Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
INAWEZEKANA baada ya dakika 90 za mtanange wa kesho
baina ya Young Africans dhidi ya Azam fc, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es
salaam, picha ya timu gani inaweza
kupewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa
2013/2014 ikafahamika.
Mchezo wa kesho umevuta hisia za mashabiki wengi na
kuwafanya makocha wa timu zote, Joseph Marius Omog wa Azam fc na Hans Van Der
Pluijm wa Yanga kutuliza akili zao kwa lengo la kupata ushindi mechi ya kesho.
Kitendawili kinachosubiriwa kuteguliwa ni je, Azam
fc watawafunga Yanga kwa mara ya pili msimu huu katika mechi za ligi kuu?.
Ikumbukwe septemba 22 mwaka jana, timu hizi
zilikutana katika mchezo wa ligi kuu na Wana Lambalamba kuibuka na ushindi wa
mabao 3-2.
Lakini kabla ya mechi hiyo, Yanga waliwafunga bao
1-0 Azam fc katika mchezo wa Ngao ya jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la
ligi kuu soka Tanzania bara msimu 2013/2014.
Mechi zilizopita, Yanga walitoka suluhu dhidi ya
Mtibwa uwanja wa Jamhuri, wakati Azam fc walishinda mabao 4-0 dhidi ya Coastal
Union.
Azam fc wapo kileleni wakijikusanyia pointi 43
katika mechi 19 walizocheza, wakati Yanga wameshuka dimbani mara 18 na
kujikusanyia mzigo wa pointi 39 katika nafasi ya pili.
Mtandao huu ulipata nafasi ya kuzungumza na kocha wa
zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula `Mzazi` , lengo likiwa ni kujua mtazamo
wake kuelekea mechi ya kesho.
Katika mahojiano hayo maalumu, Mwaisabula alianza
kwa kusema mchezo wa kesho utakuwa mgumu
kwa Yanga, kwasababu wameathiriwa na matokeo ya mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa
Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
“ Kutoka suluhu na Mtibwa kutawafanya wacheze kwa
nguvu kutafuta matokeo ya ushindi. Hawatakubali kufungwa au kutoka sare kwani
wakipata matokeo hayo, kutawafanya wapunguze hadhi yao ya kutetea ubingwa wao”.
“Lakini Azam fc wapo kwenye reli, wapo kwenye mwendo
mzuri. Wanashinda mechi zao, wanaonekana kuiandaa timu yao vizuri. Ukizingatia haya utaona kuwa
mechi ya kesho itakuwa na upinzani mkubwa”. Alisema Mwaisabula maarufu kwa jina
la `Mzazi`.
Mwaisabula aliendelea kusema kuwa Azam fc wamewekeza
sana kwenye timu yao, hivyo hakuna wanachohitaji msimu huu zaidi ya ubingwa.
“Azam wamechukua nafasi ya pili zaidi ya misimu
miwili, mwaka huu hakuna wanachokitafuta zaidi ya Ubingwa. Naamini kesho kila
timu itacheza kwa malengo ya kutafuta pointi tatu muhimu”. Aliongeza Mwaisabula.
Aidha, Mwaisabula alisema kwa namna timu hizi mbili
zilivyosheheni nyota wenye gharama kubwa hategemei mizengwe ya nje ya uwanja.
“Kinachotakiwa ni mpira kuchezwa uwanjani, mambo ya
nje ya uwanja, nadhani yasiwe na nafasi kwa sasa. Timu zimesajili kwa
gharama kubwa, hakuna maana ya kumwaga fedha kwenye timu, halafu unafanya
mizengwe nje ya uwanja. Binafsi sikuelewi kabisa”. Alisema.
Naye beki wa zamani wa Simba, Moro United na APR ya Rwanda,
Boniface Pawasa alisema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa timu zote kwasababu
itaweza kutoa nafasi ya timu yoyote kujikita kutafuta ubingwa ua kutoka katika
mbio za ubingwa.
