Search This Blog

Thursday, March 13, 2014

NIONAVYO MIMI: MOURINHO NI KOCHA WA SAYARI NYINGINE.


Na Oscar Oscar Jr
 
0789-784858 

Kuna watu wengi sana katika medeni ya soka wanaamini kuwa kocha wa sasa wa Chelsea Jose Mourinho,alishindwa kupata mafanikio akiwa na timu ya Real Madrid huko nchini Hispania ambako ameinoa timu hiyo kwa misimu mitatu. Hii imetokana na pengine kocha huyo kushindwa kuwapatia klabu ya Real Madrid ubingwa wa 10 wa klabu bingwa Ulaya ambapo mpaka sasa timu hiyo inashikilia rekodi ya kutwaa taji hilo mara 9, kushindwa kuvunja ubabe wa Barcelona nchini Hispania na mvurugano baina ya kocha huyo na watawala, wachezaji wake kama nahodha Iker Cassilas, beki mreno mwenzie Pepe na Sergio Ramos kwa nyakati tofauti ni kati ya sababu ambazo watu wengi wanazitumia kumkosea heshima kocha Jose Mourinho! 

Ni kweli hayo yote yalitokea lakini, unamjua Mourinho au unamsikia? Jose Mourinho ni mshindi wa Ballon D'or kama kocha bora wa dunia mwaka 2010, ametwaa taji la ligi kuu katika nchi 4 tofauti, alifanya hivyo akiwa na timu za Fc Porto ya nchini Ureno, Chelsea ya Uingereza, Inter Millan ya Italia na Real Madrid ya huko Hispania. Mourinho ni miongoni mwa makocha wanne waliowahi kutwaa kombe la klabu bingwa Ulaya wakiwa na klabu mbili tofauti, alifanya hivyo akiwa na klabu ya Porto ya huko Ureno na Inter Millan ya Italia. Unapoamua kumbeza Jose Mourinho, hakikisha umefikiria mara mbili au mara tatu. 

Msimu wa 2010/2011 wakati Jose Mourinho anaanza kazi pale kwenye dimba la Estadio Santiago Bernabeu kuinoa timu ya Real Madrid, nchi ya Hispania ilikuwa imetoka kutwaa kombe la dunia kule nchini Afrika ya kusini na chachu ya mafanikio hayo ni wachezaji wa kutoka klabu ya Fc Barcelona. Ni muda ambao Barcelona ilikuwa haikamatiki, Xaiv Hernandez, Andres Iniesta, Pedro Rodriguez, Sergio Busquets na Lionel Messi walikuwa kwenye kilele cha ubora wao. 

Barcelona ilikuwa ni timu ambayo kwa lugha rahisi,utasema ilikuwa imeshindikana duniani. Kocha wa Zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson alikutana na Barcelona hiyo iliyoshindikana kwenye fainali ya klabu bingwa ulaya mara mbili mwaka 2009 na 2011 lakini hakufua dafu, na kibaya zaidi mzee huyo mwaka 2011, alijikuta akitetemeka mikono huku akiwa haamini kile anachokiona kwa watoto hao wa Katalunia. Arsenal na mzee wao Arsene Wenger,walikutana mara mbili kwenye robo fainali ya UCL na timu hiyo iliyoshindikana, waliteketezwa kama mkate kwenye chai! 

Pamoja na ubora wote ule wa Barcelona,Jose Mourinho katika misimu yake mitatu pale Bernabeu,alifanikiwa kutwaa Kombe la Mfalme kwenye msimu wake wa kwanza tu taji ambalo Real Madrid walilikosa kwa miaka 18, Mourinho msimu wake wa pili aliweza kutwaa taji la La Liga mbele ya Barcelona. Wakati dunia ikiogopa kupangwa na Barcelona hasa kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya, Mourinho alikuwa anakutana na Barcelona ile hatari mara 4 hadi mara 6 kwa msimu mmoja! 

Tangu mwaka 2003, Real Madrid ilikuwa haijawahi kutinga hatua ya nusu fainali za klabu bingwa Ulaya lakini ndani ya misimu mitatu ya Mourinho,wamecheza mfululizo nusu fainali hizo. Utakumbuka msimu wa 2010/2011 walifika nusu fainali na kutolewa na Barcelona ambao walienda kutwaa taji hilo,2011/2012 walifika na kutolewa na Bayern Munich na 2012/2013 walitolewa na Borrusia Dortmund. Ulitaka Jose Mourinho afanye nini zaidi? 

