utendaji chini ya Rage
kufikiria upya na kuyaingiza maombi ya wanachama wake.
Mwanzoni mwa makala hii nilisema, kuongoza Simba au Yanga
unagusa hisia za watu wengi, hivyo lazima uwe msikivu.
Rage inabidi akae chini na kutathimini, kama atagundua
wayatakayo wanachama ni kwa ajili ya faida ya timu, basi ayaweke katika mkutano huo. Lakini kama
anaona hayana maana kujadiliwa kwasasa basi aendelee na ajenda moja tu.
Wanachama ndio waliomuweka madarakani. Wao ndio wenye klabu,
wanapohitaji jambo fulani lijadiliwe basi wafikiriwe.
Siandiki haya kwa kujaribu kumshinikiza Rage aongeza ajenda,
lakini najaribu kuwaza endapo kutatokeoa vurugu kwenye mkutanao huo kwasababu
tu ajenda za wanachama zimekataliwa kujadiliwa, nani atabeba msalaba wa lawama?.
Bado nasisitiza jambo hili, kuongoza Simba na Yanga unagusa
maisha ya watanzania wengi. Hakuna tatizo lisilokuwa na chanzo.
Hata kufanya vibaya kwa timu kunachangiwa na viongozi.
Jaribu kuwaza mfumo unaotumika kusajili wachezaji kama unaridhisha katika klabu
hizi kubwa.
Watu wachache wanakaa chini na kutafuta wachezaji, na wakati
mwingine wanasahau hata kupitia ripoti za mabenchi ya ufundi.
Kupigana vikumbo kwa viongozi, kunyang`anyana wachezaji ndio
tabia yao. Lakini wanapogundua kuwa walisajili vibaya na benchi la ufundi
limeshindwa kuwapa makali `magalasa` wao, basi makocha wanabebeshwa mzigo wa
lawama.
Mwisho wa siku timu inacheza vibaya na kuwajeruhi mashabiki
moyoni. Watu wanazirai uwanjani kwasababu ya makosa yaliyofanywa na watu fulani.
Hakika baadhi ya viongozi hawawezi kukwepa lawama kwa haya,
ifike wakati wawe na moyo wa huruma kwa mashabiki wao. Wachezaji hawalipwi
mishahara na posho kwa wakati. Unategemea wacheze mpira gani kama wana njaa.
Lakini kuna watu wanaohusika na kukwepa majukumu yao.
Nawaasa viongozi wa Simba wawape nafasi wanachama wao
kujadili mambo ya klabu. Nafahamu kuwa uhuru wa kutoa mawazo hauzuiliwi hata
kikatiba. Katiba inatoa nafasi kwa kila mtu kutoa mawazo yake.
Wape watu nafasi ya kuzungumza, pima uzito wa hoja zao,
chukua mazuri achana na pumba.
Kikubwa kwa Rage ni kutumia busara ya utu uzima ili kuepuka
mgogoro usiokuwa wa lazima.
Katika utawala wa kidemokrasia, watu wana nafasi kubwa ya
kujadili mambo yao, usijaribu kuwanyima fursa.
Migorogoro haina tija kwa klabu. Watu wamechoka kusikia
migogoro. Wachezaji wanaathiriwa nayo hata kama si moja kwa moja.
Viongozi mnapolumbana na wanachama kwa masuala fulani,
mnatoa mwanya kwa wapinzani wenu kuwapiga bao.
Kila la heri wana Simba katika mkutanao wenu hapo kesho.
Tafuteni mwarobaini wa matatizo yenu.
Na
Baraka Mpenja , Dar es
salaam
0712461976
No comments:
Post a Comment