“Kisaikolojia, Yanga unaweza kusema wameathirika
kidogo na kupoteza mechi dhidi ya Al Alhy katika mazingira ambayo walikuwa
wanaamini kuwa wanaweza kusonga mbele. Pia hawajashinda mechi iliyopita. Sisi
wataalam wa mpira tunaamni mwisho wa mechi moja ni mwanzo wa mechi nyingine.
Wajipange kwa lkesho”. Alisema Pawasa.
Aidha, Pawasa alishauri upande wa tatu wa mchezo kwa
maana ya waamuzi kuwa makini zaidi katika mechi hiyo muhimu kwa timu zote.
“Waamuzi lazima wachezeshe kwa kufuata sheria 17. Mechi za mwishoni huwa
waamuzi wanabeba lawama nzito, cha msingi wawe makini katika maamuzi kwasababu
ni mechi kubwa itakayoamua hatima ya timu zote”. Alisema Pawasa.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa machi 10, mwaka 2012
wakati Yanga ikilala 3-1 dhidi ya Azam fc, Uwanja wa Taifa, wachezaji wa Yanga
walimpiga mwamuzi wa kati Israel Mujuni Nkongo baada ya kutoridhishwa na
maamuzi.
Mbali na kupigwa kwa mwamuzi, pia mashabiki wa
Yanga walifanya fujo na kuvunja viti
mpaka ikawalazimu polisi kutumia nguvu kutuliza ghasia hizo.
Kutokana na hali hii kutokea, ndio maana Pawasa
aliwataka waamuzi kuwa makini zaidi katika mchezo wa kesho.
Historia inaonesha kuwa klabu hizi mbili zimekutana
mara 12 katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara tangu wana Lambalamba
wapande daraja msimu wa 2008/2009 ambapo Yanga imeshinda mara nyingi.
Mechi 11 zilizopita za ligi kuu, Wanajangwani
wameibuka na ushindi katika mechi tano, wakati Azam fc wao wameshinda mechi nne, huku
timu hizo zikichoshana nguvu katika mechi mbili.
Kwa matokeo haya ya mechi zilizopita, unaweza kuwapa
Yanga nafasi ya kushinda, lakini kwenye soka kuna wakati historia haileti
matokeo.
Kwasasa vikosi vyote viko imara, huku vikiwa na
makocha wenye historia Tofauti.
Mabeki wa Azam fc ambao kwa asilimia kubwa wanategemewa
kuwa Erasto Nyoni, Said Moradi, Gadiel Michael na Aggrey Morris watakuwa na mtihani mwingine wa kuwazuia washambuliaji
wa Yanga ambao wanaweza kuwa Emmanuel Okwi, Khamis Kiiza, Didier Kavumbagu, na Simon
Msuva.
Kama Mrisho Ngassa yuko fiti na tayari kwa kuanza
kesho, basi ni hatari nyingine kwa upande wa Azam fc.
Wakati
mabeki wa Azam fc wakipeana shughuli na washambuliaji
hao wa Yanga, nao Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Nadir Haroub Canavaro,
Oscar
Joshua watakuwa majaribuni kuwazuia wakali wa wana Lambalamba, John
Raphael Bocco `Adebayor`, Kipre Herman Tchetche, Brian Umony, na kiungo
mshambuliaji Himid Mao.
Langoni mwa Azam fc atakuwepo Mwadini Ali wakati
Yanga anaweza kuanza Juma Kaseja kufuatia kipa namba moja, Deogratisu Munish
`Dida` kuwa majeruhi.
Kwa ubora wa makipa hawa, milango ya timu zote
itaweza kuwa katika mikono salama.
Vita nyingine kesho ni baina ya Haruna Niyonzima
`Fabregas`, Frank Domayo (kuingo wa ulinzi) dhidi ya viungo wa Azam fc, Michael
Balou na fundi, Abubakar Salum `Sure Boy`.
Hapa ufundi wa hali ya juu unategemewa kutoka kwa
wapishi hawa wa dimba la kati kwa timu zote.
No comments:
Post a Comment