Mourinho amerejea msimu huu kuinoa kwa mara nyingine tena klabu ya Chelsea. Mmiliki wa klabu hiyo Roman Abromovic kwa nyakati tofauti,amekuwa akibadili malengo yake. Abromovic wakati ameinunua klabu ya Chelsea,lengo lake ilikuwa ni kuifanya timu hiyo kutamba kwenye ligi kuu ya Uingereza na Kocha Jose Mourinho aliifanya kazi hiyo kwa kuwapatia Ubingwa wa EPL mara mbili mfululizo mwaka 2005/2006 na 2006/2007. Unamjua Mourinho au Unamsikia? 

Baada ya Mourinho kuondoka,Abromovic alitaka timu yake ipate mafanikio ya Ulaya na kupitia kwa kocha Roberto Dimateo na Rafael Benitez kwa nyakati tofauti,waliweza kutimiza ndoto za Bosi huyo toka Urusi kwa kutwaa kombe la klabu bingwa Ulaya na lile la Europa. Pamoja na hayo yote, Abramovic hakuridhika na sasa akasema anataka timu icheze kama Barcelona na hapo ndipo ujio wa Mata, Hazard na Oscar ulipolenga kutimiza matakwa ya bosi huyo. 

Ujio mpya wa Jose Mourinho kwenye EPL akiwa na Chelsea,ulianza huku akiwa anatamani kuifanya chelsea icheze kama Abromovic anavyotaka lakini, ilishindikana baada ya Mourinho kujikuta akipata sare nyingi na vipigo kutokana na aina hiyo ya uchezaji. Baada ya kupata ushindi wa mabao 4-3 pale Stadium of Light dhidi ya Sunderland na kupokea kichapo cha mabao 3-2 pale kwenye dimba la Britania dhidi ya Stoke City, Mourinho aliamua kubadilika na kuachana kabisa na ule mfumo wa burudani na kurudi kwenye mbinu yake ya kulinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza ambayo imempa mafanikio duniani. 

Msimu huu Mourinho ndiye kocha pekee aliyeweza kuifunga timu ya manchester city nyumbani na ugenini kwenye ligi kuu ya Uingereza na tangu mwaka 2014 uanze, hajapoteza mchezo wowote wa ligi huku dunia ikishuhudia kila mwezi mchezaji mmoja wa Chelsea akifunga ''Hat-Trick", alifunga Samwel Et'oo dhidi ya Manchester united mwezi Januari, akaja Eden Hazard akufunga dhidi ya Newcastle United mwezi Februari na huu ni mwezi machi huku Mjerumani Andre Schullre akifanya hivyo dhidi ya Fulham. Unamjua Mourinho au Unamsikia? 

Jose Mourinho anajua namna ya kwenda na wakati uwanjani na namna ya kufanya mabadiliko ya kiufundi wakati mchezo unaendelea. Msimu uliopita aliwaondoa Man United kwenye michuano ya UCL na katika mechi hiyo, dunia ilishuhudia mabadiliko ya wachezaji uwanjani yenye tija.Wakati Mourinho anajiandaa kumuingiza Karim Benzema, winga wa man united Luiz Nani alipewa kadi nyekundu, Mourinho naye fasta akabadilika na kumtoa beki Alvaro Abeloa ambaye alikuwa anamkaba Luiz Nani na Kumuingiza Luke Modric badala ya Benzema. Baada ya dakika "sifuri' Man United waliangamizwa na goli la kusawazisha la  Modric kabla ya Christiano Ronaldo, kumalizia bao la pili na kupigilia kabisa msumari. Hivi unamjua Mourinho au Unamsikia? 

Jose Mourinho anajua pia namna ya kucheza na maneno.Pamoja na kuongoza ligi kwa sasa, bado ameendelea kudai kuwa timu yake haiko kwenye mbio za ubingwa na ushindi wake dhidi ya Spurs mwishoni mwa juma, ilikuwa ni kuwahakikishia nafasi ya kumaliza ndani ya timu nne za juu. Mourinho bado hajapoteza mchezo wowote wa ligi kuu anapocheza uwanja wa nyumbani pale Stanfford Bridge tangu msimu wake wa kwanza wa 2005/2006 mpaka leo. Huyu mwanaume anachofanya hapa ni kuwaondolea presha wachezaji wake ili waone hata wanapoukosa ubingwa,sio tatizo huku akiwawashia moto Arsenal na Manchester city ambao wanaonekana kucheza kwa presha ya kutaka ubingwa bila kumsahau Liverpool ambaye pengine wengi hawampi nafasi.

Kuna muda mwingine hutakiwi kuamini sana maneno ya Mourinho, baada ya kulazimishwa sare tasa pale Stanfford Bridge na West Ham United ambao walionekana kutumia mbinu ya "kupaki Bus" aliibuka na kusema kuwa wanacheza soka la karne ya 19! Kauli hii ni wazi kuwa Mourinho anahitaji pointi 3 kwenye kila mchezo ili ikiwezekana apate ubingwa mwishoni mwa msimu huu ingawa ameendelea kukanusha jambo hilo.

Wenzetu Ulaya wachezaji ndiyo wanaolipwa fedha nyingi kuliko makocha, tofauti na hapa kwetu Tanzania ambapo ni kinyume chake. Mourinho ni kocha anayesifika kwa kutengeneza nidhamu ndani ya timu na haoni tabu kumuwajibisha nyota yoyote kwenye kikosi chake. Wakati akiwa Real Madrid, kipa na nahodha wa timu hiyo Iker Cassilas, beki mreno mwenzie Pepe na Sergio Ramos kwa nyakati tofauti,walikutana na rugu la Mourinho.

Eden Hazard kwa sasa ndiye tegemeo kwenye kikosi cha Chelsea lakini kutokana na utovu wake wa nidhamu, Mourinho alimuacha nje Star huyo kwenye mechi ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Schalke 04. Ashley Cole naye aliachwa nje kwenye mchezo dhidi ya Arsenal baada ya kugundulika kuwa beki huyo alionekana siku chache kabla ya mchezo huo akiserebuka disco na baadhi ya wachezaji wa Arsenal. Hivi unamjua Mourinho au Unamsikia?

Jose Mourinho ni aina ya kocha ambaye kila shabiki wa soka, angependa aifundishe timu anayoshabikia. Mourinho ni mpiganaji na siku zote anawaza ushindi.Unapokuwa na Mourinho siku zote unakuwa na roho ya upambanaji huku ukiamini ushindi unapatikana muda wowote. Namuheshimu sana Sir Alex Ferguson, Juup Heynches, Pep Gaudiola, Arsene Wenger, Carlo Ancelloti na makocha wengine wenye historia kwa nyakati hizi lakini, Jose Mourinho ni kocha wa sayari nyingine.

6 comments:

  1. Nimekubali shafii japo tunamchukia tu lakini mourinho ndio kocha bora duniani mi ninavyoona.

    ReplyDelete
  2. Oscar Jr anaonesha ni mnazi wa Chelsea na wakati kama huu timu iko kwenye peak anaandika makala hii kwa mbwembwe. Mourinho ni egotistic sifa zimemjaa sana ndicho kilicho mfanya ashindwe Real anataka aabudiwe, Spain wanaabudu mpira.Alishindwana na wachezaji na uongozi Real sababu yeye alitaka kuleta mpira wake ambao haukua na faida kwa wachezaji wala longrun profit maximisation ya team.Technically Mourinho ni kocha wa msimu meaning akiondoka na timu inakufa especially timu zinazocheza mpira wake. Ameongelea Barca ya 2010 na 11 kama ilikua kwenye peak nadhani kwa mtazamaji mzuri wa mpira anajua fika baka ilianza kufa 2010. Mwandishi anaonekana fika si mfatiliaji wa ligi ya Spain na Real kwa ujumla.Kwa mpira wa uingereza kila mtu anajua kua msimu huu EPL haina msisimko wa kutosha kama miaka mengine timu hapa naongelea timu kama Arsenal,Liverpool,Chelsea,Man UTD,Man City ukiangalia zote zmepoteza au ku draw mechi nyingi ambazo kwa timu walizokua nazo ni ngumu kupoteza.Article imejaa unazi zaidi ya kutuonesha ubora wa Mourinho.Mwandishi ana caliber ya Mourinho 100%

    ReplyDelete
  3. Sina shaka na Chelsea kunyakuwa kikombe cha EPL na nategemea wataishangaza tena dunia kwenye michuano ya UCL

    ReplyDelete
  4. Jose sio kocha anadili na master tu hawezi kutengeneza mastaa kama wenzie kama Wenger halafu mzee wa kupaki gari na makontena mshereshaji kama Julio wa simba ya Tanzania.

    ReplyDelete
  5. Si aende huko kwenye sayari nyingine basi

    ReplyDelete
  6. Jose bonge la kocha but sijawai kutamani aje kufundisha timu ndayo.kwasababu sifurahishi na style ya ufundishaji wake.

    ReplyDelete